Na Michael Uledi, Dodoma
BUNGE limewapuuza wanasheria akiwemo Jaji wa Mahakama ya Afrika Mashariki, Joseph Warioba, na kupitisha Azio la mabadiliko ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuanzisha Mahakama ya Rufaa.
Uamuzi huo ulipitishwa juzi jioni na wabunge, wengi wao wakiwa Chama Chama Mapinduzi (CCM) baada ya wenzao wa upinzani kuukataa, lakini zilipopigwa kura za sauti, Spika aliridhika kuwa waliosema azimio hilo lipite walikuwa wameshinda.
Azimio hilo liliridhiwa na bunge hilo licha ya kauli za awali za kuwashauri wabunmge wakatae kufanya hivyo zilizotolewa na Jaji Warioba na Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), kuwa upitishwaji wake unakiuka Mkataba wa Afrika Mashariki.
Akizungumza na gazeti hili mwezi ulipita, Warioba alisema kwa kufanya hivyo, Marais Jakaya Kikwete wa Tanzania, Yoweri Museveni wa Uganda na Mwai Kibaki wa Kenya, wangekuwa wamevunja mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa kuanzisha Mahakama ya Rufani bila kuwashirikisha wadau.
Marais hao wameamua kuharakisha kufanywa kwa marekebisho ya Mkataba wa Afrika Mashariki bila kufuata taratibu zilizowekwa kwenye mkataba huo, ili tu waweze kupata Mahakama hiyo haraka bila kujali kwamba utaratibu wa marekebisho ya mkataba ambao umeelezwa kwa uwazi kabisa umekiukwa.
Wakuu hao katika mkutano wao wa mwishoni mwa Novemba mwaka jana, walitaka kufanywa kwa marekebisho ya Mahakama ya Jumuiya, na kuwataka wanasheria wakuu wa nchi hizo kukutana mara moja kujadili jambo hilo.
Kutokana na maelekezo hayo, wanasheria hao walikutana na katika kipindi cha siku saba, yaani Desemba 7, 2006, waliwasilisha kwa Katibu Mkuu EAC mapendekezo husika.
Mapendekezo hayo yaliwasilishwa kwa Baraza la Mawaziri la EAC ambao waliyapeleka kwa wakuu wa nchi, Kikwete, Museveni na Kibaki, ndani ya mwezi huo wa Desemba na waliyapitisha wakati wa Mkutano wa Nchi za Maziwa Makuu kwa haraka, na sasa Bunge la Tanzania katika mkutano wake unaomba Jumanne ijayo linatakiwa kuridhia mabadiliko hayo.
Jaji Warioba alisema ingawa mabadiliko katika mkataba huo ni jambo la kawaida, utaratibu uliotumika unakiuka ibara ya 150 ya Mkataba wa EAC ambao unaeleza waziwazi taratibu za kufuatwa katika kutekeleza hayo.
“Utaratibu uliotumika kufanya mabadiliko hayo umevunja matakwa ya ibara hiyo katika mkataba,” alisema Jaji Warioba.
Ibara ya 150 ya Mkataba wa EAC unaeleza kwamba, nchi mwanachama au Baraza la Mawaziri wanaweza kupendekeza mabadiliko ya mkataba huo.
Kulingana na utaratibu ulioelezwa, mapendekeo hayo yanawasilishwa kwa Katibu Mkuu wa EAC ambaye ndani ya kipindi cha siku 30 anawajibika kuyasambaza kwa nchi wanachama.
Ibara hiyo inafafanua kwamba nchi wanachama wakishapokea mapendekezo hayo wanaweza kuyajadili kadri wanavyoona inafaa na kwamba yanatakiwa yawe yamerejeshwa kwa Katibu Mkuu EAC ndani ya kipindi cha siku 90 pamoja na maoni yao, ambaye atayawasilisha kwa wakuw wa nchi.
Baada ya hoja hizo za Warioba, Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) nacho kiliwashauri wabunge kutopitisha azimio hilo ili kutoa nafasi ya utaratibu wa kisheria kufuatwa.
Chama hicho kilituma ujumbe mkoani Dodoma kuomba azimio hilo lisipitishwe, lakini inaonekana ushauri wake umewekwa kando na azimio likapitishwa.
Wakijadili azimio hilo juzi, wabunge wa Kambi ya Upinzani na baadhi ya wa CCM, walionekana kumuunga mkono Warioba marekebisho hayo hayakuzingatia utaratibu uliowekwa na mkataba wa jumiya hiyo.
Wabunge wote wa upinzani waliipinga hoja hiyo kwa hoja kuwa ilikuwa ni kinyume na mkataba kuridhia marekebisho hayo kwa kuzingatia kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ilikuwa ni ya wananchi wa nchi husika na hivyo kutakiwa kuwa na ridhaa yao kabla ya kuamua kuridhia.
Msemaji wa Kambi ya Upinzani, Abubakar Bakary, akiwasilisha maoni ya kambi ya hiyo alisema kuwa baadhi ya taratibu ambazo hazikuzingatiwa ni pamoja na kuwepo kwa matatizo mengi katika jumuiya hiyo ambayo yangehitaji marekebisho kabla ya kurukia kujiingiza katika suala hilo.
Msemaji huyo wa upinzani alisema kuwa kimsingi tatizo hilo ni la Kenya pekee na hivyo isingefaa marekebisho hayo kufanywa kabla ya Kenya wenyewe kerekebisha tatizo hilo na kwamba kuna haja gani kushughulikia tatizo moja badala ya kufanya marekebisho katika mambo yote ambayo ni tishio kwa jumuiya.
Alisema kuwa serikali inakiuka ibara ya 150 kifungu cha nne na cha 5 cha mkataba huo ambazo zinataka nchi wanachama watoe mapendekezo yao ndani ya siku tisini na kwamba baada ya siku tisini katibu mkuu apelike maoni kwa kwa wakuu wan chi.
“Vilevile mkataba huo uanasisitiza kuwa hata katika utangulizi wake kwamba lazima wadau (wananchi) washirikishwe ipasavyo. Hatukufanya hayo...kambi yetu inasikitishwa sana kwa serikali kukiuka matakwa ya mkataba huo,” alisema Msemaji huyo wa upinzani.
Akichangia majadiliano ya hoja hiyo Mbunge wa Karatu Dk Wilbroad Slaa (Chadema), alisema kuwa ni vyema serikali ikaliona kama ni tatizo kubwa hasa kwa kuwa Kenya
ilipitisha kuridhiwa mabadiliko hayo bila kufika bungeni na kwamba kwa kufanya hivyo Tanzania inajiingiza katika mgogoro mkubwa kwani inafanya mambo kinyume na
sheria.
Mbunge wa Viti Maalum, Halima Mdee (Chadema) alipinga hoja ya kuridhia kuundwa kwa mahakama hiyo kwa kile kilichoelezwa kuwa utaratibu mzima na mambo ya mikataba yalistahili kuhakikishwa yanazingatia maslahi ya taifa na kuacha kufanywa kisiasa kama ambavyo Bunge liliamua kufanya.
Mdee alisema katika mambo ya msingi kama hayo ni vyema kufuatwa utaratibu ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wananchi katika maamuzi mazito kama hayo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe alisema kuwa ibara ya 150 ya mkataba wa jumuiya hiyo umekaa vibaya na akapendekeza hoja hiyo iridhiwe na kisha hitilafu zilizomo zirekebishwe.
Akiwasilisha Azimio la kuridhia marekebisho ya mkataba wa kuanzishwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Waziri wa ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk.Ibrahim Msabaha alisema kuwa ibara ya 150 ya mkataba huo inaeleza utaratibu wa kufuatwa katika kufanya marekebisho.
Msabaha alisema kuwa marekebisho yaliyowasilishwa yalilenga kuanzishwa kwa mahakama ya rufaa lengo likiwa ni kutoa nafasi,uhuru na haki ya kukata rufaa kwa mtu au asasi itakayohitaji fursa hiyo.
Bunge liliridhia mkataba huo baada ya kuwapo majadiliano yaliyotawaliwa na wabunge ambao kitaaluma ni wanasheria ambao walipambana kwa hoja za kitaalamu na mwisho uamuzi wa kura ulipitisha kuridhiwa kwa mabadiliko hayo.