Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Maaskofu Waanglikana duniani wakutana Dar
Maaskofu Waanglikana duniani wakutana Dar
By Habari Tanzania | Published  02/14/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:

Na Simon Berege
Maaskofu wakuu wa Kanisa la Kianglikana duniani, leo wataanza mkutano wao wa siku sita jijini Dar es Salaam kujadili mambo mbalimbali yanayohusu kanisa hilo.

Askofu wa Anglikana Jimbo la Dar es Salaam, Valentino Mokiwa, alithibitisha kuwapo kwa mkutano huo ambao alisema utafanyika katika hoteli ya Whitesands.

"Mkutano huu ni wa ndani na unawahusu maaskofu wakuu tu, mimi si Askofu Mkuu kwa hiyo nashindwa kuwa msemaji wa mkutano huo" alieleza Askofu Mokiwa na kuongeza kwamba anachojua kutakuwa na ulinzi mkali sana eneo la mkutano.

Askofu Mokiwa alisema kwamba hadi kufikia jana jioni walikuwa wakitarajia kupokea ugeni wa zaidi ya maaskofu wakuu 38 kutoka sehemu mbalimbali duniani wanaohudhuria mkutano huo muhimu na wa kihistoria.

Hata hivyo, wakati mkutano huo unaanza leo kuna habari kwamba wanaharakati wa kimataifa wa kuhamasisha ushoga duniani nao wametua jijini Dar es Salaam wakiwa na kibarua cha kuvishawishi vyombo vya kutunga sheria nchini kukubali kurekebisha sheria za nchi ili kuruhusu ndoa za watu wa jinsi moja.

Mkutano huo umetajwa kuwa mzito kwani unaweza kuweka historia mpya ya kanisa hilo kutokana na kuwepo kwa kundi la maaskofu hasa kutoka Africa wanaotaka kanisa hilo kutoa msimamo wake juu ya ushoga hasa baada ya kanisa la Marekani kukubali kumsimika kuwa askofu mtu aliyejitangaza hadharani kuwa shoga.

Ugumu wa mkutano huo unatajwa kuongezwa na kuwepo kwa Askofu Mkuu mwenye msimamo mzito kutoka nchini Nigeria, Peter Akinola (63) ambaye ameweka msimamo kutaka kurejeshwa kwa heshima ya kanisa hilo hasa kupinga kukumbatiwa kwa ushoga.

"Nina imani baada ya kukamilika kwa mkutano wa Tanzania tutakuwa na picha halisi ya mwelekeo wa kanisa" alieleza Askofu Mkuu Akinola kama ilivyoripotiwa kwenye gazeti la Lagos Daily akiwa katika maandalizi ya kuhudhuria mkutano huo muhimu.

"Maamuzi ya mkutano huu yanaweza kabisa kuonyesha muelekeo wa kanisa, na kuna hatari kukatokea mpasuko kati ya maaskofu wa Magharibi na wale wa Afrika na Asia," kilieleza moja ya vyanzo vyetu kutoka ndani ya kanisa hilo ambacho hakikupenda kutajwa jina lake gazetini.
Wachambuzi wa mambo wanaeleza kwamba Askofu wa Marekani, Katherine Schori ambaye ni mwanamke, anaweza kukumbana na makali ya Askofu Akinola kutokana na kauli yake ya kuunga mkono hatua ya kanisa hilo kumbariki kasisi wa kimarekani aliyejitangaza kuwa shoga.
Huo utakuwa ni mkutano wa kwanza kuhudhuriwa na Askofu Schori tangu aliposimikwa kushika wadhifa huo sambamba na wapya wengine 13 wanaotoka nchi mbalimbali duniani.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Nations baadhi ya Maaskofu wameapa kutokukaa meza moja na Askofu Schori huku wengine wakiwa wametishia kutoa nje ya ukumbi wa mkutano endapo Askofu huyo ataingia ndani ya ukumbi huo .
Hata hivyo, Askofu Schori mwenyewe alikaririwa akisema kwamba mgogoro uliyopo ni wa tafsiri ya biblia na wala si ushoga kwa madai kwamba kumekuwa na maaskofu na watumishi mashoga kwa miaka mingi isipokuwa kuliweka hadharani suala hilo ndiyo hatua mpya.
Askofu huyo ameeleza zaidi kwamba hata kama atabezwa katika mkutano huo hatataharuki kwani litakuwa si jambo geni kwake. Na alipotakiwa kueleza itakuwaje endapo wajumbe wenzake wataamua kumnyanyapaa alisema " Haina haya ya kuchanganyikiwa kiasi hicho wakati maisha yenyewe ni mafupi"
Habari ambazo Mwananchi imezipata zimeeleza kwamba wakati mkutano huo ukianza leo pia Mwanaharakati mkuu wa kupigania haki za mashoga duniani, Cary Alan Johnson inasemekana ametua nchini hapa huku shughuli yake kubwa ikiwa kuyashawishi makundi mbalimbali ya watu wenye ushawishi kufanya marekebisho ya sheria ili kuwe na kipengele kinachoruhusu ndoa za mashoga.
Mwanaharakati huyo hivi karibuni alikuwa nchini Kenya kwa shughuli kama hiyo na historia inaonesha kwamba walifanikiwa kushawishi Bunge la Afrika Kusini kuweka kipengele kinachotoa uhuru wa ndoa za watu wa jinsi moja, yaani wanaume kwa wanaume ama wanawake kwa wanawake.
Mkutano huo leo utaanza na semina elekezi itakayoendeshwa na Askofu Mkuu wa Canterbury, Rowan Williams ambaye pia ndiye mwenyekiti wa kikao hicho na baadaye maaskofu watatu kutoka nchini Marekani watatoa mada kuhusu hali ya kanisa hilo kwa sasa.
Baadhi ya maaskofu wa kanisa hilo walivunja mahusiano yao na kanisa la Marekani baada ya kukubali kumtawaza kasisi aliyejitangaza kuwa Shoga kuwa Askofu pamoja na kuruhusu ndoa za watu wa jinsi moja.
Naye Michael Uledi kutoka Dodoma, mchungaji wa Kanisa la Kimethodisti Tanzania Ipagala Dodoma, Joseph Bundala amesema kurusu kuwepo kwa viongozi wa dini mashoga ni batili kwa mujibu wa imani ya kikristo.

Mchungaji alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma na kusema ni dhambi mbaya kuliko zote na kuwataka wanadamu kufahamu kuwa vitendo vya ushoga ni kwenda kinyume na mipango ya mungu.

Alisema ushoga ni kitu cha kishetani na kinapaswa kukemewa kwani mungu alimuumba mwanamume na mwanamke kwa mpango mahususi na hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kupambana na namna mbinu zote za kueneza ushoga.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.