SERIKALI inatafuta walimu zaidi ya 9,000 wanaotakiwa kufundisha katika sekondari mpya zilizofunguliwa na wananchi, kabla ya Machi mwaka huu.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Margaret Sitta alisema jana kuwa Wizara inataka walimu hao kutokana na idadi ya wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza mwaka huu kuongezeka na kufikia asilimia 90 badala ya asilimia 75.
Vijana waliomaliza kidato cha sita na kufaulu wametakiwa kuomba nafasi hizo na watapewa mafunzo ya mwezi mmoja katika vyuo mbalimbali vya ualimu nchini, alisema. Alisema wanahitajika vijana 6,000 kuhudhuria mafunzo hayo kwenye vyuo vya Monduli, Morogoro, Korogwe, Mpwapwa, Tabora, Tukuyu, Butimba, Mtwara na Kleruu. Waziri alishauri vijana hao waombe nafasi katika vyuo vilivyo karibu na mikoa yao.
Mafunzo hayo yataanza Februari 26 na yatamalizika Machi 24 na wote watakaomaliza watasambazwa katika sekondari mbalimbali kwa ajili ya kufundisha, alisema. Kuhusu walimu wengine, Waziri alisema walimu wengine 3,124 watakaomaliza mitihani ya stashahada mwezi huu nao watapangiwa katika shule mbalimbali kupunguza upungufu huo.
Wizara pia itaajiri walimu 450 kutoka vyuo vikuu na walimu wastaafu 250 wataajiriwa kwa mkataba alisema na kuongeza kuwa idadi ya walimu wote wanaohitajika ni 9671 ambao watatawanywa katika shule mpya 667 za sekondari zilizofunguliwa mwaka huu.
Alisema serikali imetenga fedha kwa ajili ya kugharamia mafunzo ya muda mfupi ya walimu watakaohudhuria mafunzo ya mwezi mmoja na watalipwa mishahara yao watakapoanza kazi kwa sababu iko tayari.
Waziri alisisitiza kuwa vijana wanaotaka kujiunga na mafunzo hayo ni lazima wapeleke maombi yao kabla ya Februari 15 ili yaweze kufanyiwa kazi haraka na waanze masomo yao.
Akizungumzia wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza alisema kati ya wanafunzi 467,997 waliofaulu mwaka huu kujiunga na kidato cha kwanza, wanafunzi 421,368 watajiunga na sekondari baada ya shule hizo kuongezeka. “Wananchi wameonyesha moyo wa kujenga sekondari, ni jukumu letu kutafuta walimu ili wakafundishe kwenye shule hizo,” alisema.