Na Mathew Kwembe
RAIS Jakaya Kikwete amesema baadhi ya watendaji wa serikali wanaoshughulika na utoaji leseni na mfuko wa kodi, wanadumaza uwekezaji nchini kutokana na urasimu.
Kauli hiyo aliitoa jana wakati akifungua mkutano wa pili wa wawekezaji wa ndani, jijini Dar es Salaam.
Rais kikwete, alisema serikali yake inanuia kurekebisha dosari hizo ili kujenga mazingira mazuri ya kuvutia zaidi wawekezaji.
Alisema serikali yake inatambua mchango wa sekta binafsi katika kuinua uchumi wa nchi, ndiyo maana imejidhatiti kusaidia taasisi hiyo ili kuleta ufanisi zaidi.
Kikwete, alisema serikali yake iko tayari kujenga mazingira ya urafiki na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kuifanya Tanzania kuwa mahali pazuri pa kuwekeza na kwamba inalichukulia kwa uzito wa pekee suala la kila mwekezaji anayekuja nchini kufanya biashara.
Hata hivyo alielezea matumaini yake kuwa sheria mpya ya biashara itasaidia kwa kiasi kikubwa kutatua dosari hizo.
Huo ni Mkutano wa kwanza kufanyika tangu serikali ya awamu ya nne kuiingia madarakani na umeongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Biashara ambaye ni Rais Kikwete.
Mkutano wa kwanza wa wawekezaji wa ndani nchini ulifanyika mwaka 2002 na kuongozwa na aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Marten Lumbanga.