Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Tanzania sasa kurudi COMESA
Tanzania sasa kurudi COMESA
By Habari Tanzania | Published  02/11/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Mwandishi Wetu

KATIKA moja ya mabadiliko makubwa katika sera za biashara, serikali imeanza kufikiria kuirejesha Tanzania katika Soko la Pamoja la Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA), miaka saba baada ya kujitoa.

Serikali imefikia hatua hiyo baada ya kubanwa sana na wafanyabiashara ambao wanadai kuwa, kujitoa COMESA lilikuwa ni kosa kubwa, kwani kumeinyima nchi fursa ya kukuza biashara.

Hayo yalithibitishwa na Waziri wa Uchumi, Uwezeshaji na Mipango, Dk. Juma Ngasongwa, aliyesema kuwa hatua ya Tanzania kurudi tena kwenye soko hilo umezingatia zaidi maslahi ya taifa.

“Ni kweli tulijitoa kwenye jumuiya hii kwa kipindi cha miaka saba iliyopita, lakini baada ya kukaa na kutafakari kwa kina, tumeona ni vyema tukarudi tena, hasa kwa kuzingatia maslahi ya taifa na wafanyabishara wetu,” alisema Waziri Ngasongwa.

Alisema tangu Tanzania ijitoe COMESA, wafanyabiashara wengi wa ndani walikosa fursa ya kuuza bidhaa zao kwenye soko hilo, hali iliyosababisha kurudi nyuma kimaendeleo.

Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa, wafanyabiashara wenye viwanda wamepoteza zaidi dola za Kimarekani 80 milioni kwa kushindwa kutumia fursa za COMESA kufanya biashara.

Kiasi kikubwa cha fedha hizo kimeenda Kenya na Uganda, ambao bado ni wanachama wa COMESA, hivyo wafanyabiashara waliweza kusafirisha bidhaa kwenye nchi wanachama chini ya taratibu zilizowekwa.

Taarifa zinaonyesha kuwa, Kiwanda cha Kioo Limited, kilipoteza kiasi cha dola za Kimarekani milioni 2 baada ya kushindwa kusafirisha chupa za Coca Cola kwenda Zimbabwe na Malawi chini ya makubaliano yaliyokuwa yamesainiwa mwaka 2003.

Badala yake, nchi hizo ziliagiza chupa hizo kutoka Mashariki ya Kati.

Kutokana na hali hiyo, wafanyabiashara kadhaa wamekuwa wakiishinikiza serikali kutaka Tanzania irejee COMESA.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari, Dk. Ngasongwa alisema uamuzi wa kurejea COMESA, umepewa uzito na Rais Jakaya Kikwete juzi wakati alipokutana na wawekezaji wa ndani katika mkutano wa kitaifa uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Katka mkutano huo, Rais Kikwete aliwataka wawekezaji hao kukaa na kufikiria upya uamuzi wa kurudi kwenye jumuya hiyo.

“Juzi, wakati Rais Kikwete amekutana na wawekezaji aliwataka wafanyabiashara kujenga hoja upya ya kurudi kwenye jumuiya hii haraka kwa lengo la kuhakikisha wafanyabishara wetu wanapata nafasi ya kuuza bidhaa bila tatizo,” alisema Waziri Ngasongwa.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabishara, Viwanda na Kilimo, Elvis Musiba alisema suala hilo linatarajia kufikishwa kwenye Kamati ya Uchumi na Uwezeshaji ya Bunge ili liweze kujadiliwa kwa kina na hatimaye kufikia muafaka.

“Baada ya kupata baraka za rais wetu, sasa suala hili tutalipeleka kwenye Kamati ya Uchumi na Uwezeshaji ya Bunge letu ili tulizungumze na hatimaye tufikie makubaliano kwa maslahi ya taifa letu,” alisema Musiba.

Alisema kurudi COMESA, itakuwa ni moja ya hatua kubwa ambayo itasaidia uwekezaji kukua, hasa sekta ya kilimo, ambayo mpaka sasa uwekezaji wake ni asilimia 5 tu.

Mwenyekiti huyo, aliitaka serikali kuhakikisha inatoa ardhi kwa wananchi, ili waweze kuimiliki. Alisema hatua hiyo itasaidia wananchi kupata mikopo kupitia benki, tofauti na ilivyo sasa.

“Kuwawezesha wananchi kwa kumiliki ardhi, hasa maeneo ya vijijini, ni moja ya hatua kubwa sana itakayosaidia sekta binafsi kupiga hatua dhidi ya umasikini,” alisema Musiba.

Tanzania ilijitoa COMESA mwaka 2000 baada ya kudai kuwa hainufaiki na jumuia hiyo.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.