Na Midraji Ibrahim
UKIUKWAJI wa taratibu za matumizi ya fedha za serikali, ikiwamo kutoa zabuni bila kuzingatia taratibu za manunuzi, umelifanya Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE), kupata hati chafu ya ukaguzi wa mahesabu ya mwaka 2005/06.
Ripoti ya ukaguzi wa mahesabu ya DSE uliofanywa na Shirika la Ugaguzi wa Hesabu (TAC), inaonyesha kwa matumizi ya Sh74,585,797 yaliyotumika kuwalipa watu mbalimbali waliotoa huduma, hayakufuata taratibu za ununuzi wa vifaa na huduma.
"Kwa mfano mwaka 2006/07, zabuni tatu kati ya 12 za kusambaza vifaa ndizo zilizotangazwa kuwa zinashindanishwa. Tunakupa mfano mdogo wa kampuni zilizoshinda zabuni hizo (majina tunayo)," inasema ripoti.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa katika utetezi wake, menejimenti ilisema mfumo huo ulitumiwa kwa ajili ya kupata vifaa na huduma bora, maelezo ambayo yanapingwa na wakaguzi wa hesabu kuwa yanakosa mhimili wa kuyasimamia kulingana na Sheria ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma.
"Kwa mazingira haya, tumeshindwa kuelewa iwapo kampuni ilitoa zabuni kwa watu wenye uwezo, vile vile, tumeshindwa kujiridhisha kwa iliyoandikwa kwenye bei ya mkataba kwa ajili ya utengenezaji wa ofisi na utoaji huduma kama ilikuwa ya ushindani," inasema sehemu ya taarifa hiyo.
Ripoti hiyo inasema, hakuna sehemu ambako imeandikwa kwa sera ya DSE kwamba, itatumia utaratibu huo. Kulingana na kanuni za zabuni, mfumo huo unaweza kutumika iwapo kampuni husika ndio pekee inayotoa huduma hiyo.
Vile vile, ripoti hiyo ya TAC inabainisha kuwepo kwa udhaifu katika matumizi ya magari ya kampuni. Mwaka 2005/06, Sh1,522,097 zilitumika kwa ajili ya mafuta ya magari na matengenezo, ikiwa ni zaidi ya bajeti ya Sh21,845,000.
"Vile vile, tumebaini kipindi cha mwaka 2005/06, Sh4,392,765 zilitumika kununua mafuta na kufanya matengenezo ya gari la Mtendaji Mkuu," inasema ripoti hiyo na kuongeza kuwa, kati ya Julai 2005 na Oktoba 2006, Mtendaji Mkuu alilipwa fedha za mafuta Sh3,930,000.
Inaonyesha gharama za mafuta na matengenezo ya gari la Mtendaji Mkuu, ziliongezeka na kufikia Sh8,322,765 kwa mwezi.
Kutokana na mkataba wa ajira wa Mtendaji Mkuu kukaa kimya kuhusu matumizi ya magari ya kampuni, kulipwa kwake Sh230,000 za mafuta kwa mwezi (lita 300), wakaguzi wamesema sio rahisi kufahamu ukomo wake wa matumizi ya magari.
Ripoti ya hesabu inaonyesha Mtendaji Mkuu, anatumia kilomita 50 kila siku kwa gari la kampuni kufanyia shughuli zake nje ya ofisi.
"Tumegundua mwaka 2005/06, Mtendaji Mkuu amelipwa mara mbili mafao ya likizo, kinyume na kanuni za wafanyakazi za mwaka 1999, kifungu namba 38 (a) (i) na (iii)," inasema na kuongeza:
"Tumebaini kuwa, likizo ya pili aliyolipwa wamejaribu kuigeuza kuwa amelipwa mafao ya likizo inayofuata kabla, kinyume na mkataba wa ajira na kanuni za fedha za mwaka 1999."
Taarifa ya ukaguzi inaonyesha zaidi ya Sh16 milioni zililipwa na DSE kwa ajili ya simu za mikononi kwa maafisa watano, ilhali hakuna bajeti iliyoidhinishwa na mamlaka husika kwa huduma hiyo, huku ankara za zaidi ya Sh4 milioni zikisubiri kulipwa.
"Kwa ujumla DSE kuna upuuzaji wa udhibiti na maadili ya wafanyakazi kama unavyoainishwa kifungu 3.0 na 5.5. Kifungu kinaelekeza kila mfanyakazi wa DSE katika kiwango cha menejimenti jinsi anavyotakiwa kuwa makini na matumizi wakati akiwa kazini," inasema.
Kulingana na mchanganuo wa mapato ya kampuni kwa miaka miwili, hayatoshelezi matumizi, huku ikibainishwa kuwa mwaka 2005/06 ilipata hasara ya Sh76.4 milioni na mwaka 2004/05, ilipata hasara ya Sh113.4 milioni.
Upungufu mwingine ambao umebainishwa ni kutokuwepo kwa kitabu cha orodha ya mali ya kampuni, udhibiti wa ununuzi wa vifaa na kwamba, hata vifaa vipya vilivyopo havijawekewa alama ambazo zinaweza kusaidia kuvidhibiti.
Tathmini iliyofanywa inaonyesha kwamba kukosekana kwa kitengo cha ukaguzi wa mahesabu wa ndani ambacho kisheria kinapaswa kuwepo, ndiyo chanzo kikuu cha matatizo hayo.
Alipoulizwa Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DSE, Isabela Komba, kuhusu tuhuma hizo, alisema hadi sasa bodi haijakaa kupitia ripoti hiyo, hivyo ni vigumu kueleza nini kilichomo.
Komba alisema bodi ndio imetoa kazi ya kufanya ukaguzi na kwamba matokeo yake, ushauri na jinsi ya kufanya, lazima kwanza bodi ikae ndipo ripoti itatolewa hadharani.
Alisema hadi sasa ripoti ya mwaka ya DSE haijatolewa na kuongeza kuwa, maandalizi yaliyopo sasa ni ya kufanya mkutano wa bodi ambao hata hivyo, alisita kutaja tarehe rasmi.