Na Mwandishi Wetu, Singida
SERIKALI imeinyang'anya Kampuni ya Sietco eneo la urefu wa kiliomita 30 mkoani Singida na kuipatia Kampuni ya Konoike, baada ya kubainika kuwa kampuni hiyo haina uwezo wa kuijenga kutokana na kuwa na vifaa chakavu.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Perseko Kone, alisema jana kuwa ni kweli Sietco wameshindwa kukarabati sehemu korofi za eneo la Mkiwa, Isuna na Kamenyanga.
Kone alisema kutokana na hali hiyo, serikali imeamua kuingia mkataba mpya na Kampuni ya Konoike wa kujenga kilomita 30 kutoka Manyoni hadi Mkiwa kupitia Kamenyanga na Sietco imebakiwa kilomita 25 za kutoka Isuna hadi Mkiwa.
Siteco iliyopewa zabuni ya kujenga barabara ya Singida Manyoni, imeshindwa kabisa kurekebisha sehemu korofi zilizo haribika vibaya kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha na kusababisha magari kukwama kwa zaidi ya siku nne.
Kone alisema hadi kufika Jumatano wiki, iliyopita, Kampuni ya Konoike ilikuwa imekwisha kuanza kutengeneza maeneo yaliyo kuwa yameharibika, ikiwamo eneo la Kamenyanga ambako magari yalikuwa hayapiti kabisa kutokana na kuharibika kwa barabara.
Kone alisema serikali kupitia wakala wa barabara (Tanroads) mkoani Singida
imeweka mkakati wa kuhakikisha kuwa uzembe wa kampuni za ujenzi unadhibitiwa kwa kufuatilia kwa makini matengenezo ya barabara.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Lawrencre Tarimo, alisema hali ya barabara katika maeneo hayo sasa ni nzuri kwani magari yameanza kupita.