SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), limependekeza kima cha chini cha mshahara kwa mtumishi wa umma nchini uwe Sh 315,000 kwa mwezi. TUCTA imemweleza Rais Jakaya Kikwete kuwa huo ni mshahara anaostahili kulipwa mtumishi aweze kumudu gharama za maisha kama za chakula, mavazi, elimu kwa watoto, nishati, malazi, matibabu na gharama nyingine.
Uchunguzi wa HabariLeo umebaini kuwa hayo yamo katika mchanganuo ambao TUCTA imempelekea Rais Kikwete kupitia Tume aliyoiunda kushughulikia uboreshaji wa maslahi ya watumishi wa umma. Tume hiyo iliyoongozwa na aliyewahi kuwa Katibu Mkuu katika Wizara ya Utumishi, Deogratius Ntukamazina ilikabidhi ripoti yake kwa Rais, Januari 22 mwaka huu.
Rais aliunda Tume hiyo Mei 18 mwaka jana, na alipokabidhiwa ripoti yake, aliahidi kuisoma, kuitafakari na kuifanyia kazi ili kuboresha maslahi ya wafanyakazi na wiki iliyopita alisisitiza kuwa anaendelea kuifanyia kazi ingawa inaweza kuchukua muda kabla ya utekelezaji wake.
Katika mapendekezo yake, TUTCA imesema kwamba mtumishi mwenye mke au mume na watoto wanne wenye umri wa chini ya miaka 18 anahitaji si chini ya Sh 31, 275 kwa mwezi kwa ajili ya a kifungua kinywa na Sh 53, 675 za chakula cha mchana. Shirikisho hilo linaundwa na vyama 14 vya wafanyakazi na linakadiriwa kuwa na wanachama wasiopungua 360,000 nchi nzima.
Katibu Mkuu wa TUCTA, Nestory Ngulla, jana alithibitisha kuwa Oktoba mwaka jana, Shirikisho hilo lilikabidhi mchanganuo huo kwa Tume ya Ntukamazina iliyokuwa na makamishna 11.
Ngulla alisema, kima cha chini cha mshahara cha Sh 35,000 kwa wafanyakazi wa mashambani na Sh 48,000 kwa wafanyakazi wa mijini ni kama utani kwa vile hakiwawezeshi kumudu hata nusu ya gharama za msingi za maisha ya kila siku.
Kwa mujibu wa Ngulla, kiwango kilichopendekezwa ni matokeo ya utafiti uliofanywa mwaka jana wa mahitaji ya msingi ya mtumishi kwa kuzingatia bei za bidhaa kwa wakati huo.
“Kama kweli tunataka kila mtumishi aliyeajiriwa aweze kulipwa minimum wage (kima cha chini) inayostahili, sisi tunaamini kuwa Sh 315,000 ndiyo anastahili kulipwa kwa kuwa ndiyo kinaweza angalau kumsaidia muhusika kwa wakati huo,” alisema Ngulla.
Mchanganuo huo umebainisha kwamba, mtumishi anahitaji kulipwa mshahara wa Sh 315,000 kwa mwezi ili pia apate Sh 30,000 za kulipa kodi ya nyumba yenye vyumba vitatu, kimoja akitumie yeye na mumewe au mkewe, kingine watoto wa kike na kinachobaki cha watoto wa kiume.
TUCTA pia imesema, kiwango hicho kitamwezesha pia mtumishi kupata Sh 4,500 za umeme, mafuta ya taa, na mishumaa kwa vyumba vitatu, Sh 6,000 za maji ya matumizi mbalimbali na Sh 4,250 kwa ajili ya kununua sabuni, dawa ya meno, mafuta ya kupaka watu sita.
Kwa mujibu wa mchanganuo wa TUCTA, kima cha chini cha mshahara cha mtumishi wa mjini au mashambani ni kidogo kuliko mahitaji ya chakula cha jioni cha mwezi mmoja cha mtumishi.
TUCTA inaamini kuwa mtumishi anahitaji kiwango cha chini cha Sh 4,189.67 kwa siku kwa ajili ya chakula cha jioni au Sh 58,475 kwa mwezi kwa ajili ya mtumishi huyo, mke au mume na watoto wanne wenye umri wa chini ya miaka 18.
Ngulla alisema mtumishi mmoja anahitaji kiwango cha chini cha Sh 141, 425 kwa mwezi za chakula cha mchana, jioni na kifungua kinywa. Rais ameambiwa pia kwamba mtumishi anayekwenda na kurudi kutoka kazini kwa mabasi anatumia kiwango cha chini cha Sh 25,000 kwa mwezi ikiwa atalipa Sh 250 kwa safari moja.
Kwa mujibu wa mchanganuo huo wa TUCTA mtumishi anayesomesha watoto wanne shule ya msingi anatumia kiwango cha chini cha Sh 29,000 kwa ajili ya nauli, sare za shule na madaftari.
Katibu Mkuu wa TUCTA alisema jana kuwa, familia ya mtumishi huyo inahitaji kiwango cha chini cha Sh 15,000 kwa mwezi kwa ajili ya mavazi ya watu sita na Sh 180,000 kwa mwaka kununulia mavazi, na Sh 20,000 za malazi kununua vitanda, magodoro, shuka, na vyandarua.
Ngulla pia alisema, mtumishi mmoja akilipwa kiwango kilichopendekezwa kitamwezesha kupata Sh 30,000 za tiba ya watu sita kwa mwezi na Sh 9,000 za dharura.
Kutoka: Habari Leo