Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Mvua yazua maafa Tanga, Moro
Mvua yazua maafa Tanga, Moro
By Habari Tanzania | Published  02/15/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
Na Waandishi Wetu, Moro na Tanga

MVUA zinazoendelea kunyesha nchini, zimeanza kusababisha maafa baada ya nyumba kadhaa kubomoka na nyingine kuezuliwa mapaa katika mikoa ya Tanga na Morogoro.

Wilaya zilizoathirika zaidi mkoani Tanga ni Korogwe na Pangani, wakati mvua hizo pia zimepeleka kilio katika Wilaya ya Momero mkoani Morogoro.

Wilayani Korogwe, zaidi ya wakazi 224 wa vijiji viwili, hawana mahali pa kuishi baada ya nyumba 59 na madarasa matatu kuezuliwa kutokana na mvua kubwa zilizonyesha ambazo ziliambatana na upepo mkali.

Wakazi wa Korogwe wanasema kuwa upepo huo huenda ulitokana na kimbunga maarufu kwa jina la Bondo ambacho kimekuwa kikisambaza upepo mkali kutokea katika Bahari ya Hindi.

Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Betty Mkwasa, zinasema kimbunga hicho kilizuka Jumapili iliyopita katika vijiji vya Lwengela Darajani na Lwengela Relini vilivyopo Kata ya Old Korogwe, pamoja na kitogoji cha Majengo mjini Korogwe.

Katika Kijiji cha Lwengela Darajani, nyumba 22 ziliezuliwa na upepo huo wakati nyingine 10 zilibomolewa. Pia vyumba vitatu vya madarasa ya katika Shule ya Msingi Lwengela Darajani viliezuliwa mapaa.

Kijiji cha Lwengela Relini, nyumba 34 ziliezuliwa mapaa kutokana na kimbunga hicho kilichozuka majira ya saa 7.40 mchana na kusababisha wananchi kukimbia kwa hofu. Katika Kitongoji cha Majengo, nyumba tatu ziliezuliwa mapaa.

“Kimbunga kiliambatana na mvua kubwa na kusababisha kijiji chote kuwa katika giza nene nyakati za mchana, jambo liliotutia hofu tukadhani ni mwisho wa dunia,” alisema Mwajuma Dafa, mkazi wa Lwengera Relini.

Mkwasa alisema kutokana na kimbunga hicho, jumla ya wanafunzi 135 wa Shule ya Msingi Lwengela Darajani walilazimika kukosa masomo kwa siku mbili hadi serikali wilaya ilipofanya jitihada za kuweka madarasa ya muda.

Mkuu huyo wa Wilaya alisema watu waliokosa mahali pa kuishi baada ya nyumba zao kuezuliwa mapaa na baadhi kubomolewa, wamehifadhiwa na jirani zao na jitihada zinafanyika kuezeka nyumba zilizoezuliwa na kubomoka.

Katika Wilaya ya Pangani, nyumba 25, yakiwamo makanisa mawili ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) katika kata za Mkalamo na Kipumbwi, zimeezuliwa na upepo mkali ulioambatana mvua na kusababisha wananchi kukosa makazi na mmoja kuvunjika mbavu.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Zipora Pangani, ni kuwa upepo huo ulitokea juzi Jumapili katika vijiji vya Kwakibuyu kilichopo Kata ya Mkalamo na Kipumbwi.

Zipora alisema upepo huo ambao ulivuma kwa dakika tatu majira ya saa 9.30 alasiri, pia uliezua paa la zahanati ya Kijiji cha Mkalamo na kuharibu vifaa vya umeme wa jua, vyote vikiwa na thamani ya Sh4,360,900.

Majengo mengine yaliyoathirika katika Kijiji hicho ni pamoja na makanisa mawili ya Lutheran na nyumba 12 zilizoezekwa kwa bati na nyingine 13 zilizoezekwa kwa makuti.

Kwa upande wa Kijiji cha Kwakibuyu, Mkuu wa Wilaya alisema kimbunga kiliezua jumla ya nyumba 18, likiwamo Kanisa.

Alitaja athari zilizotokana na upepo huo kuwa ni pamoja na kuanguka kwa nguzo za umeme na kuumia kwa mtu mmoja, aliyemtaja kwa jina la Asha Rashid, ambaye amevumnjika ubavu mmoja wa kulia.

Zipora alisema kutokana na janga hilo, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo imeanza kuchukua hatua mbalimbali za kuwahakikishia usalama waathirika na akaomba watu kutoka maeneo mbalimbali kujitokeza kuwasaidia.

“Hawa waathirika wamekuwa wakihifadhiwa na ndugu na jamaa, hali ni mbaya tunaomba asasi na watu mbalimbali wajitokeze kuwasaidia kwa hali na mali,” alisema.

Wilayani Mvomero, familia kadhaa hazina mahali pa kuishi baada ya nyumba zao kuezuliwa na upepo mkali wiki iliyopita.

Wakizungunza na waandishi wa habari waliotembelea baadhi ya nyumba zilizoathirika katika Kijiji cha Mgudeni, wananchi walisema siku ya tukio majira ya saa 10.00 Jioni, upepo ulivuma kwa kasi kubwa na kuvunja miti pamoja na kung'oa mapaa ya nyumba.

"Hakuna aliyejeruhiwa, lakini sasa tunalazimika kulala wazi kwa kuwa hatuna uwezo wa kununua mabati, mbao, misumari na fedha za kuwalipa mafundi kuezeka," alisema Iddi Ali, mmoja wa watu walioathirika na upepo huo. Ali ana familia ya watu watano.

Afisa Mtendaji wa Kijiji, Mussa Kinye, alisema upepo huo ambao kawaida hutokea mwezi Januari kila mwaka na kuathiri nyumba mbalimbali, ulitokea Januari 28.

Baadhi ya watu walioathirika na upepo huo ambao nyumba zao zimeezuliwa mapaa ni Kwembe Ismail, Henry John, Iddi Ally, Sefu Abdallah, Shaban Ouki na Hamisi Omari wote wakazi wa kijiji hicho.

Awali Katibu Tarafa wa Mvomero, John Mtolela, alisema uongozi wa tarafa hiyo umewaagiza wanakikijiji kupanda miti ya aina mbalimbali ikiwemo ya matunda na Mbao ili kuzuia upepo huo.

Mtolela alisema eneo kubwa kilipo kijiji hicho kuna ukanda usiokuwa na miti ya kutosha kudhibiti kasi ya upepo ambao umekuwa ukisababisha athari kama hizo kila mwaka.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Hawa Ng'humbi, alikiri kupata taarifa za maafa hayo na akasema serikali imeagiza uongozi wa tarafa kuandaa tathmini ya hasara iliyojitokeza.

Januari mwaka jana, wanafunzi wa shule ya Msingi Mgudeni, walinusurika kufa baada ya upepo mkali kuezua paa la shule na kulitupa mbali.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.