Na John Stephen
MKUU wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali George Waitara amewaonya wanajeshi 80 walioondoka jana kwenda Lebanon kushiriki katika Jeshi la Umoja wa Mataifa la kulinda amani nchini humo, kutojiingiza kwenye vitendo vya uasherati, ulevi na anasa nyinigne ili kulinda afya zao na maslahi ya Taifa.
Jenerali Waitara alitoa onyo hilo jana katika kikosi cha Jeshi la Anga, Ukonga Dar es Salaam, wakati akiwakabidhi Bendera ya Taifa wanajeshi hao, kabla ya kuondoka na ndege ya Jordan kuelekea Lebanon. Kikosi hicho kiliagwa na ndugu, marafiki na familia zao.
Akizungumza na wanajeshi hao katika kikosi hicho, Jenerali Waitara aliwataka wanajeshi hao kuepuka kufanya kujiingiza kwenye anasa na starehe ambazo zinaweza kuhatarisha maisha yao ikiwemo kuambukizwa ukimwi.
"Epukeni anasa na starehe ili muweze kuboresha maisha yenu mtakaporejea nyumbani. Pia kumbukeni kwamba Taifa limewapa dhamana kubwa ya kuliwakilisha, hivyo natumaini mtaliletea Taifa sifa kubwa," alisema Jenerali Waitara.
Mkuu huyo alisisitiza kitendo chochote cha utovu wa nidhamu hakitavumiliwa kwa namna yoyote na kwamba endapo watafanya hivyo watakuwa wameliaibisha Taifa.
Akizungumzia maandalizi ya kuwapeleka wanajeshi hao Lebanon, Jenerali Waitara alisema kikundi hicho kiliandaliwa kwa muda wa miezi mitatu na kupatiwa mafunzo ya shughuli za kijeshi watakazofanya wakiwa huko.
"Maandalizi ni mazuri. Vifaa vitakavyotumika tayari vimeshaplekwa kwa meli nchini Lebanon, mnachotakiwa kufanya ni kutunza vifaa hivyo ili baadae viweze kutumika," alisema.
Waitara pia aliishukuru Serikali kwa kulirejeshea fedha zake ambazo lilitumia katika shughuli za kuwaandaa wanajeshi hao kwa kuwa fedha hizo zilikuwa kwenye bajeti yake ya kufanya mambo mengine.
Katika hatua nyingine, Meja Jenerali Hamisi Semfuko, alisema ni mara ya kwanza kwa JWTZ kupeleka kundi kubwa la wanajeshi, nje ya Afrika kwenda kulinda amani nchini Lebanon.
Serikali ya Tanzania imepeleka jumla ya wanajeshi 80 wakiwemo maafisa 11, askari 69 na kati yao wanawake 10, akiwemo afisa mmoja na askari tisa.
Sherehe hizo, zilihudhuriwa pia na mwakilishi wa Umoja wa Mataifa (UN), Robert Kuenstep kwa niaba ya Oscar Taranko.
Mapema mwaka huu Rais Jakaya Kikwete aliridhia kuwapeleka wanajeshi wa Tanzania nchini Lebanon kushirika katika operesheni ya kulinda amani chini ya usimamizi wa UN.
Hata hivyo uamuzi huo wa Rais Kikwete ulipingwa na wananchi kadhaa wakiwemo viongozi wa vyama vya upinzania wakidai kuwa ni kuhataria maisha ya askari wake kutokana na hali ilivyo nchini Lebanon.