Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  RVF:Tanzania yazuia mifugo kuingia Kenya
RVF:Tanzania yazuia mifugo kuingia Kenya
By Habari Tanzania | Published  02/8/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:

Na Claud Gwandu, Arusha

SERIKALI imepiga marufuku yake kwenda nchini Kenya na kuhamisha mifugo kiholela nchini ikiwa ni hatua ya tahadhari yakukabiliana na ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa (RVF) ambao hadi sasa umesababisha vifo vya watu wawili nchini.

Kutokana na agizo hilo, mifugo itakayohamishwa kutoka mikoa ya Kanda ya Kaskazini ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro kwenda sehemu nyingine ya nchini italazimika kupewa kibali cha madaktari wa mifugo baada ya mifugo hiyo kukaguliwa kiafya na kuonekana kuwa haina tatizo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo, Anthony Diallo, alisema kuwa hatua hiyo itaanza rasmi leo baada ya Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo katika wizara hiyo kutoa taarifa kisheria.

Diallo ambaye pamoja na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Profesa David Mwakyusa walikuwa mjini hapa kukutana na viongozi wa mikoa hiyo na wilaya zake, alisema kuwa ingawa taarifa za awali za marehemu wawili zinaonyesha kuwa walikufa kwa ugonjwa huo, bado majaribio mengine ya kimaabara yanasubiriwa, ili matokeo yake yathibitishe ugonjwa huo au la.

“Ni kweli kuna vifo vya watu wawili waliokufa kwa ugonjwa huo lakini bado tunasubiri majaribio mengine ya kimaabara kuthibitisha au kubaini kama kweli watu hao walikufa kwa ugonjwa huo au la,” alisema Diallo.

Alifafanua kuwa utafiti wa awali uliofanywa katika maeneo waliyotoka marehemu hao, kwa mifugo waliyokuwa nao na jamaa zao haukuonyesha kuwa nao wameambukizwa ugonjwa huo, jambo linalohitaji uchunguzi zaidi katika maabara.

Marehemu hao ni Nashiel Molle (45), mkazi wa Makuyuni katika wilaya ya Monduli mkoani Arusha na Yesaya Kupela (39), mkazi wa kijiji cha Terat kilichopo wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara ambao walikufa Januari 31, mwaka huu katika hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru.

Kauli hiyo ya Waziri Diallo inaonesha kupingana na kauli ya Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Evance Balama aliyetangaza awali taarifa ya serikali ya kuingia kwa ugonjwa huo nchini.

Balama katika taarifa aliyokaririwa na vyombo vya habari alisema uchunguzi wa madaktari na wataalam wa afya juu ya vifo hivyo, umethibitisha kuwa watu hao walikufa kwa ugonjwa huo, ambao kwa kifupi unaitwa RVF .
“Wataalam wetu wamethibitisha kuwa vifo vya watu hao vimetokana na ugonjwa hatari wa homa ya bonde la ufa na hiyo ni dalili kwamba inawezekana ugonjwa huo umeingia nchini..., lakini serikali imechukua tahadhari zote zinazostahili,” alisisitiza Balama.

Akifafanua, alisema taarifa za awali zinaonyesha kuwa Kupela alikula nyama ya mbuzi kati ya Januari 24 na 25 na baada ya siku tatu alianza kuumwa, ndipo alipokimbizwa hospitali ya mkoa kwa matibabu, ambako iligundulika kuwa ameambukizwa ugonjwa huo.

Katika kipindi hicho pia mgonjwa mwingine kutoka Makuyuni, wilayani Monduli ambaye alikuwa na dalili za ugonjwa huo, alifikishwa hospitalini hapo na alifariki siku hiyo hiyo.

Kutokana na kufariki kwa wagonjwa hao, sampuli za damu za marehemu hao zilipelekwa Kenya kwenye kituo cha utafiti wa magonjwa ya binadamu cha CDC, kilichopo Nairobi, kwa uchunguzi zaidi.

Alieleza kuwa kituo hicho kiliandika barua ya majibu ya sampuli za damu za marehemu hao juzi, ambayo ilithibitisha kuwa wote walikufa kutokana na kuambukizwa ugonjwa huo hatari.


Diallo alisema juzi katika kituo cha afya cha Holili mkoani Kilimanjaro raia mmoja kutoka Kenya alifikishwa hospitalini hapo kutafuta matibabu lakini alifariki baadaye na kurudishwa kwao Kenya akidhaniniwa kufa kwa Homa ya Bonde la Ufa.

Akifafanua zaidi, Waziri huyo alisema serikali imeagiza halmashauri za Manispaa, Miji na Wilaya katika mikoa hiyo mitatu kupunguza idadi ya maduka yanayouza nyama ili iwe rahisi kusimamia hali ya usafi katika maduka hayo.

Alisema imeonekana kuwa utiriri wa maduka hayo ya nyuma unaweza kuchangia ongezeko la hatari ya ugonjwa huo ambao hadi sasa hauna tiba lakini akawataka viongozi wa halmashauri hizo watende haki ili ushindani katika biashara hiyo uendelee.

Alisema halmashauri hizo zimetakiwa kusimamia kwa ukamilifu usafi katika biashara ya nyama kuanzia machinjioni hadi katika maduka ya nyama ili kusiwepo na mwanya wa maambukizi ya ugonjwa huo.

Pia aliwataka wananchi kuacha kununua nyama ambazo hazijapita katika maduka yanayosimamiwa na halmashauri zao na wasikubali kununua au kula nyama ambayo hawajui chanzo chake.

Alisema serikali tayari imetoa dozi 500,000 kwa ajili ya kampeni ya kuchanja mifugo hasa mbuzi na kondoo ambao ndio wanaoshambuliwa zaidi na maradhi hayo na kiasi kingine cha dawa ya chanjo kimeagizwa nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kudhibiti ugonjwa huo.

Diallo aliwataka wananchi wasitumie maziwa ambayo hayajachemshwa vya kutosha wala kula nyama yenye damu damu na kushauri kwamba wananchi wale nyama ilivyochemshwa vizuri ili kuepuka ugonjwa huo.

Akizungumza katika mkutano huo, Profesa Mwakyusa alisema tangu kuzuka kwa ugonjwa huo nchini Kenya, Wizara yake imekuwa na mawasiliano ya mara kwa mara ya kuangalia namna ya kushirikiana katika kudhibiti maambukizi hasa kwa wafugaji wanaoishi maeneo ya mipaka ya nchi hizo kutoka Tanga hadi Mara.

Profesa Mwakyusa alisema kwa sasa wananchi hawana sababu ya kuwa na wasiwasi kwa kuwa wataalam wa wizara hiyo, Shrika la Afya Duniani (WHO) na kituo cha udhibiti wa magonjwa cha Nairobi nchini Kenya
wanashirikiana kuchunguza ugonjwa huo.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.