Mishahara kupandishwa ni mwanzo tu
Na Maura Mwingira, Babati
RAIS Jakaya Kikwete, amewaahidi Watanzania kwamba mambo mazuri yanakuja, baada ya kuboresha mishahara ya watumishi wa umma katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha.
Akihutubia kwenye mkutano wa hadhara mjini hapa jana, kuwashukuru wananchi kwa kumchagua kuwa Rais wa Jamhuri, Rais Kikwete alisema maboresho yatakuwa mazuri zaidi, baada ya kukamilika kazi ya tume aliyounda kupitia mishahara ya watumishi wa umma na kutoa mapendekezo.
Rais aliahidi kutekeleza ahadi alizotoa kwenye kampeni, akisema kwamba ni za kweli, hazikuwa danganya toto na kwamba Watanzania si mabwege wa kudanganywa, kwani wameamka.
Aliahidi maisha bora kwa kila Mtanzania, ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma za kijamii na kuweka mazingira mazuri ya kujiajiri na kujiongezea kipato. Alisisitiza ujenzi wa barabara kwa lami kutoka Minjingu hadi Singida kuanza mwaka huu wa fedha na barabara ya kutoka Babati - Kondoa - Dodoma na ile itakayounganisha makao makuu ya mkoa yenye urefu wa kilometa 250.
Akigeukia rushwa na tabia mbaya za watumishi wa umma, Rais Kikwete alisema hakuna maelezo sahihi ya kuielezea rushwa, zaidi ya kuwa rushwa ni "haramu haramu haramu!" na kuongeza kuwa, watumishi wengi wa umma wamekuwa wakiomba na kupokea rushwa kwa kisingizio kwamba mishahara wanayopata ni midogo na haikidhi haja.
Rais alisema kuna watumishi wanaotekeleza majukumu yao kana kwamba hawajaenda shule, kwa kutoa uamuzi unaokwenda kinyume cha taaluma zao, na kuwalazimisha wananchi kutoa rushwa kwa huduma wanazotakiwa wazitoe bure. Alisema ataendelea kuwakumbusha kutekeleza wajibu kwa kuzingatia taaluma walizosomea.
Alisisitiza kwamba, ifike mahali watumishi wa umma waachane na tabia ya kuwaambia wananchi 'nenda rudi kesho' bila kutoa majibu sahihi, akaongeza kwamba watumishi wote wa umma wako katika nafasi zao za kazi kwa ajili ya kuwatumikia wananchi na kusukuma maendeleo yao .