SHIRIKISHO la Vyama vya wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limekubali kubadili katiba ya shirikisho hilo kukidhi matakwa ya Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) ya uwakilishi wa uwiano katika TUCTA.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya shirikisho hilo zimesema kuwa TUCTA itaitisha mkutano wa dharura kushughulikia suala hilo. Kwa mujibu wa habari hizo, Baraza Kuu la CWT litakutana mwishoni mwa mwezi huu ili chama hicho kiweze kurudi TUCTA baada ya kujitoa kwa miezi kadhaa.
HabariLeo ina taarifa za uhakika kuwa TUCTA itaitisha Mkutano Mkuu wa dharura wakati wowote kuanzia mwezi ujao na kabla ya mkutano wa kawaida uliopangwa kufanyika baada ya miaka miwili na nusu ikiwa ni maamuzi ya mkutano mkuu wa Shirikisho hilo uliofanyika Arusha mwaka jana.
Katibu Mkuu wa TUCTA, Nestory Ngulla alithibitisha taarifa hizo jana na mmoja wa wasaidizi wake alisema anafahamu kuwa kutakuwa na mkutano mkuu wa dharura kwa ajili ya suala la CWT lakini hafahamu utafanyika lini na wapi.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa maamuzi ya TUCTA ni matokeo ya majadiliano kati ya wawakilishi wa shirikisho hilo na uongozi wa CWT yaliyofanyika Ijumaa iliyopita ili kuunusuru uanachama wa walimu.
Kujitoa kwa CWT katika shirikisho hilo kumekuwa kukielezwa kuwa lingekuwa pigo kubwa kwa TUCTA na mshikamano wa wafanyakazi nchini.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari katika shirikisho hilo lenye wanachama 360, 000, endapo CWT isingejitoa katika shirikisho mfumo wa uwakilishi wa sasa ungeendelea hadi mwaka 2009 wakati wa Mkutano Mkuu wa Kikazi wa Shirikisho utakapofanyika.
Ngulla alithibitisha taarifa hizo Jumanne iliyopita kwa kusema kuwa CWT imejitoa kwa muda katika shirikisho kwa sababu inaona kuwa hoja yake ya kutaka uwakilishi wa uwiano katika shirikisho hilo unapuuzwa hasa baada ya kutojadiliwa katika mkutano mkuu wa TUCTA uliofanyika Arusha mwaka jana.
CWT kinataka kiwe na uwakilishi unaolingana na idadi ya wanachama wao katika TUCTA hivyo kinataka katiba ya shirikisho hilo irekebishwe ili kiwe na uwakilishi unaolingana na idadi ya wanachama wake.
Chama cha Walimu Tanzania ni miongoni mwa vyama 14 wanachama wa TUCTA na ndicho chenye wanachama wengi kuliko vyama vingine katika shirikisho hilo hivyo kujitoa kwake kungeathiri pia mapato ya TUCTA.
Ngulla aliliambia gazeti hili kuwa kwa mujibu wa taratibu za TUCTA, uongozi wake hauna mamlaka ya kubadili katiba ili kuongeza idadi ya wanachama wa CWT katika shirikisho na kwamba mkutano mkuu ndiyo wenye mamlaka hayo.
Alikiri kuwa hoja ya CWT ni ya msingi lakini itabidi CWT isubiri maamuzi ya chombo chenye mamlaka ya kubadili katiba ya shirikisho kuidhinisha uanachama wa uwiano.