Na Wandishi Wetu, Mwanza
AFYA za wafanyabiashara na vibarua wanaojishughulisha na ukaushaji wa mabaki ya minofu ya samaki maarufu kwa jina la mapanki eneo la Mkolani, Wilaya ya Nyamagana, jijini Mwanza itaendelea kuwa hatarini, ikiwa inzi na funza wanaozagaa eneo hilo hawatadhibitiwa.
Hali hiyo imebainika baada ya washiriki wa kozi ya uandishi wa habari za mazingira na mawasiliano katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT) cha jijini Mwanza walipotembelea eneo hilo mwishoni mwa wiki.
Wadudu hao ambao ni hatari kwa afya ya binadamu, walionekana wakizagaa kwa wingi eneo hilo huku shughuli za ukaushaji, utenganishaji wa vichwa na ngozi na mafuta ya samaki ukiendelea kama kawaida.
Mwenyekiti wa Kikundi cha Ukaushaji na Uuzaji Mabaki ya minofu ya Samaki, Leonard Hinkuye, alikiri kukithiri kwa wadudu hao.
"Tumekuwa na mkakati wa kutumia dawa ya kuua wadudu hawa ambayo thamani yake ni Sh35,000 kwa lita. Kwa hapa kwetu kwa wiki tunatakiwa kutumia lita moja na nusu, sawa na Sh210,000 kwa mwezi, kiasi ambacho ni kikubwa sana ukilinganisha na kipato chetu," alisema.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa eneo hilo lina tatizo kubwa la maji na ni la muda mrefu, hali inayosababisha usafi kufanyika mara moja kwa wiki.
"Tunalazimika kufanya usafi kwa muda huo hasa kwa sababu ya ugumu wa upatikanaji wa maji ambapo gharama ya maji hayo ni kubwa," alisema.
Aliongeza kusema kuwa ingekuwa vyema kama Serikali au wasamaria wema wangewasaidia kuwapatia bomba la maji katika eneo hilo, ili kuweza kufanikiwa katika zoezi zima la kufanya usafi wa kila siku.
Pia sakafu yote inayotumiwa na waandaji wa mabaki ya minofu ya samaki kwa ujumla imechakaa sana na kuwa na mashimo, hivyo hata wanapofanya usafi huwa vigumu kuondoa uchafu wote.
Katika eneo lote hilo ambalo shughuli ya utengenezaji wa mabaki ya samaki hufanyika halijaezekwa kiasi kwamba mvua inaponyesha au jua kuwaka, huwafanya wahusika kufanya kazi zao katika mazingira magumu.
Mmoja wa wanunuzi wa mabaki ya minofu ya samaki hayo aliyekutwa eneo hilo, Upendo Bonifas, mkazi wa Mkuyuni, Mwanza, alisema kwamba kwa ujumla mazingira yaliyopo katika eneo hilo ni machafu na hayaridhishi.
"Mimi huwa nakuja hapa kwa lengo la kununua mabaki ya minofu ya samaki na kwenda kukaanga na kuuza mitaani, suala hili mazingira ya uchafu linanisikitisha, lakini ni wajibu wa viongozi wao kushughulikia," alisema.