Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Mashoga wapiga kambi mkutano wa maaskofu Dar
Mashoga wapiga kambi mkutano wa maaskofu Dar
By Habari Tanzania | Published  02/15/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
Na Simon Berege
WAWAKILISHI wa wanaharakati wa kimataifa wa kutetea haki za mashoga na wasagaji ndani ya kanisa la Kianglikana, wamefanikiwa kuweka kambi katika hoteli ya Whitesands ya jijiji Dar es Salaam, eneo linalotumiwa na maaskofu wakuu wa kanisa hilo duniani kujadili mambo mbalimbali yanayolihusu kanisa.

Kama ilivyo kwa wanaharakati hao, pia wawakilishi wa vikundi vya kimataifa vinavyopinga ushoga na usagaji ndani ya kanisa, nao wamefanikiwa kupata malazi katika hoteli hiyo, wakiongozwa na Askofu Martin Minns kutoka taasisi ya Marekani iitwayo White English Priest. Kila kikundi kimekuwa kikijitahidi kufanya ushawishi wa viongozi hao wa kanisa kuunga mkono upande wao.

Wakati hayo yakitokea, Mkuu wa kanisa hilo duniani, Askofu Mkuu wa Canterbury, Rowan Williams, jana alikuwa na mkutano wa ndani na maaskofu wakuu wapya 11 wanaohudhuria mkutano huo kwa mara ya kwanza tangu kuwekwa wakfu, akiwemo Askofu Mkuu wa kanisa hilo nchini Marekani, Katherine Schori ambaye ni mwanamke wa kwanza kupewa wadhifa huo nchini humo.

"Tumekuja kuwashawishi viongozi wetu wa kiroho wasikie sauti yetu na kuzingatia haki za mashoga na wasagaji ndani ya kanisa, kwani kuwepo kwao katika kanisa hakuna madhara yoyote " alieleza Mchungaji Colin Coward wa kanisa hilo kutoka Uingereza, ambaye ni Mkurugenzi wa taasisi ya kuhamasisha mabadiliko chanya ya kimtazamo juu ya ushoga na usagaji ndani ya kanisa la Anglikana.

Akizungumza na Mwananchi hotelini hapo jana, Mchungaji Coward alisema tayari wawakilishi wanne kutoka nchi mbalimbali duniani wapo hotelini hapo kuhakikisha wanafanikiwa kutetea haki za waumini hao kutokana na maslahi yao kuwa matatani hasa baada ya kuongezeka kwa harakati za kuwapinga mashoga ndani ya kanisa hilo.

Mchungaji huyo alisema tayari alishafanikiwa kuonana na maaskofu watatu ambao wamesikiliza hoja yake kwa makini na kwamba yeye na wenzake wataendelea kubaki hotelini hapo hadi mkutano huo utakapokwisha kwa lengo la kufanikisha azima yao.

"Tunajua mabadiliko hayawezi kutokea kwenye kikao hiki lakini itakuwa hatua muhimu ya kufikia malengo yetu ya kutetea kundi letu lisilona hatia," alisema Mchingaji Coward na kuwataja wenzake walio nchi hapa kwa shughuli hiyo kuwa ni pamoja na Scot anayetokea inclusive church na Caro wote wakitokea nchini Marekani na Davis Mac-Lyalla kutoka Nigeria.

Wakati hayo yakitokea, Mkurugenzi wa Mawasiliano kutoka makao makuu ya kanisa hilo, James Rosenthal, alisema Askofu Mkuu wa Nigeria, Peter Akinola, amewasilisha barua kwa Askofu Mkuu wa Canterbury, Rowan Williams, ingawa bado maelezo yaliyo katika barua hiyo hayajawekwa wazi.
Mwandishi wa gazeti hili alipata wasaa mfupi wa kuzungumza na Askofu Akinola akiwa katika gari maalum ya kubebea wageni hotelini hapo, ambaye alikiri kuwasilisha barua hiyo kwa mkuu wa kanisa ingawa yaliyomo katika barua hiyo bado ni siri kati yake na Askofu Mkuu.

"Hadi sasa hii barua ni suala la mimi na yeye ila kama itastahili kuwekwa mbele ya vyombo vya habari basi watu wetu watawapatia" alieleza Askofu huyo na kuondoka. Mikutano hiyo inafanyika kwa usiri mkubwa chini ya ulinzi mkali.

Hata hivyo kati ya waliomlaki Askofu huyo kwenye lango la kuingilia hotelini hapo alikuwa Mkurugenzi wa kutetea haki za Mashoga na Wasagaji kutoka nchini Nigeria, Davis Mac-Lyalla ambaye naye ameweka kambi hotelini hapo kwa lengo la kushawishi maaskofu kusaidia kusitisha mchakato wa kuanzisha sheria ya kupinga ushoga na usagaji nchini Nigeria.

Askofu Akinola ndiye aliye mstari wa mbele kupinga ushoga ndani ya kanisa hilo na ameshawahi kukaririwa akitishia nchi yake na Afrika kwa ujumla kujitenga kutoka katika kanisa hilo endapo ushoga hautapigwa vita ndani ya kanisa.

Alipoiona sura ya Mac-Lyalla, Askofu Akinola alimhoji alichofuata jijini hapa na kama amealikwa ambapo alimjibu kwamba hajaalikwa lakini amefika kuwasilisha ujumbe mahsusi.

Akizungumza na wanahabari hotelini hapo, Mac-Lyalla alisema tayari wameshaandika waraka kwenda kwa maaskofu wakuu wanaofanya kikao hotelini hapo kwa lengo la kuwaomba waishawishi serikali ya Nigeria kusitisha mchakato wa mswaada wa sheria ya kupinga ushoga ulioanza kujadiliwa na Bunge la nchi hiyo jana.

Alisema endapo sheria hiyo itapita, kuna hatari kwa familia nyingi kuathirika kwani kifungo kilichopendekezwa kwa watu watakaothibitika kujihusisha na ushoga ama usagaji nchini humo ni kati ya miaka mitano hadi 14.

"Kuwepo kwetu katika kanisa hakuna shida yoyote kwani hata wanawake wengi Nigeria hawaogopi kusikia mume wake akiwa na mahusiano na mwanaume mwenzie kwani hawezi kuzaa na kuanzisha familia mpya," alisema Mac-Lyalla.

Mkutano huo unatajwa kuwa mzito kwani unaweza kuweka historia mpya ya kanisa hilo kutokana na madai ya kuwepo kwa kundi la maaskofu wakuu 20 kati ya 38 wanaoongozwa na Askofu Akinola wanaotaka kanisa hilo kutoa msimamo wake juu ya ushoga, hasa baada ya kanisa la Marekani kukubali kumtawaza, Gene Robinson kuwa Askofu mbali na kujitangaza hadharani kuwa ni shoga.

Kundi la maaskofu hao pia linampinga Askofu Mkuu mwanamke wa kanisa hilo nchini Marekani, Katherine Schori ambaye ameonyesha msimamo wa kumuunga mkono Askofu Robinson.

Askofu Mkuu Schori ni miongoni mwa maaskofu wanaohudhuria mkutano huo wa Whitesands, lakini Askofu Robinson hayupo katika mkutano huu kwa kuwa yeye si Askofu Mkuu.

Wachambuzi wa mambo wanaeleza kwamba Askofu Schori ambaye ni mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo nchini humo, anaweza kukumbana na makali ya Askofu Akinola kwenye mkutano wao unaoanza leo huku pia kukiwa na taarifa za kuwepo kwa maaskofu waliopanga kumnyanyapaa.

Baadhi ya maaskofu wa kanisa hilo walivunja uhusiano yao na kanisa la Marekani baada ya kukubali kumtawaza kasisi aliyejitangaza kuwa Shoga kuwa Askofu pamoja na kuruhusu ndoa za watu wa jinsia moja.

How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.