Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Homa Bonde la Ufa yazidi kusambaa
Homa Bonde la Ufa yazidi kusambaa
By Habari Tanzania | Published  02/14/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:

Na Mwandishi wetu, Arusha

IDADI ya watu wanahofiwa kufariki dunia kwa ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa (RVF) mkoani Arusha sasa imefikia watano huku wengine wawili wakiwa wamelazwa katika hospitali ya mkoa ya Mount Meru.

Vifo vipya vya watu watatu hao, vinaripotiwa kutokea wilayani Ngorongo watu wawili na mmoja katika Manispaa ya Arusha.

Ingawa hadi jana kulikuwa hakuna taarifa za vifo katika Manispaa ya Arusha, habari za ndani ya Hospitali ya mkoa ya Mount Meru zinasema kwamba mtu mmoja alifariki dunia Februari 7, mwaka huu kutokana na ugonjwa huo.

"Hili jambo ni zito jana (juzi) tulikuwa na kikao cha wafanyakazi wote hapa na maelekezo yametolewa kuwa hatupaswi kutoa taarifa za jambo hili na tunatakiwa kuchukua tahadhari kubwa tunapowahudumiwa wagonjwa wenye dalili za ugonjwa huu," alisema Afisa mmoja wa hospitali huyo ambaye aliomba kutotajwa jina kwa sababu habari za ugonjwa huo kwa sasa zinatolewa na Mkuu wa Mkoa..

Alisema aliyefariki dunia ni mfugaji Margwe Darida na kwamba kifo chake kilitokea Februari 7, mwaka huu aliyekuwa amefikishwa katika hospitali hiyo akitokea eneo la Magugu wilayani Babati mkoa wa Manyara.

Muhudumu mmoja wa chumba cha kuhifadhi maiti katika hospital ya mkoa alithibitisha kupokelewa kwa mwili wa marehemu Jumatano wiki iliyopita na kufanyiwa uchunguzi, hata hivyo alisisiza kwamba yeye si msemaji wa suala hilo.

"Ni kweli tulipokea mwili huo uchunguzi ulifanywa na ndugu walipong'ang'ania kwenda kumzika walipewa utaratibu maamlum ili kuwakinga na maambukizi," alisema.

Habari za uhakika toka katika hospitali ya mkoa ya Mount Meru zinaeleza kuwa watu wanaungua ugonjwa huo wamelazwa katika wodi namba sita.

Vifo vya watu wengine wawili jana vilithibitishwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Saimon Soinda, ambaye alisema kwamba ofisi yake imepokea taarifa ya vifo vya watu wawili ambao wanahofiwa kukufa kwa ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa

"Ni kweli nimepokea taarifa hizo na hivi sasa nipo Ngorongoro...tumejepanga kuhakikisha wataalam wetu wanafika katika hayo maeneo ambayo watu hao wamefariki ili kujua ukweli," alisema Soinda.

Aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Mondo Ole Ngobei (70) na Nalari Sindima (20), wote ni wakazi wa wilaya ya Ngorongoro wakitoka katika maeneo ya Nainokanoka na Engarasero mpakani mwa Tanzania na Kenya.

Hata hivyo, habari zaidi ya ugonjwa huo zimekuwa ngumu kupatikana kwani hata Mkuu wa kituo cha utafiti wa maradhi ya mifugo kanda ya kaskazini, Dk Emanuel Swai jana alikataa kuzungumza na waandishi wa habari.

Dk Swai akijibu kupitia katibu muhutasi wake alisema hana jambo la kuzungumza kwani yeye na timu ya wataalam wengine wapo katika kazi za msingi kutembelea na kuchukuwa sampuli za watu na mifugo ambao wanadaiwa kuugua ugonjwa huo.

Alisema hana muda wa kuzungumza kwani anajiandaa kuondoka kwenda Longido wilayani Monduli kukusanya takwimu," alisema katibu muhutasi wake.

Vifo hivi vinatokea baada ya watu wengine wawili kufariki dunia wiki mbili zilizopita kutokana na ugonjwa huo. Watu hao ni Naishiye Lendeyani mkazi wa Makuyuni wilaya ya Monduli na Isaya Kapera wa Terati wilayani Simanjiro.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Samuel Ndomba, aliiambia Mwananchi jana mjini hapa kuwa anayo taarifa ya kuwapo kwa wagonjwa wawili waliolazwa katika hospitali ya Mount Meru, lakini alikuwa bado hajapewa taarifa juu ya vifo vingine vilivyotokea, aliahidi kutoa taarifa kwa vyombo vya habari mara tu atakapo taarifiwa kuhusu vifo hivyo vipya.

Wakati huo huo, Mabucha mengi ya nyama jijini hapa yamefungwa kutokana na watu kususia kununua nyama huku bei za kuku, dagaa, samaki, zikiwa zimepanda.

Katika mabucha mengi licha ya kuwa na nyama kiasi kidogo, bado wateja wamekosekana wengi wakihofia kuambukizwa ugonjwa huo.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi imebaini kuwa hivi sasa kuku mmoja wa kisasa amekuwa akiuzwa kati ya Sh5,000 hadi 6,000 huku kuku wa kienyeji wakiwa wanauzwa kiasi cha kuanzia Sh6,000 hadi Sh7,000.

Awali bei za kuku hao ilikuwa ni kati ya Sh3,000 hadi 5,000 na walikuwa wakipatikana kwa wingi tofauti za hivi sasa, pia bei ya samaki, dagaa zimepanda katika soko kuu la Arusha na soko la Kilombero.

Ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa umeingia nchini ukitokea Kenya ambako hadi sasa umeua idadi kubwa ya watu na unaendelea kusambaa katika maeneo mbali mbali.

Naye Burhani Yakub, kutoka Tanga anaripoti kuwa Shirika la Afya Duniani (WHO) limeungana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii katika kuongeza nguvu ya kupambana na wimbi la maambukizi ya RVF lililojitokeza kwa kasi katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini.

WHO inashirikiana na Wizara ya Afya pamoja na kituo cha udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza chenye makao yake makuu Atlanta Marekani (CDC) katika kutoa elimu ya kujikinga pamoja na maelekezo ya kitaalamu juu ya ugonjwa huo.

Hayo yalibainika jana wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliotishwa na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga kuelezea juhudi zinazofanyika kudhibiti maambukizi ya RVF.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Magreth Mhando, WHO imeongeza nguvu ya kupambana na maambukizi hayo na Afisa wake wa Ufuatiliaji wa magonjwa ya kuambukiza, Dk William Mwengee, anashirikiana na maafisa wa idara za Afya kutembelea maeneo mbalimbali.

Dk Mhando ambaye pia ni Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Bombo alisema Hospitali hiyo jana ilipokea rasmi majibu ya vipimo vya Marehemu Razaro Milia aliyekufa wiki na kwamba imebainika kuwa kifo chake kilitokana na RVF.

Alisema hata hivyo katika majibu hayo ya vipimo vilivyokuwa vimeplekwa Arusha watu wa familia yake Pamoja na majirani wanaoishi katika Kijiji cha Mwanyumba wameonyesha kutopata maambukizi ya ugonjwa huo.

“Leo jumanne tumepokea rasmi majibu kutoka Nairobi ...hata hivyo majirani zake 10 pamoja na familia yake ya watu saba hawana virusi hivyo," alisema.

Mganga huyo alifafanua kuwa hakuna mgonjwa mwingine aliyefikishwa katika hospitali au kituo cha afya katika wilaya zote za mkoa wa Tanga ambaye ameonekana kuwa na dalili za ugonjwa huo na akawataka wananchi kuondoa wasiwasi.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.