SPIKA wa Bunge, Samuel Sitta ameikabidhi Taasisi ya Kuzuia Rushwa (PCB) jukumu la kuchunguza madai yaliyotolewa na Mbunge wa Moshi Mjini, Phillemon Ndesamburo (Chadema) kuwa baadhi ya wabunge walipokea rushwa kutoka kwa mfanyabiashara maarufu, Yussuf Manji.
Uamuzi huo unatoa fursa ya sheria kuchukua mkondo wake kwa wabunge ambao itabainika
walipokea rushwa kupindisha ukweli katika shauri la Mbunge wa Mkuranga, Adam Malima (CCM) na Reginald Mengi, Mwenyekiti wa IPP, kuhusu tuhuma kwamba Mengi amekuwa akitumia muda mwingi kuliko viongozi wa taifa katika televisheni yake ya ITV.
Sitta alimuelekeza Katibu wa Bunge, Damian Foka kumwandikia Mkurugenzi wa PCB, Edward Hosea na tayari amekwisha kuandika barua hiyo Januari 26, mwaka huu kuomba taasisi hiyo kutekeleza wajibu wake wa kuchunguza madai hayo ya rushwa.
Ndesamburo ametakiwa kutoa ushirikiano kwa PCB ili ukweli ufahamike juu ya madai hayo ya rushwa. Spika pia amemwagiza Foka kumpatia ushauri kamili wa uhalali wa Ndesamburo akiwa mjumbe wa kamati ya bunge, kufanya mawasiliano yasiyo rasmi na mmoja wa watu wanaochunguzwa wakati uchunguzi unaendelea.
“Ingewezekana kuiagiza kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kufuatilia jambo hili, lakini nimeona si hekima kufanya hivyo kwa sasa,” alisema Sitta.
Spika alisema anachelea kuchukua hatua zozote ambazo zitaonekana kumwekea vipingamizi au kumziba Ndesamburo hasa kwa sababu tuhuma za rushwa anazielekeza kwa wabunge wenzake.
Alisema ameamua kulifikisha suala hilo kwa PCB kwa vile kauli za mbunge huyo zimekuwa zinapingana juu ya namna alivyopata malalamiko ya Mengi. “Awali alidai Mengi alimpigia simu, lakini baadaye alidai alikutana na Mengi,” alisema Sitta.
Kauli nyingine ni ambayo Ndesamburo, awali alidai rushwa hiyo ilitolewa kwa wajumbe wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, lakini baadaye alidai rushwa hiyo ilienda kwa wabunge, alisema Spika.
Kutokana na utata huo, Sitta alimwandikia barua na majibu ya mbunge huyo yalieleza kuwa wanaohisiwa kula rushwa ni wabunge na hakubainisha kama ni wajumbe wa kamati ama wabunge nje ya kamati.
Spika alisema hata katika hali inayozidi kukanganya katika barua yake ya Januari 24, Ndesamburo alikanusha kwamba yeye hakuwahi kumtaja Yusufu Manji aliyemtukana magazetini bali alimtaja Manji ambaye anamjua Mengi na huenda siyo Yusufu Manji.
Alisema tuhuma za wabunge kupewa rushwa ni nzito kutokana na kutolewa na mbunge ambaye ni mtu mzima na mzoefu, hivyo haziwezi kupuuzwa hata kidogo. “Kutokana na sababu hiyo na kwa kuzingatia ukweli kuwa kupokea au kutoa rushwa ni kosa la jinai kwa mujibu wa sheria. Na kwa vile kwa kosa la jinai Wabunge hatuna kinga yoyote nimeagiza PCB ilishughulikie suala hili,” alisema.
Wakati huo huo, Spika amesema Malima alisema uongo kuhusu tuhuma zake dhidi ya kituo cha televisheni cha ITV na Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi. Uamuzi wa Sitta unatofautiana na ushauri aliopewa na Kamati ya Kinga, Maadili na Madaraka ya Bunge ambayo iliridhika kuwa Malima hakusema uongo ndani ya Bunge.
Uamuzi wa jana wa Spika unafanana na ushauri tofauti uliotolewa na wabunge wawili, Christopher Ole Sendeka na Anne Kilango Malecela, ambao waliandika ripoti zao tofauti na ile ya Kamati.
Katika ushauri wao kwa Spika walibainisha kuwa madai ya Malima kwamba ameshuhudia rais na waziri mkuu wanapewa dakika moja na nusu kila mmoja na mmiliki wa ITV anapewa dakika 10 hayakuwa na ukweli.
Akitoa uamuzi wake jana bungeni dhidi ya malalamiko yaliyowasilishwa kwake na Mengi kwa upande mmoja na Malima kwa upande mwingine, Sitta alisema pamoja na mbunge kuwa na kinga ya kisheria kwa yale anayotamka ndani ya Bunge, lakini kinga hiyo haipo iwapo atabainika kusema uongo.
Licha ya mbunge kuwa na uhuru wa kutoa maoni yake bungeni, lakini hakuna uhuru usio na mipaka na kwamba uhuru wa majadiliano bungeni nao pia una mipaka iliyowekwa na katiba na sheria nyingine za nchi, alisema.
Alisema ushahidi uliowasilishwa na pande hizo mbili Katika Kamati husika haukuweza kuthibitisha madai ya Malima. Kutokana na uamuzi huo, Sitta amemwagiza Katibu wa Bunge awasiliane na wahusika wakutane ofisini kwake Dar es Salaam waweze kuzungumza pamoja.