MATUKIO kadhaa katika wiki chache zilizopita nchini Tanzania, yamenifanya nimkumbuke aliyekuwa rais, dikteta wa Uganda, Nduli Idi Amin Dada.
Amin alikuwa na tabia nyingi, na sifa nyingi. Mwandishi mmoja, James Surowiecki, aliwahi kumtaja Amin kama mtawala katili sana, mjanja-mjanja, mpenda makuu, na mtu aliyependa kujianika (kutangazwa) sana na vyombo vya habari.
Ndiyo maana katika hatua isiyo ya kawaida, mwaka 1974 Amin alikubali kushiriki katika filamu binafsi iliyoandaliwa na Barbet Schroeder, iitwayo ‘General Idi Amin Dada: A Self Portrait’.
Kama sikosei, alikuwa rais wa kwanza kushiriki filamu binafsi ya aina hiyo. Katika miezi michache iliyopita, nilisikia kuna kampuni inaandaa filamu ya kuitangaza Tanzania na imemuomba Rais Jakaya Kikwete kushiriki katika filamu hiyo. Aweza kuwa rais wa pili kucheza filamu za kujitangaza? Tusubiri tuone. Anataka kujifananisha na Amin katika hilo? Tusubiri, huku kwanza tukimjadili Nduli Amin.
Amin alikuwa bingwa wa matusi na kejeli. Aliwahi kuwadhalilisha Wazungu wa Kiingereza kwa kuwalazimisha wambebe kwenye machela, eti wafanye kama wakoloni walivyowalazimisha Waafrika wawabebe.
Mara kwa mara, Amin aliwahi pia kumkejeli Rais wa Tanzania wakati huo, Julius Nyerere. Wakati fulani alimtumia ujumbe wa simu ya maneno akisema: “Nataka ujue kwamba nakupenda sana, na kwamba kama ungekuwa mwanamke ningetamani kukuoa, ingawa kichwa chako kimejaa mvi. Lakini kwa kuwa wewe ni mwanamume, basi uwezekano huo haupo tena.”
Ni rais aliyejitapa mno, mwenye suluhisho la kila tatizo; ambaye katika filamu hiyo, anatumia muda mwingi akizungumza ‘bila kikomo.’ Huyo mwandishi niliyemtaja hapo juu, akiandika katika jarida la ‘Slate’, anasema: “Amin anazungumza; na kuzungumza; na kuzungumza huku akijitapa kwa mambo ya kipuuzi. Kwa mfano, aliwahi kujitapa kwamba, Uganda ina mameneja wengi wa hoteli kuliko nchi yoyote ya Afrika. ‘Tuna mameneja wanne, na mameneja wasaidizi wawili’.”
Ajabu ni kwamba, katika kufanya hivyo, kwenye filamu hiyo, Amin hachoshi hadhira inayomsikiliza au inayomtazama. Eti, licha ya vituko vyake vya ‘kijinga’ anaburudisha; ana mvuto! Kutokana na ‘kamera kumpenda’ Amin, gazeti la New York Times, lilipoandika tanzia ya kifo chake mwaka 2003, lilimtaja Amin kuwa ‘telegenic.’
Mtengeneza filamu hiyo, Shroeder, anamtaja Amin kuwa ni mtu mchangamfu kupindukia, na mtu wa vituko. Tatizo moja alilokuwa nalo Amin ni kwamba hatabiriki. Usingeweza kujua angefanya nini au angesema nini dakika inayofuata.
Alicheza filamu hiyo akidhani ingemtukuza. Alidhani ingekuwa na mwisho mwema. Alizipenda tabia zake. Na waliojikomba kwake, walijifanya kuzipenda tabia hizo kutetea mlo wao, ingawa kwa ndani kabisa walijua madhara yake.
Katika tukio mojawapo, Amin alikutana na Baraza la Mawaziri. Akawahenyesha mawaziri kwa makosa waliyofanya, na kuwaeleza: “Msiwe dhaifu kama mwanamke… kila mmoja wenu lazima ampende kiongozi wake (yaani yeye).” Huku akisema hivyo, filamu hiyo inaonyesha baadhi ya mawaziri wakiinama na kuchukua ‘notes.’
Hata akiwaudhi kwa kauli na vitendo vyake, mawaziri hawathubutu kuondoka. Kama asemavyo, Surowiecki, mmoja wa wachambuzi mahiri wa filamu hiyo, kila mmoja wao anajua kuwa akithubutu tu kuondoka, ndiyo mwisho wa maisha yake. Ataondoka na risasi.
Mara Amin, anamfokea waziri wake wa Mambo ya Nje kwamba hajatangaza vema mafanikio makubwa ya Uganda katika medani ya kimataifa. Ni waziri huyo huyo ambaye wiki mbili baadaye alikufa kwa kuliwa na mamba mtoni.
Na katika kikao hicho, Amin anaonekana kuwa msemaji sana; bingwa wa kila jambo. Kauli inayomtoka kinywani kila mara anaposisitiza neno mbele ya mawaziri ni hii: “Nataka nieleweke wazi kabisa kwamba…” Lakini ni mtu huyo huyo ambaye alikiri kwamba anaongoza nchi bila itikadi. Aliyesema: “Sisi hatufuati dira yoyote.” (sitaki kuamini kwamba marehemu Kolimba aliazima maneno ya Amin pale aliposema CCM haina dira…)
Amin anasema kwamba ili Uganda iendelee, lazima watu wawe na ari mpya, na wafuate ushauri wake. Anasema lazima watu wafanye kazi kwa bidii zaidi, na wanawake waamke mapema, saa 11 alfajiri – na wawapende viongozi wao. Na anawatahadharisha kuwa, kama maendeleo hayatapatikana, si kwa sababu ya uongozi mbovu, bali kwa sababu wananchi hawajajibidiisha vya kutosha.
Huyo ndiye Amin. Mwisho wa ubabe wake unafahamika kwa wengi. Cha ajabu ni kwamba kuna Watanzania walithubutu kumhusudu Amin. Namjua mtu mmoja kijijini kwetu ambaye wakati wa vita ya Uganda (1978-79), aliwahi kutoa kauli za kejeli dhidi ya Nyerere, baada ya kusikia hotuba yake mojawapo. Akasema: “Hivi Nyerere anamchezea Amin? Anamjua au anatania?”
Sisi wengine tulikuwa watoto wa shule wakati huo, lakini tuliona baadhi ya watu wazima wakimshangaa jamaa huyo (sasa ni marehemu). Haishangazi. Amin, licha ya ubabe wake, alipata sifa za watu.
Kwa nini nimekumbuka filamu hiyo iliyotolewa mara ya kwanza mwaka 2002? Napata hofu ninaposoma mambo yanayoendelea nyumbani; yanayofanywa na viongozi wetu, na ambayo wanatamani kuyasifu. Naona wanavyojitahidi kupambwa na vyombo vya habari hata pasipokustahili. Naona mvuto wao. Nasikiliza ahadi na hekima zao.
Napata habari za watu (wakiwamo waandishi) wanaotumiwa vitisho kimya kimya kwa kuanika maovu ya serikali. Naona nchi inavyoongozwa bila itikadi; Watanzania wanavyokodoa macho; walivyolala, na walivyo kimya. Tunajenga himaya ya kidikteta?
Yapo mengi, lakini machache niliyoyasoma katika habari za serikali kukerwa na kazi nzuri ya HakiElimu, na vitisho vilivyoambatana nayo, yamenitisha. Baadaye nikasoma HakiElimu wakiitwa na kupewa ‘twisheni’ ya namna ya kufanya vema kazi yao kwa kuishirikisha na serikali.
Nimesikia pia matamko ya Rais Jakaya Kikwete na Jaji Mkuu Barnabas Samatta kuhusu ukosoaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA).
Nimesikia Rais Kikwete akishangazwa na jinsi watu hawa wanavyoshindwa kuona na ‘kutangaza mazuri ya serikali.’
Niliwafananisha wote hawa, HakiElimu na TAMWA, na yule Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, aliyelaumiwa hadharani kwa kutotangaza mafanikio makubwa ya Uganda. Nikasema kimoyomoyo ‘wasije nao wakakutwa wameliwa na mamba.
Lakini nikawaza kuwa tofauti kubwa kati ya waziri yule na wenzetu hawa ni kwamba yeye alikuwa na jukumu hilo (labda); lakini si hawa. Si kazi ya HakiElimu kufanya kazi ya serikali. Serikali ina mikono mingi. Inaiamini mikono hiyo.
Imesema inafanya kazi kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya. Na imewapatia semina elekezi watendaji wake wakuu wote, pale hotelini Ngurdoto. HakiElimu na TAMWA hawamo kwenye kundi hilo.
Zaidi ya hayo, haya ni makundi yaliyosajiliwa na sheria za nchi kutimiza malengo waliyoyaainisha. Wamevunja sheria? Hapana. Wameikosoa serikali. Dhambi hiyo?
Kama serikali inayo mazuri mengi, hiyo si kazi ya mashirika haya. Serikali inavyo vyombo vingi vya kuitangazia mema yake. Kama havijafanya kazi hiyo, zipo sababu. Ama hayapo, au vyombo hivyo havijui, vimeshindwa kufanya kazi hiyo.
Kuna watu wanalipwa mshahara na serikali – kutokana na kodi yetu - kufanya kazi ya kuipamba serikali. Kama wameshindwa, waelezwe, walaumiwe hao. HakiElimu na TAMWA hawastahili lawama hizo.
Lakini matukio haya na mengine, yanaonyesha hulka halisi ya serikali yetu. Inapenda kusifiwa, kutangazwa hata kwa sifa za kulazimisha. Na pale inapokosolewa kidogo tu, inaamsha ‘makucha’ yake.
Ndiyo maana wadau tumegundua ‘janja’ ya serikali katika muswada wa uhuru wa habari. Walio serikalini na mashabiki wao, wanadai ni muswada mzuri utakaosaidia kukuza uhuru wa kujieleza na kuboresha viwango vya taaluma ya habari.
Wanaoijua tabia halisi ya serikali hii, wanajua kuwa hawa si viongozi wa kupenda uhuru wa kukosolewa na kunyoshewa vidole. Watu hawa ambao wameogopa vikaragosi wa HakiElimu na TAMWA?
Mwandishi anapatikana kwa barua pepe ansbertn@yahoo.com na simu +447828696142