Na Nora Damian
ULINZI wa Mkuu wa Mkoa wa zamani wa Tabora, Ditopile Mzuzuri, utaimarishwa na polisi ili kuwadhibiti watu wanamzunguka na kumfunika khanga mahakamani, kwa ajili ya usalama wake.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Charles Kenyella, wakati akizungumza na gazeti hili kufuatia vitendo hivyo.
Alisema kufanya hivyo ni kosa, kwani watuhumiwa wa aina hiyo wanatakiwa kulindwa kwa ajili ya usalama wao, kwa kuwa si rahisi kutambua anayemfikia ana lengo gani.
Alisema kosa hilo limetokana na polisi wanaofika mahakamani hapo, kudhani kuwa watu wanaomkaribia mtuhumiwa huyo ni ndugu zake na kwamba wangeweza kuwa wastaarabu, lakini wameshindwa kuonyesha hilo.
"Hatukutarajia kitu cha namna hiyo, lakini sasa kimetokea, ninachoweza kusema ni kwamba hakitarudiwa tena," alisema Kenyella.
Kenyella aliyasema hayo muda mfupi baada ya Hakimu Mkuu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Sivangilwa Mwangesi, kuitisha mkutano wa waandishi wa habari na kuwashutumu polisi kwa kushindwa kudhibiti vitendo vinavyofanywa na watu wanaodai kuwa ndugu wa Ditopile.
Pamoja na kumzunguka mtuhumiwa huyo na kumfunika khanga, watu hao wamekuwa wakiwashambulia na kuwatukana waandishi wa habari kwa kuripoti kuhusiana na kesi hiyo yenye mvuto kwa jamii.
Mwangesi alisema kuwa polisi walionyesha uzembe, kwani hawakuwajibika ipasavyo tukio hilo lilipotokea.
Alisema kuwa sheria hairuhusu watu kufanya kitendo kama hicho mahakamani na kwamba ulikuwa ni utovu wa nidhamu.
“Kitendo walichokifanya, sisi kama mahakama tunakilaani, kwani sheria hairuhusu watu kufanya hivyo mahakamani,” alisema Mwangesi.
Juamatatu ya wiki iliyopita, ndugu wa Ditopile ambaye anayekabiliwa na kesi ya maujaji, walisababisha mtafaruku mkubwa katika Mahakama ya Kisutu, baada ya kufanya fujo na kuwatukana waandishi wa habari kwa madai kuwa wanafuatilia sana kesi hiyo.
Wakati mtuhumiwa huyo akivuta hatua kuingia mahakamani hapo, baadhi ya ndugu hao walianza vioja vyao kwa kumvamia na kumfunika kwa kanga mtuhumiwa huyo ili kuwazuia wapiga picha wasimpige picha.
Huku wengine wakiwa wamemfunika kwa kanga, ndugu wengine waliokuwa wamekaa kwenye viti walitoa lugha chafu na za kejeli na matusi mazito dhidi ya waandishi wa habari waliokuwa kazini.
Ditopile alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Novemba 6, chini ya ulinzi mkali wa polisi akikabiliwa na shitaka la mauaji ya dereva wa daladala Hassan Mbonde.
Inadaiwa kuwa Novemba 4, mwaka huu, majira ya saa 1:00 usiku, katika eneo la njia panda ya Bagamoyo na Kawe wilayani, Kinondoni dereva huyo wa daladala. Kesi hiyo itatajwa tena Februari 12 mwaka huu.