BUNGE limeishauri Serikali kurejesha mafunzo ya lazima ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa vijana wanaomaliza kidato cha sita na chuo kikuu.
Kamati ya Ulinzi na Usalama katika ripoti yake iliyowasilishwa bungeni jana ilieleza kuwa mafunzo hayo ni muhimu kurejeshwa na ikaomba serikali kulifanyia kazi agizo hilo ili utekelezaji wake uanze mwaka ujao wa fedha. Mwenyekiti wa Kamati hiyo, William Kusila alisema, "Kwa kuanzia kamati inashauri kwamba utaratibu huu uanze kwa kuwachukua vijana wote waliohitimu chuo kikuu."
Alisema kwa kuwa sheria ya vijana kujiunga na JKT kwa lazima bado ipo Serikali ianze utekelezaji wake haraka. Kusila alisema sambamba na ushauri huo ni maoni ya kamati kuwa JKT ipanuliwe kwa lengo la kuwa na kambi kila wilaya ili kutoa mafunzo ya ufundi na ulinzi kwa vijana.
Kamati hiyo imetoa pendekezo hilo ikisema kuwa JKT ni taasisi pekee ambayo ilileta mshikamano katika nchi, jambo linalohitajiwa kwa sasa kuimarisha uzalendo miongoni mwa Watanzania suala ambalo nchi inajivua kwa miaka mingi. Katika ripoti hiyo, kamati imesema iwapo JKT ikiimarishwa ipasavyo vijana wengi watapata ajira kwa kuajiriwa au kujiajiri wenyewe baada ya kumaliza mafunzo hayo.
Kamati hiyo pia imeshauri Serikali iangalie uwezekano kwa siku zijazo kupeleka fedha za mikopo kwa vijana kupitia JKT kama ilivyo kwa fedha zinazopelekwa mikoani ili wanaohitimu mafunzo na stadi mbalimbali za watu wapewe mikopo ya vifaa na mitaji ya kuanzisha shughuli za uchumi.
Alisema utaratibu huo utakuwa na matokeo mazuri zaidi kwa kuwa watakaokopeshwa watakuwa na ujuzi wa kuzalisha mali na hivyo kuweza kurejesha mikopo hiyo.
Kuhusu mpango wa sasa wa kufufua JKT, Kusila alisema mpango huo unaohusisha vijana wanaojitolea umeonyesha mafanikio makubwa. Katika kambi ambako kamati yake ilizuru iliona namna vijana wanavyofanya kazi za uzalishaji mali pamoja na utunzaji wa mazingira, alisema. Alisema kamati yake ilishuhudia ukakamavu, nidhamu na usafi vitu ambavyo ni muhimu kwa vijana ambao ndilo kielelezo cha uhai wa taifa.
Hata hivyo alisema wakati kamati yake ilipotembelea kisiwa cha Pemba iligundua kuwa kisiwa hicho hakina kituo cha uhamiaji katika bandari ya Pemba. Alisema uingiaji na utokaji wa wageni katika kisiwa hicho umekuwa unaongezeka jambo alilodai ni hatari kwa usalama wa nchi.
Katika ripoti hiyo pia, kamati hiyo imeeleza namna ilivyobaini kuwapo kwa polisi wachache katika vituo vya mpakani tofauti na nchi jirani ya Kenya ambayo vituo vyake vina polisi karibu 200 huku Tanzania ina polisi tisa tu.
Kuhusu wakimbizi kamati hiyo imeshauri wakimbizi hao kurejea kwao kwa vile katika nchi wanazotoka tayari kuna amani. Pia kambi zote ambazo hazihudumiwi na mashirika ya kimataifa kamati imeshauri zifungwe.
Pamoja na kwamba mipaka ni shwari, lakini kamati hiyo imeshauri Serikali ihakikishe barabara za mikoa ya mipakani zinapitika wakati wote wa mwaka kurahisisha shughuli za ulinzi na za biashara kati ya Tanzania na nchi majirani.