Milka Ezekiel na John Dotto, Singida
MAWAZIRI wanne wa serikali ya awamu ya nne waliokwenda kukagua ubovu wa barabara ya Dodoma-Singida walifika jana kwa helikopta ya jeshi na kujionea hali halisi ya barabara hiyo, lakini wakaondoka bila kutoa kauli yoyote.
Barabara waliyokwenda kukagua mawaziri hao imeharibika kwa kipindi kirefu sasa, ambapo magari zaidi ya 900 na maelfu ya watu wamekwama kutokana na ubovu wa barabara hiyo.
Kutokana na hali hiyo ambayo imekuwa kero kubwa kwa wasafiri, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Perseko Kone, aliwataka wanaotaka kusafiri kupitia barabara ya kati kuahirisha safari zao kwa muda hadi itakapoanza kupitika.
Barabara hiyo ndiyo pekee inayopitisha bidhaa mbalimbali yakiwemo mafuta kuingia nchi jirani za Burundi,Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) na hata Ugnda.
Kone alisema hali ni mbaya sana katika vijiji vya Isuna na Mkiwa na maeneo ya Kaminyanga, ambako kuna magari mengi na watu wamekwama.
Aliwataka wasafiri hao kuwa watulivu wakati serikali inafanya jitihada za kuwanasua.
Pia kutokana na kero hiyo, wasafiri wanaopita njia ya Kaskazini kupitia kenya na Uganda kwenda mikoa ya Kanda ya Ziwa, wameongezeka.
Jana watu 13 waliripotiwa kufariki dunia baada ya basi la Spider lililokuwa likisafiri kutoka Mwanza kuja Dar es Salaam kugonga na uso kwa uso na daladala moja katika eneo la Kisii nchini Kenya.
Basi la Spider liliondoka Mwanza jana asubuhi kabla ya kupata ajali hiyo huko Kisii likielekea Nairobi ambapo inadaiwa kwamba watu wote waliofariki walikuwa kwenye daladala.
Mawaziri waliotembelea barabara hiyo ni Miundombinu,Andrew Chenge, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,Mizengo Pinda, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Profesa Juma Kapuya na Waziri wa Usalama wa Raia, Bakari Mwapachu.
Mawaziri hao walizunguka hewani kukagua barabara hiyo, hasa katika maeneo ya Mkiwa, Kamenyanga, Itigi na Manyoni.
Baada ya kuzunguka na kujionea ubovu huo, mawaziri hao walitua katika eneo la Isuna wilaya ya Singida Vijijini, ambapo madreva wa magari yaliyokwama, abiria na baadhi ya wananchi wa maeneo hayo walikusanyika ili kusikiliza tamko la serikali kuhusu barabara hiyo lakini waliambulia patupu.
Kilichowashangaza wananchi ni kuona mawaziri hao hawako tayari kuzungumza chochote wala kutoa kauli ya serikali juu ya tatizo hilo.
Aliyeokoa jahazi ni Mkuu wa Mkoa huo, aliyekuwa ameongozana na mawaziri hao, ambaye aliwaambia waandishi wa habari kwamba kauli ya Serikali juu ya tatizo hili itatolewa baada ya mawaziri hao kupeleka taarifa kwa Waziri Mkuu, Edward Lowasa, ambaye ndiye aliwatuma kukagua barabara hiyo.
Kone alisema kuwa ingawa bado kuna magari mengi yaliyokwama katika msururu mrefu katika umbali wa kilomita14, hivi sasa baadhi ya magari yameanza kupita kidogo kidogo baada ya wakandarasi wanaojenga wa barabara hiyo, SIETCO, kuamriwa na serikali mkoani hapa kufanya ukarabati wa muda kwenye sehemu korofi ili angalau ipitike kwa dharura.
Abiria na madreva wamelaani vikali kitendo cha mkandarasi huyo kwa kutoijali barabara hiyo, kutotengeneza sehemu korofi na kusababisha wao kushindwa kabisa kuendelea na safari zao ambapo wamekwama kwa siku tatu hadi sita.
Abiria hao waliitaka serikali kuangalia uwezekano wa kuchukua hatua mathubuti ili kukarabati barabara hiyo, vinginevyo inaweza kuathili uchumi wa nchi kwa kuwa inachangia kwa kiasi kikubwa katika kuingiza pato la taifa.
Jeshi la Polisi mkoani hapa limepeleka kikosi cha askari katika eneo la tukio, ili kuimarisha ulinzi kutokana na sehemu hizo kuwa na watu wengi pamoja na magari.
Vile vile hospitali ya mkoa imepeleka madaktari na dawa kutokana na hofu ya kuzuka kwa magonjwa ya milipuko