Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Wapinga watoto wao kufaulu darasa la saba
Wapinga watoto wao kufaulu darasa la saba
By Habari Tanzania | Published  02/11/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Mako Shaweshi, Serengeti

KATIKA hali ya kushangaza, baadhi ya wazazi wilayani hapa, mkoani Mara, wameijia juu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi baada ya kutangaza kuwa watoto wao ni kati ya wanafunzi waliofaulu mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi.

Wazazi hao wanadai kuwa, maendeleo ya watoto wao katika masomo yalikuwa duni kiasi kwamba inawawia vigumu kuamini kuwa wamefaulu bila ya kuonyeshwa majibu ya mitihani hiyo.

Walisema, inashangaza kuona watoto wao wamefaulu wakati mpaka wanaingia darasa la saba, walikuwa hawawezi hata kuandika majina yao sawasawa.

Tanzania Daima imepata baadhi ya majina ya watoto hao kuwa ni Ryoba Nyamhanga aliyefanya mtihani kwa kutumia namba ya PS.016/027, Samweli Magoiga mwenye nambari PS/016/034, Ibrahim Machage PS/016/013, Ibrahim Benson PS/016/012 na Samson Mwita PS/016/030. Wote walikuwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Kebosongo, Kata ya Manchira.

Watoto hao wote wamechaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari Manchira, wilayani hapa.

Akizungumza na Tanzanaia Daima, mzazi wa Ryoba, Charles Nyamhanga, alishangaa mtoto wake kuchaguliwa kuingia kidato cha kwanza baada ya kufaulu, wakati alikuwa hawezi hata kuandika jina lake sawasawa.

Naye Mniko Mwita, mzazi wa Samson Mwita, alisema ameshindwa hata kwenda kuchukua fomu ya kumwezesha mwanawe kujiunga na shule ya sekondari aliyopangiwa kwani anajua wazi kuwa matokeo yale yalijaa udanganyifu.

Akihojiwa na Tanzania Daima, mmoja wa wanafunzi hao, Samson Mwita, alikiri kupewa majibu na walimu wao ambao waliwaambia wanakili kama yalivyo.

Mwalimu mmoja wa shule hiyo, ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema kuwa ni kweli waliwapatia watoto hao majibu ya mitihani yao.

Alidai kuwa, walifikia hatua hiyo kwa kuogopa kuwekwa kitimoto na Baraza la Madiwani kama ilivyotokea mwaka 2002 baada ya kushindwa kufaulisha wanafunzi.

“Nani anapenda kusumbuliwa kwa kuhojiwa bwana?” alihoji mwalimu huyo na kuongeza kuwa mwaka 2002 walipewa barua wakitakiwa wajieleze baada ya shule yao kuwa miongoni mwa shule zilizofanya vibaya.

Alipotakiwa kulizungumzia suala hilo, Ofisa Elimu wa Wilaya ya Serengeti, aliyetambuliwa kwa jina moja la Ishengoma, alisema kuwa kama kweli kuna mwalimu alimuonyesha mwanafunzi majibu, basi atakuwa ametenda kosa kubwa.

Alibainisha kuwa, kabla ya kufanyika kwa mitihani hiyo mwaka jana, ilifanyika semina iliyowahusisha wasimamizi wote, na maofisa kutoka Usalama wa Raia, na kutoa msisitizo juu ya kuzuia udanganyifu katika mitihani.

“Yeyote aliyeonyesha majibu kwa mwanafunzi, atakuwa amekiuka kanuni namba 70 ya usalama au kutotunza siri, ambayo adhabu yake ni kifungo,” alisema Ishengoma na kuahidi kulifanyia uchunguzi wa kina suala hilo.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya, Andrea Manyerera, alisema kuwa ofisi yake ilikuwa haijapokea suala hilo, lakini baada ya kupata fununu hizi, amewaagiza watendaji wa idara hiyo kufuatilia.

Tanzania Daima ilipomtafuta Ofisa Elimu Mkoa wa Mara, Ramadhani Chomola, naye alidai kuwa taarifa hiyo ni mpya kwake, lakini aliahidi kuifuatilia.

Wakizungumza na gazeti hili, wadau wa elimu wilayani hapa, walizitaka mamlaka zinazohusika kutokurupuka na kuanza kuwahoji watu kuhusu matatizo ambayo yapo juu ya uwezo wao.

Walisema Shule ya Msingi Ikolongo, iliyotajwa kufanya vibaya kitaifa, ina wanafunzi zaidi ya 500 wakati ina walimu watatu tu.

Walisema katika mazingira kama hayo, si vema kumlaumu mwalimu iwapo itatokea wanafunzi kufanya vibaya.

Hata hivyo, bado watu wanahoji wanafunzi kama hao walifanyaje mtihani wa darasa la nne na kufaulu kuendelea darasa la tano?


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.