Shirika la umoja wa mataifa linalohudumia wakimbizi UNHCR limetoa ufadhili wa shilingi milioni kumi na sita kusaidia ujenzi wa shule ya sekondari ya kata ya Nkundutsi wilayani Kasulu.
Afisa mtendaji wa kata ya Muzye wilayani humo Bw. Ezekiel Ndayeza amebainisha hayo leo wakati akitoa taarifa kwa mkuu wa wilaya ya Kasulu Said Bwanamdogo aliyekuwa katika ukaguzi wa shule hiyo.
Bw. Ndayeza amebainisha kuwa ufadhili huo kutoka UNHCR umetokana na juhudi za wananchi kuchangia nguvu zao pamoja na kutoa pesa zilizofanikisha ujenzi wa madarasa mawili.
Amesema wananchi wameonesha moyo wa hali ya juu katika ujenzi huo baada ya kusukumwa na serikali pamoja na kuwepo kwa hamasa kubwa ya kielimu katika kata yao .
Aidha wananchi waliokuwa katika eneo la ujenzi wa shule hiyo wamempongeza mkuu wa wilaya ya Kasulu kwa juhudi zake katika kuhimiza masuala ya elimu na wameahidi kumpa ushirikiano zaidi.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kasulu Said Bwanamdogo amewahimiza wananchi kuandaa zana za ujenzi zisizo za dukani ili kurahisisha ujenzi huo hususani nyakati za kiangazi.
Wilaya ya Kasulu inatarajia kuwa na shule za sekondari 35 kutoka 24 zilizopo, ifikapo mwishoni mwa mwaka huu