Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Mahakama yaelezwa Ditopile alivyoua
Mahakama yaelezwa Ditopile alivyoua
By Habari Tanzania | Published  02/16/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:

Andrew Msechu na Tausi Ally

UPANDE wa mashitaka katika kesi ya mauaji inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Ditopile Mzuzuri, jana ulitoa maelezo ya mashahidi 23 wa upande wa mashitaka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Katika maelezo ya mashahidi hao ambao watasimama dhidi ya Ditopile wakati kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania, walieleza namna tukio zima la mauaji ya dereva wa daladala Hasani Mbonde, anayedaiwa kuuawa na Ditopile lilivyotokea.

Kwa mujibu wa maelezo hayo yaliyosomwa na jopo la waendesha mashitaka watano likiongozwa na Mratibu Mwandamizi wa Polisi, Germanus Mhume, mbele ya Hakimu Michael Luguru, mashahidi hao wameeleza jinsi tukio zima lilivyotokea baada ya kutokea kutoelewana kati ya Ditopile na dereva huyo wa daladala.

Kati ya maelezo ya ushahidi ya mashahidi hao yamo ya Kamishna wa Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam, Alfred Tibaigana na Abdallah Msika ambao wanaeleza namna mtuhumiwa alivyohusika katika tukio hilo la mauaji na kuonyesha majuto yake.

Mhume akisoma maelezo ya Kamanda Tibaigana, alidai kuwa siku ya tukio majira ya saa saba usiku, Naibu Kamishna wa Polisi, Abdallah Msika, alimpigia simu na majira ya saa nane usiku alifika nyumbani kwake akiwa ameongozana na Ditopile.

Aliendelea kueleza kuwa baada ya kuwaona na kuwasalimia alimuita Mkuu huyo mheshimiwa ambaye katika hali ya kuchanganyikiwa alikanusha kuitwa hivyo huku akimwambia “mimi si mheshimwa tena, mimi ni muuaji, maskini nimepoteza muda wangu wote wa kazi bure.”

Alidai kuwa baada ya Ditopile kumsimulia matatizo yaliyomkuta, aliamuru baadhi ya viongozi wa Jeshi la Polisi kumshikilia mtuhumiwa huyo kwa ajili ya uchunguzi wa tukio hilo la mauaji na kukamilisha taratibu za kisheria.

Naye Msika alidai kuwa siku hiyo hiyo, Ditopile alimpigia simu akimtaka waonane kwa kuwa ana tatizo kubwa lililomsibu na anataka amsaidie.

Alidai baada ya taarifa hiyo Ditopile alimuuliza kama anataarifa zozote juu ya tukio la mauaji lilitokea jioni ya Novemba 4, mwaka jana katika njia panda ya Kawe na kumthibishia kwamba tayari Polisi wanamtafuta mhusika alimjulisha kuwa yeye ndiye anayehusika na kumtaka waonane ili amueleze kwa undani na alifanya hivyo.

“Nilishtuka kusikia hivyo na nilitaka kuonana naye, lakini aliniambia kwamba yupo njiani akitokea Bagamoyo kurejea Dar es Salaam,” alidai katika maelezo hayo.

Msika alidai kuwa alikwenda nyumbani kwa Ditopile majira ya saa tano usiku na kuonana naye, ambako alimueleza bayana namna alivyo fanya mauaji hayo huku akimuonyesha mkono aliojuruhiwa baada ya kushambuliwa katika eneo la tukio na baadaye kumpeleka nyumbani kwa Kamanda Tibaigana.

Katika maelezo hayo ya ushahidi mashuhuda wanne waliokuwapo katika eneo la tukio akiwamo dereva msaidizi wa marehemu Mbonde, inadaiwa kuwa katika gari la mtuhumiwa kulikuwa na watu watatu akiwamo mwanamke mmoja aliyevali nguo aina ya Kanga Kavu.

Waliendelea kudai kuwa mtuhumiwa, baada ya gari lake kugongwa na kushuka, aliwatishia watu watatu akiwamo dereva wa pili wa gari hilo ambaye pia alimpiga makofi mawili na hatimaye kurudi kwa kondakta na abiria aliyekuwa nyuma ya kiti cha marehemu ambaye baada ya kupendekeza waende polisi, alitolewa lugha chafu na mtuhumiwa huyo huku akitishia kutoboa tairi za gari kwa kutumia bastola.

Hata hivyo, kabla ya kutokea kwa mauaji, dereva aligoma kushuka kwa kuwa gari lake lilikuwa halina breki akidai linaweza kuserereka na kusababisha ajali na kuwadhuru abiria wake kwa kuwa kulikuwa na msongamano wa magari.

Baada ya dereva kusema maneno hayo, mtuhumiwa alizungumza kwa dharau akidai kuwa "inamaana abiria wako wanathamani kuliko gari langu," "unajua thamani ya gari wewe’," alidai abiria aliyekuwa amekaa nyuma ya kiti cha dereva na kuongeza kudai kwamba aliangukiwa na mwili wa marehemu Mbonde miguuni mara baada ya kupigwa risasi.

Mashahidi wengine watatu ambao ni dereva wa mtuhumiwa, ndugu wa mtuhumia aliyejulikana kwa jina la Mzee Twaha na mtuhumiwa mwenyewe walidai kuwa siku ya tukio walikuwamo wao watatu tu ndani ya gari hiyo.

Baada ya kumaliza kusoma maelezo hayo ya awali, Muhume alidai vitakavyotumika katika ushahidi wa kesi hiyo mara itakapoanza kusikilizwa katika Mahakama Kuu ni taarifa ya uchunguzi wa mwili wa marehemu, maelezo ya ungamo la mtuhumiwa, ramani ya eneo la tukio, fomu za gwaride la utambulisho, na taarifa ya uchunguzi ya milipuko.

Kwa upande wake Ditopile kupitia maelezo yake kama yalivyoandikwa na ASP Sabasi na kusomwa mahakamani na Mhume mbele ya Hakimu Luguru, alidai kuwa mara baada ya marehemu Mbonde kugonga gari lake alimtaka ashuke chini ili aweze kumpeleka katika kituo cha polisi.

Alidai kuwa dereva huyo aligoma kushuka huku akimwambia 'imetoka hiyo' na kisha akamsonya na alipokuwa akigonga kioo kidogo cha mlango wa basi aina ya Isuzu Journey, alishtuka baada ya kugundua kuwa risasi imefyatuka na kumpiga kichwani dereva huyo.

Baada ya kuona hali hiyo, aliingia ndani ya gari hilo kwa kupitia mlango wa abiria na kuomba msaada kwa abiria waliokuwamo ndani ya gari hilo ili aweze kumpeleka majeruhi hospitali.

Aliendelea kudai kuwa abiria waligoma kutoa msaada na kumtaka ambebe mwenyewe kwa kuwa yeye ndiye aliyemuua huku wakimshambulia hali iliyomlazimu kutoa magazini ya bastola iliyokuwa na risasi tano ili isiweze kufyatuka tena.

Alichukua magazini hizo na kuziweka mfukoni na bastola kiunoni huku akitafuta namna ya kuondoka katika eneo hilo baada ya kujeruhiwa mkononi kwa chuma kwa kuwa aliona maisha yake yako hatarini.

Aliendelea kueleza kwamba baada ya tukio hilo, alikimbilia Bagamoyo kwa nia ya kusubiri kundi la watu litawanyike katika eneo la tukio na baadaye alimua kujisalimisha kwa Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi nchini, Abdallah Msika.

Awali jopo la mawakili watano wanaomtetea mtuhumiwa huyo likiongozwa na Nimrod Mkono, liliiomba mahakama impatie dhamana mteja wao kwa kuwa kosa linomkabili sasa ni mauaji ya bila kukusudia na linadhaminika kisheria.

Ombi hilo lilikuja mahakamani hapo mara tu baada ya upande wa mashitaka kusoma hati mpya ya mashitaka ya kuua bila kukusudia badala ya ile ya awali ya mauaji.

Baada ya ombi hilo, kutolewa Hakimu Luguru alisema baada ya kupitia hoja zote za msingi kutoka kwa mawakili hao wa upande wa utetezi, kwa maoni yake ni kwamba mahakama ya Kisutu bado haina uwezo wa kutoa dhamana hadi Mahakama Kuu ya Tanzania.

Wakati hayo yote yakiendelea mahakamani hapo, Ditopile ambaye alisimama kizimbani kwa muda wa saa tatu mfululizo alionekana mwenye huzuni huku akitoka na machozi, hususani wakati akisomewa maelezo ya ushahidi ya mashahidi 23 ambao wanatarajia kutoa ushahidi katika kesi hiyo.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by captain)
    Rating
    baada ya kusoma maelezo ya habari ya kesi ya bw. ditopile kupitia kwenye mtandao,kwa kweli inasikitisha kuona kwamba sheria inapotoshwa kutokana namuelekeo wa kesi unavyokwenda.bw.ditopile amekuwa si muuwaji tena badala yake ameuwa bila kukusudia?huu ukiritimba wa kulindana waheshimiwa utakwisha lini?hata asipopewa haki yake marehemu mbonde. bw. dito ni muuwajı tu
     
Submit Comment


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.