Habari Tanzania - http://www.habaritanzania.com
Makampuni ya kigeni yajitosa kukarabati kivuko
http://www.habaritanzania.com/articles/2868/1/Makampuni-ya-kigeni-yajitosa-kukarabati-kivuko
By Ramadhan Semtawa
Published on 02/8/2007
 
MAKAMPUNI matatu ya kigeni, yamejitosa kutaka kukifanyia matengeneza kivuko cha Mv Kigamboni ambacho kiko katika hali mbaya.

Na Ramadhan Semtawa

MAKAMPUNI matatu ya kigeni, yamejitosa kutaka kukifanyia matengeneza kivuko cha Mv Kigamboni ambacho kiko katika hali mbaya.

Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Ufundi na Umeme kutoka Wizara ya Miundombinu, John Ndunguru, aliyataja makampuni hayo kuwa ni Ms Johs Gram-Hanseen ( kutoka Denmark), Ms Dutchmed International B.V (Uholanzi) na Ms Neue Ruhr Stert Schiffsweft (Ujerumani).

Alisema makampuni hayo na la Ms Professional Marine Contractors LTD la hapa nchini, yaliyoomba zabuni hiyo baada ya kufunguliwa wiki iliyopita.

Ndunguru, alisema kinachofanyika kwa sasa ni kupitia zabuni hizo na kuona kampuni iliyokidhi vigezo vya kutengeneza kivuko hicho.

" Makampuni yaliyoomba ni manne, matatu ya kigeni, tayari zabuni imekwishafunguliwa, kinachofanyika sasa ni tathimini," alifafanua.

Kivuko cha Mv Kigamboni kinataka kufanyiwa matengenezo makubwa ambayo yatakifanya kusimama kazi kwa kipindi cha miaka miwili.

Tayari Wizara ya Miundombinu kupitia kitengo hicho cha umeme, kimetangaza zabuni ya kutafuta kivuko cha kukodi ambacho kitachukua nafasi ya Mv Kigamboni.

Moja ya vigezo ya kivuko hicho ni kutaka kiwe na uwezo wa kubeba abiria hadi 800 kwa wakati mmoja.

Mv Kigamboni kiko katika hali mbaya na mara kwa mara kimekuwa kikizima baharini na wakati mwingine kupoteza mwelekeo.