Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Shule za wasichana zaongoza kufaulu Tanzania kidato cha nne
Shule za wasichana zaongoza kufaulu Tanzania kidato cha nne
By Habari Tanzania | Published  02/10/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:

Na Muhibu Said

MATOKEO ya mtihani wa taifa wa kidato cha nne uliofanyika nchini Oktoba, mwaka jana yametangazwa jana na Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), huku shule za sekondari za wasichana za St. Francis ya mkoani Mbeya na Marian ya Pwani zikiongoza katika orodha ya shule 10 bora zilizofaulisha vizuri.

Katika matokeo hayo yaliyotangazwa na Katibu Mtendaji wa Necta jijini Dar es Salaam, Dk Joyce Ndalichako, Mkoa wa Kilimanjaro umeongoza kwa kuwa na shule nyingi zilizofaulisha vizuri huku Zanzibar ikishika mkia kutokana na kuwa na shule nyingi zilizofanya vibaya. Mikoa inayofuata kwa kufanya vibaya ni Ruvuma, Tanga na Mtwara.

Matokeo hayo ni ya mtihani wa kidato cha nne (CSEE), mtihani wa maarifa (QT) na mtihani wa ualimu daraja A (GATCE).

Akitangaza matokeo ya shule 10 bora zenye watahiniwa 35 au zaidi, Dk Ndalichako alizitaja shule nyingine zilizofanya vizuri, mbali ya hizo mbili za wasichana kuwa, ni Seminary ya Uru (Kilimanjaro), Agape Lutheran Junior Seminary (Kilimanjaro), St James Seminary, Kilema (Kilimanjaro), St Mary's Mazinde Juu (Tanga), Msolwa (Morogoro), Feza Boys (Dar es Salaam), Dungunyi Seminary (Singida) na St Mary Goreti (Kilimanjaro).

Dk Ndalichako alizitaja shule 10 bora zenye watahiniwa chini ya 35 kuwa ni St Joseph-Kilocha (Iringa), Maua Seminary (Kilimanjaro), Rubya Seminary (Kagera), Nyegezi Seminary (Mwanza), St Mary's Junior Seminary (Pwani), Katoke Seminary (Kagera), Likonde Seminary (Ruvuma), Arusha Catholic Seminary (Arusha), Don Bosco Seminary (Shinyanga) na Kasita Seminary (Morogoro).

Dk Ndalichako, alizitaja shule 10 zilizofanya vibaya zenye watahiniwa 35 au zaidi kuwa ni Mwaal (Tanga), Lukumbule (Ruvuma), Mataka (Ruvuma), Kangagani (Pemba), Shemsanga (Tanga), Tumbe (Zanzibar), Mkwese (Singida) Kitangari (Mtwara), Sasawala (Ruvuma) na Mbesa (Ruvuma).

Aidha alizitaja shule 10 zenye watahiniwa chini ya 35 zilizofanya vibaya kuwa ni Kilindi (Pemba), Dole (Zanzibar), Uondwe (Pemba), Makongeni (Zanzibar), Badri (Tabora), Ngwachani (Zanzibar), Namasakata (Ruvuma), Kitogani (Zanzibar), Nakapanya (Ruvuma) na Mtende (Zanzibar).

Dk Ndalichako, aliwaambia waandishi wa habari kuwa matokeo hayo yanaonyesha kuwa ufaulu wa watahiniwa mwaka jana umeshuka kwa asilimia 1.26 ikilinganishwa na mwaka juzi.

Alisema jumla ya watahiniwa 116,647 wa shule na wa kujitegemea, sawa na asilimia 82.30 ya waliofanya mtihani mwaka jana, wamefaulu wakati watahiniwa 25,081, sawa na asilimia 17.70, hawakufaulu. Mwaka juzi, asilimia 83.56 ya watahiniwa waliofanya mtihani walifaulu.

Hata hivyo, Dk Ndalichako alisema idadi ya watahiniwa wa shule waliofaulu mtihani mwaka jana, imeshuka kidogo kwa asilimia 0.08, wakati wale wa kujitegemea, imepanda kwa asilimia 0.33 ikilinganishwa na mwaka juzi.

Alisema kwa upande wa madaraja waliyopata watahiniwa wa shule katika CSEE mwaka jana, jumla ya watahiniwa 30,694, sawa na asilimia 35.7, wamefaulu katika madaraja ya kwanza hadi ya tatu, huku idadi kubwa wakiwa ni wavulana na ndogo wasichana.

Wakati idadi ya wavulana ikiwa ni 20,167 (sawa na asilimia 40) waliofanya mtihani, wasichana ni 10,527 (sawa na asilimia 29.1).

Kwa mujibu wa Dk Ndalichako, matokeo ya CSEE yanaonyesha wavulana wameongoza kwa kufanya vizuri zaidi kuliko wasichana. Hata hivyo, alisema wavulana 4,946, sawa na asilimia 10.0, wameshindwa mtihani huo wakati wasichana wakiwa 4,395, sawa na asilimia 12.1.

Kuhusu ufaulu wa kimasomo, Dk Ndalichako alisema watahiniwa wamefanya vizuri zaidi katika somo la Kiswahili, ambalo asilimia 85.4 ya watahiniwa wote wa shule wamefaulu. Hata hivyo, alisema wasichana wamefanya vizuri zaidi katika somo hilo kulinganisha na wavulana.

Dk Ndalichako, alisema ufaulu katika somo la Hisabati upo katika kiwango cha chini kwani ni asilimia 23.1 tu ya watahiniwa wote wa shule wamefaulu na kwamba, asilimia ya wasichana waliofaulu somo hilo ni 14.7 na wavulana waliofaulu ni asilimia 29.7.

Alisema watahiniwa 5,878, sawa na asilimia 31.31 ya vijana 27,587 waliofanya mtihani wa QT, wamefaulu. Ufaulu katika mtihani huo mwaka jana, umepungua kwa asilimia 0.64 ikilinganishwa na mwaka juzi.

Dk Ndalichako, alisema watahiniwa 5,903, sawa na asilimia 98.35 ya waliofanya mtihani wa GATCE daraja la A mwaka jana wamefaulu, huku watahiniwa 99, sawa na asilimia 1.65, wameshindwa mtihani huo.

Idadi ya watahiniwa wa mtihani huo mwaka juzi waliofaulu, ilikuwa 7,523 (99.58%) na idadi ya walioshindwa ilikuwa 32 (0.42%). Kutokana na hali hiyo, idadi ya watahiniwa waliofaulu mtihani huo, imeshuka kwa asilimia 1.23.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.