Na Claud Gwandu, Arusha
UGONJWA wa homa ya bonde la ufa (Rift Valley Fever) ambao umekuwa ukitikisa nchini Kenya umeingia nchini na tayari umeau watu wawili mkoani Arusha.
Serikali mkoani hapa imethibitisha kuingia nchini kwa ugonjwa huo usiokuwa na tiba.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Evance Balama, alisema serikali tayari imechukua hatua za kukabiliana na ugonjwa huo.
Aliwataja waliokufa kutokana na homa hiyo kuwa ni Naishie Mollel (45) mkazi wa Makuyuni wilayani Monduli na Yesaya Kupela (39) wa Terat katika Manispaa ya Arusha.
Balama ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Arusha, alisema kuwa taarifa za kuwapo kwa ugonjwa huo zilianza kujitokeza pale watu hao kufikishwa katika hospitali ya mkoa wa Arusha ya Mount Meru wakiwa na dalili za ugonjwa huo na kufariki Januari 31, mwaka huu.
Alisema uchunguzi wa madaktari na wataalam wa afya wa vifo hivyo, umethibitisha kuwa watu hao walikufa kwa ugonjwa huo ambao kwa kifuipi unaitwa RVF .
“Wataalam wetu wamethibitisha kuwa vifo vya watu hao vimetokana na ugonjwa hatari wa homa ya bonde la ufa na hiyo ni dalili kwamba inawezekana ugonjwa huo umeingia nchini...lakini serikali imechukua tahadhari zote zinazostahili,” alisisitiza Balama.
Akifafanua, alisema taarifa za awali zinaonyesha kuwa Kupela alikula nyama ya mbuzi kati ya Januari 24 na 25 na baada ya siku tatu alianza kuumwa na ndipo alipokimbizwa hospitali ya mkoa kwa matibabu ambako iligundulika kuwa ameambukizwa ugonjwa huo.
Katika kipindi hicho pia mgonjwa mwingine kutoka Makuyuni wilayani Monduli ambaye alikuwa na dalili za ugonjwa huo alifikishwa hospitalini hapo na alifariki siku hiyo hiyo.
Kutokana na kufariki kwa wagonjwa hao, sampuli za damu za marehemu hao zilipelekwa Kenya kwenye kituo cha utafiti wa magonjwa ya binadamu cha CDC kilichopo Nairobi kwa uchunguzi zaidi.
Alieleza kuwa kituo hicho kiliandika barua ya majibu ya sampuli za damu za marehemu hao juzi ambayo ilithibitisha kuwa wote walikufa kutokana na kuambukizwa ugonjwa huo hatari.
Kuhusu hatua walizochukua kukabiliana na ugonjwa huo, Balama alisema wamesitisha shughuli za uchinjaji wa wanyama katika maeneo yote ambayo dalili za ugonjwa huo zimeripotiwa na pia kuzuia usafirishaji wa mifugo kutoka katika maeneo hayo.
Pamoja na hatua hiyo, alisema timu ya madaktari na wataalam wa magonjwa ya mifugo tayari imepelekwa katika maeneo yanayotiliwa shaka kuwa na dalili za ugonjwa huo kwa ajili ya utafiti zaidi.
Kaimu Mkuu huyo wa mkoa aliwataka wananchi kuacha kula nyama ya ng’ombe, mbuzi na kondoo na badala yake watumie zaidi samaki na mbogamboga za maji hadi ugonjwa huo utakapodhibitiwa kikamilifu.
Dalili za ugonjwa huo unaosababishwa na virusi vinavyoitwa Phlebovirus, ni kuwa na homa kali, kuumwa kichwa, maumivu ya mwili, kichefuchefu, kizunguzungu na kupungua uzito na kutokwa damu katika sehemu mbalimbali kwa wale waliozidiwa.
Kwa wanyama dalili za ugonjwa huo ni homa kali na kuzubaa, kuharibika mimba, na wanyama kuharisha damu.
Ugonjwa huo unasababishwa na mbu ambao wameambukuziwa virusi hivyo na kwa kula nyama ya mnyama mwenye virusi, kwa kushika damu, majimaji kutoka mwili wa mnyama na mtu aliyeambukizwa.
Mwezi uliopita, serikali ilitoa tahadhari kuhusiana na ugonjwa huo na kuwataka wananchi kuchukuwa tahadhari kufuatia uwezekano wa ugonjwa huo kuingia nchini.
Tahadhari hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo, Charles Nyamrunda,, ikieleza dalili na jinsi ya kujilinda na ugonjwa huo.
Alisema ugonjwa mara nyingi hutokea baada ya mvua nyingi na mafuriko yanayofuatia ukame wa muda mrefu.
Kwa mujibu wa Nyamrunda, uchunguzi uliofanywa na Shirika la Kilimo na Chakula Duniani (FAO) unaonyesha kuwa maeneo yaliyo na hatari zaidi ya kuambukizwa na ugonjwa huo ni pamoja na Kenya, Kusini mwa Somalia, Kusini na Kusini Mashariki mwa Ethiopia, Kusini mwa Sudan na Kaskazini mwa Tanzania.
Ugonjwa huo umeleta madhara makubwa Kenya na hadi Januari 15, mwaka huu, watu 142 walikuwa wameugua na 78 kati yao walikuwa wameshapoteza maisha.
Vile vile mifugo mingi ikiwa ni pamoja na ng’ombe 500, mbuzi 1,500, kondoo 1,500 na ngamia 500 walikuwa wameugua na baadhi yao kufa kutokana na ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa Nyamrunda, ugonjwa huo ni hatari na unaweza kusababisha vifo kwa maelfu ya mifugo na mamia ya watu kama ilivyotokea katika nchi ya Misri.
“Virusi hivi huweza kuishi kwenye mayai ya mbu aina ya aedes, ambayo yana tabia ya kuishi kwenye vumbi kwa muda mrefu na kuanguliwa wakati wa mafuriko.
Baada ya kuanguliwa mbu hawa husambaza ugonjwa kwenye mifugo na kwa watu wakati wanapofyonza damu. Mbu aina nyingine kama vile Culex, Mansonia, Anopheles, na Eretmapodites wanaweza kusambaza virusi vya ugonjwa kati ya wanyama na wanyama na kati ya wanyama na binadamu,” alisisitiza Nyamrunda.
Alisema binadamu wanaweza kupata ugonjwa kupitia kugusa damu au majimaji ya aina nyingine ya wanyama wakati wa kuchinja, kuzalisha wanyama wagonjwa, kushika vitoto vya mbuzi au kondoo vilivyokufa au kutokana na kula vyakula visivyopikwa vizuri vitokanavyo na wanyama wagonjwa au wenye virusi.
Alizitaja dalili za ugonjwa huo kuwa katika wanyama ni kuharibika kwa mimba kwa wingi hususan katika kondoo na ngamia na vifo vingi vya ghafla kwa karibu asilimia 90 ya mbuzi na kondoo wachanga.
Kwenye mbuzi na kondoo wakubwa dalili za ugonjwa ni pamoja na kutapika, kutokwa makamasi yenye damu na kuharisha, rangi ya njano kwenye ngozi ya ndani inayofunika macho, midomo na sehemu za uzazi na vifo katika asilimia 10 hadi 20 ya wanyama hawa. Ng’ombe hawaugui sana kama ilivyo kwa mbuzi na kondoo.
Kwa upande wa binadamu dalili zake alizitaja kuwa ni pamoja na kuumwa kichwa, kuumia macho wakati yanapoangalia mwanga mkali, mafua, homa kali, tumbo kuuma, kutapika na wakati mwingine kutapika damu.
Kwa mujibu wa Nyamrunda, virusi vya ugonjwa huo huchukua muda wa siku mbili hadi sita tangu kuingia mwilini hadi kuanza kuonyesha dalili na ugonjwa unaweza kusumbua kwa muda wa siku tatu hadi saba au zaidi na kwamba vifo kwa binadamu vinaweza kutokea baada ya virusi vya ugonjwa huo kushambulia ubongo na viungo vingine vya mwili ambapo husababisha kuvuja damu.
Aliwataka wananchi watoe taarifa kwa wataalam wa mifugo walioko katika maeneo yao endapo wataona dalili za ugonjwa wa aina hii katika mifugo yao.