SERIKALI imesema mchakato wa kulikodisha Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa mwekezaji mpya, umefikia ukingoni.
Waziri wa Uchumi, Mipango na Uwezeshaji, Dk. Juma Ngasongwa, aliwaambia waandishi wa habari juzi usiku kwenye Hotel ya Movenpick, Dar es Salaam kuwa, karibu taratibu zote kuhusu ukodishwaji wa shirika hilo zimekamilika.
Alibainisha kuwa, katika kipindi cha wiki moja ijayo, serikali itatoa tamko kuhusu hatma ya shirika hilo.
“Ni kweli tumekuwa na mazungumzo na mwekezaji mpya juu ya kuchukua shirika hilo na mambo yote karibu yamekamilika, tunategemea ndani ya wiki moja au mbili serikali itatoa tamko rasmi juu ya TRC kukodshwa,” alisema Waziri Ngasongwa.
Katika kuonyesha kuwa ukodishaji wa TRC umekamilika, Dk. Ngasongwa aliwatajia waandishi wa habari kuwa, shirika jipya litakuwa chini ya Tanzania Railways LTD.
Alisema kuwa ukodishwaji wa shirika hilo unalenga kuongeza ufanisi ndani ya chombo hicho muhimu kwa usafiri wa walalahoi.
“Chombo hiki ndiyo kitakuwa na kazi ya kuongoza shirika hili na kwa kweli hatutaki kurudia makosa kama ilivyokuwa hapo awali,” alisema Waziri Ngasongwa.
Alisema katika makubaliano yaliyofikiwa na mwekezaji mpya, ni pamoja na kukarabati kilometa 648 za reli zilizo katika hali mbaya.
“Tumekubaliana nao kuwa, watakarabati urefu huo, kama mnavyojua reli yetu ina urefu kilomita 2,000, sasa hizi zinazosalia itakuwa jukumu letu sisi kukarabati na kuhakikisha inapitika wakati wote,” alisema.
Alisema kubinafsishwa kwa reli hiyo ni kutaka kuongeza ushindani wa soko huria na kuhakikisha inazivutia nchi zisizo na bandari kuendelea kutumia miundombinu ya Tanzania.
Alizitaja baadhi ya nchi hizo kuwa ni pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Rwanda na Burundi ambazo zimekuwa zikitumia zaidi bandari ya Dar es Salaam.
Hivi karibuni, gazeti hili liliripoti kuwa, TRC iko hoi kifedha na imekuwa ikitumia zaidi ya sh milioni 60 kila siku kama ruzuku kutoka serikalini.
Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Linford Mboma, aliiambia Tanzania Daima kuwa, shirika hilo limeshindwa kujiendesha kutokana na kuporomoka kwa mapato kulikosababishawa na pamoja na mambo mengine, uchakavu wa miundombinu.
Mboma alisema kwa sasa, menejimenti ya TRC haiwezi kufanya lolote kulinusu shirika na majaaliwa yake yapo chini ya mwekezaji mpya ambaye atatangazwa hivi karibuni.