Na Ally Sonda, Moshi
BODI ya Chama cha Ushirika cha Msingi Kirima Boro, katika Jimbo la Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro, kinatuhumiwa kukwamisha juhudi za Mbunge wake, Dk Cyrill Chami, kujenga Kiwanda cha Ngozi.
Tuhuma hizo zilifichuka juzi kwenye mkutano maalumu ulioitishwa na Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika, Mkoa wa Kilimanjaro, Kasya Kasya.
Katika Mkutano huo uliofanyika nje ya ofisi za chama hicho zilizopo katika Kata ya Kirima, wanachama walidai kuwa Bodi ya chama hicho imegoma bila sababu yoyote kutoa eneo la hekari 40 kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda hicho kutoka kwenye shamba la Kahawa Estate, linalomilikiwa na chama hicho.
Ilielezwa kuwa Dk Chami ambaye ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, alimpata mwekezaji wa kujenga Kiwanda cha Ngozi na kwamba tayari mwekezaji huyo kutoka nje ya Afrika, aliridhia kujenga kiwanda kwenye shamba hilo ambalo hivi sasa viongozi Bodi ya chama hicho wanagoma kulitoa.
Walisema licha ya Mkutano Mkuu wa Ushirika uliokutana mwaka jana kuamua kuwa hekari hizo zitengwe kwa ajili ya kumkabidhi mwekezaji, aliyetafutwa na mbunge wao kwa lengo la kuongeza ajira na kuboresha pato la taifa, mpaka sasa Bodi haijatekeleza maamuzi hayo.
Kutokana na hali hiyo, wanachama walimweleza Mrajisi Msaidizi kuiagiza Bodi hiyo kwamba ifikapo Februari 28, mwaka huu iwe imelitoa eneo tayari kukabidhiwa kwa mwekezaji kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Kiwanda chake.
Akizungumza katika Mkutano huo, uliohudhuriwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Stewart Lyatuu na baadhi ya madiwani, Mrajisi Msaidizi aliwataka wanachama kuwa makini na baadhi ya viongozi wasioheshimu maamuzi halali ya wanachama.
Mrajis Msaidizi huyo aliwaagiza kwa viongozi wote wa vyama vya ushirika mkoani hapa kuheshimu na kuyatekeleza maamuzi mbalimbali ya kimaendeleo yanayoamuliwa na mikutano mikuu ya vyama vyao ili kuepuka migogoro inayosababishwa na ubabe wa viongozi.
Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Muhidin Komu na baadhi ya wajumbe walijitetea kuwa hakuna Mkutano Mkuu ulioagiza ushirika utoe hekari 40 kwa ajili ya Kiwanda cha Ngozi na pia hawajawahi kuweka mipango ya kumhujumu Mbunge wao, majibu ambayo yalisababisha wanachama kuwazomea na kumtaka Mwenyekiti huyo akae chini.