Ili kuleta ushindani wa kuwania nafasi, kambi ijayo ya timu ya taifa, Taifa Stars, itaongezewa mlinda mlango mmoja, imeelezwa.
Kocha mkuu wa Taifa Stars Mshindo Msolla alisema jijini mwishoni mwa wiki kuwa kwasababu walinda mlango kwa kawaida huwa ni watatu katika kikosi cha timu, na kwasababu kwasasa kikosi hicho kina walinda mlango watatu tayari, mchezaji mmoja ataongezwa kambi ijayo.
Msolla ambaye inadaiwa ameshikilia nafasi hiyo wakati shirikisho la soka, TFF, likisubiri kutimizwa kwa ahadi ya serikali ya kuajiri kocha wa kigeni, hakuwa tayari kutaja jina la milnda mlango atakayeongezwa hatahivyo.
Stars itaingia tena kambini Juni baada ya mazoezi ya wiki moja mapema mwezi huu.
Msolla alisema wanaongeza mlinda mlango huyo ili kuleta ushindani utakaobakiwa wachezaji watatu walio kwenye kiwango cha juu katika michuano ya kimataifa.
’’Ushindani muhimu na tunaangalia wenye uwezo. Hawa watatu sio kwamba hawafai bali hata katika mashindano tutawatumia watatu, hiyo lazima awepo wa nne ili kuleta ushindani na tuchague watatu bora,’’ alisema Msolla.
Alisema watampata kipa huyo kwa kuangalia mchango kwa timu yake katika michuano ya kimataifa na ligi kuu ya Bara kwa mwaka jana na msimu huu.
Stars ambayo inajiandaa na michuano ya awali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa ajili ya fainali zitakazofanyika Ghana mwaka 2008, ina walinda mlango watatu ambao ni Farouk Ramadhani wa Moro United, Juma Kaseja wa Simba na Ivo Mapunda wa Yanga.
Stars imepangwa Kundi la Saba ikiwa na timu za Bukina Fasso, Msumbiji na Senegal, na itaanza kurusha kete yake ya kwanza Septemba kwa kuikaribisha Bukina Fasso.
SOURCE: Lete Raha