Na Simon Berege, Dodoma
WATAALAM wa Kikosi cha Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) cha 302, wamegundua kwamba baadhi ya wananchi wakijipenyeza kwa siri kwenye uwanja wa shabaha wa Shule ya Mafunzo ya Kijeshi ya Kalunde, mkoani Tabora na kukusanya mabomu yaliyochwa kwenye eneo hilo wakidhani ni vyuma chakavu.
Akiwasilisha taarifa ya hali ya uhalifu nchini bungeni jana, Waziri wa Usalama wa Raia, Bakari Mwapachu, alisema wachunguzi hao waliwahoji watu 14 na kubaini kwamba mizigo mingi ya chuma chakavu iliyogundulika kuwa na mabomu, ilitoka mkoani Tabora, hivyo walienda kufanya ukaguzi.
Alisema baada ya kupata mabomu hayo, uchunguzi umeonesha kwamba watu hao huyakusanya na kuyajumuisha na vyuma vingine chakavu, kisha kuvisafirisha
kwenda Dar es Salaam kwa wenye viwanda vya nondo ambako wahusika hushindwa kuyatambua mabomu hayo.
Uchunguzi huo unafuatia tukio la kulipuka kwa bomu moja katika eneo kiwanda cha nondo kilichoko wilayani Temeke, jijini Dar es Salaam Desemba 27, mwaka jana
Alisema ili kukabiliana na hali hiyo isitokee tena, Serikali iliunda timu iliyoshirikisha wajumbe kutoka jeshi la Polisi, Usalama wa Taifa , JWTZ , Mkemia
Mkuu wa Serikali, kuchunguza vyanzo vya mabomu na kushauri hatua za kuchukua ili tukio kama hilo lisitokee tena.
Mwapachu alisema kwamba hadi kufikia Januari mwaka huu, jeshi lilikwisha kagua
maeneo ya viwanda saba vinavyotengeneza nondo jijini Dar es Salaam.