POLISI jijini Dar es Salaam wanamtafuta dereva wa gari lenye namba T167 ALD Toyota Surf kwa tuhuma za kuwagonga watoto watatu wa Shule ya Msingi Kumbukumbu na kusababisha kifo cha mmoja wao.
Mtoto aliyekufa ni Sarafina Omary, ambaye alikufa papo hapo wakati Upendo Akio na Sharifa Ali walijeruhiwa vibaya.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Jamal Rwambow alisema jana kuwa dereva huyo baada ya kuwagonga watoto hao wakati wakivuka barabara ya Kawawa eneo la Morocco juzi. Alisema watoto waliojeruhiwa wamelazwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na hali zao sio nzuri na mwili wa mtoto aliyefariki umehifadhiwa katika hospitali hiyo.
Katika tukio jingine lililotokea jana, dereva wa daladala lenye namba T431 ADG, Toyota Costa alikimbia baada ya kumgonga na kusababisha kifo cha mtu asiyefahamika maeneo ya Buguruni Rozana.
Wakati huohuo mtoto Emanuel Amir (2) alikufa juzi jioni baada ya kutumbukia kwenye kisima wakati akicheza na watoto wenzake maeneo ya nyumbani kwao, Kipunguni Kisiwani. Kamanda Masindoki alisema mtoto huyo alikufa baada ya kunywa maji mengi na mwili wake umehifadhiwa hospitali ya Amana.