Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Msimamo huu wa wazazi Serengeti wa kuigwa
Msimamo huu wa wazazi Serengeti wa kuigwa
By Habari Tanzania | Published  02/11/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated

MOJA ya habari kubwa katika gazeti hili, ni kuhusu hatua ya kushangaza iliyochukuliwa na baadhi ya wazazi wilayani Serengeti, mkoani Mara, waliojitokeza kupinga watoto wao kuwamo katika orodha ya wanafunzi waliofaulu mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi.

Kwa ujasiri mkubwa, wamedai kwamba, hawaamini kwamba watoto wao waliohitimu katika Shule ya Msingi Kebosongo katika Kata ya Manchira, wamefaulu kwa akili zao.

Wamesisitiza kwamba, maendeleo ya watoto wao katika masomo yalikuwa duni kiasi kwamba inawawia vigumu kuamini kuwa wamefaulu bila ya kuonyeshwa majibu ya mitihani hiyo.

Wanashikilia msimamo huo kwa kutokana na kile walichodai kwamba, mpaka wanaingia darasa la saba, walikuwa hawawezi hata kuandika majina yao sawasawa.

Mmoja wa wazazi hao, amekacha hata kuchukua fomu ya kumwezesha mwanawe kujiunga na shule ya sekondari aliyopangiwa, akidai hakufaulu na kama jina la mwanawe limo katika orodha, basi mtihani ulijaa udanganyifu.

Na kweli, wanafunzi wenyewe wamedaiwa kukiri, kama ilivyo kwa walimu wa shule hiyo.

Imeelezwa kwamba, mmoja wa walimu amefichua siri akisema ni kweli walihusika na utoaji wa majibu kwa wanafunzi, kutokana na hofu ya kuwekwa kitimoto na Baraza la Madiwani, kama ilivyowahi kuwatokea mwaka 2002 kutokana na kushindwa kufaulisha wanafunzi.

Kwa dhati kabisa, tunaupongeza msimamo wa wazazi hao, ambao hawakutaka kuvimba vichwa kwa watoto wao kuingia kidato cha kwanza, ilhali walikuwa ‘bongo lala’.

Msimamo wao umeonyesha jinsi wazazi hao wasivyo na mzaha katika suala la elimu.

Tunaamini, kama wazazi wengine wangekuwa au watakuwa na msimamo wa aina hii, wanafunzi wengi watajikita katika masomo, badala ya kuyapa uzito mdogo kwa kutegemea msaada wa walimu na hata wazazi wenyewe katika kutafuta mbinu za kudanganya katika mitihani.

Kwa staili ya wazazi hawa wa Serengeti, tunaamini kiwango cha elimu kitapanda, si kwa kigezo cha wingi wa madarasa yasiyo na walimu wala samani, bali kwa maana halisi ya uelewa wa wanafunzi katika ngazi husika za masomo zinazowahusu.

Kinyume cha hapo, tutakuwa tunajidanganya kwa kuwa na shule nyingi zilizojaza mambumbumbu, lakini tukijiaminisha kwamba tunazalisha wataalamu.

Kwa aina hii ya baadhi ya wanafunzi waliozalishwa shule ya Kebosongo, hatuamini kama Tanzania itashika kasi katika dhana nzima ya kuinuka kielimu.

Ndiyo maana tunasema kwamba, kwa dhati kabisa tunawaunga mkono wazazi waliokataa upuuzi unaodaiwa kufanywa na walimu katika kuwaibia wanafunzi wao matokeo ya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi.

Pamoja na kuwapongeza wazazi, tunaiomba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kujifunga kibwebwe katika kuhakikisha inatoa mafunzo bora kwa walimu wanafunzi ili waweze kuwa na mbinu za kunoa akili za watoto, badala ya kutafuta njia za mkato zitakazohalalisha kuwepo kwao kazini.

Njia hizi haziwasaidii wanafunzi, walimu na hata taifa, kwani mwisho wa siku, tutajikuta tukiwa na idadi kubwa na wasomi hewa, wasioweza kujipambanua kiakili na wale wasiojua hata harufu ya chaki darasani.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.