Na Claud Gwandu, Arusha
JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC), itaanzisha kituo cha utafiti wa amani na utatuzi wa migogoro katika nchi za Kusini mwa Afrika.
Kituo hicho ambacho kitakuwa na ofisi kwenye makao makuu ya jumuiya hiyo mjini Arusha, kitaitwa Nyerere Peace Research Centre, kwa heshima ya Baba wa Taifa, Marehemu Mwalimu Julius Nyerere.
Kwa mujibu wa Msemaji wa EAC, Magaga Alot, uamuzi wa kuanzishwa kwa kituo hicho, ulifikiwa Februari 1, mwaka huu katika kikao cha Baraza la Mawaziri wa Jumuiya hiyo, kilichofanyika mjini hapa.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana, A lot, alisema kituo hicho kitashirikiana na Chuo Kikuu cha Arcadia cha Marekani katika shughuli za utafiti wa migogoro na usuluhishi.
Mkataba wa ushirikiano huo katika ya EAC na Chuo kikuu hicho, ulitiwa saini mwishoni mwa wiki iliyopita, katika makao makuu ya jumuiya hiyo.
Malengo ya kituo hicho, ni pamoja na kufanya utafiti kuhusiana na migogoro katika nchi za Afrika na kuwapa watunga sera serikalini, matokeo ya utafiti huo kwa ajili ya utekelezaji.
Kituo hciho kimepewa jina la Nyerere ikiwa ni kutambua na kuenzi mchango wake katika kutetea ukombozi wa nchi za Afrika na pia kazi za usuluhishi alizokuwa akizifanya wakati wa uhai wake katika nchi zenye migogoro kama Burundi.
Kabla ya kifo chake, Oktoba 14, mwaka 1999 kilichotokea katika hospitali ya Mtakatifu Thomas nchini Uingereza, Nyerere alikuwa Mwenyekiti wa Mazungumzo ya kutafuta Amani nchini Burundi, kati ya serikali ya nchi hiyo na waasi.