Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  IGP atimua wawili kitengo cha kuzuia dawa za kulevya
IGP atimua wawili kitengo cha kuzuia dawa za kulevya
By Habari Tanzania | Published  06/16/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
Ni kwa wizi wa vielelezo vya sh. milioni 90
 
Na Ramadhan Mkoma
 
POLISI wawili wa Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya wamefukuzwa kazi kuanzia jana kwa tuhuma za wizi wa dawa hizo, zenye thamani ya sh. milioni 90 ambazo ni vielelezo ambapo mmojawapo tayari amekutwa amenunua nyumba.
 
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna wa Polisi, Robert Manumba, alitangaza uamuzi huo jana, katika mkutano na waandishi wa habari, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya jeshi hilo, jijini Dar es Salaam.
 
Aliwataja askari hao ambao walikuwa lindo siku ya tukio kuwa ni F. 7153 Konstebo Kachero, Dickson Muganyizi (22) na F. 6869 Konstebo Kachero Waryuba Nyahurya (24), wote kutoka kitengo hicho kilichopo, barabara ya Kilwa mjini Dar es Salaam.
 
Kwa mujibu wa Manumba, askari hao pamoja na mtu ambaye hamkumtaja jina, wanatuhumiwa kuiba vielelezo hivyo, ambavyo ni kilo 5.2 za dawa za kulevya aina ya Heroin na Cocaine, vilivyokuwa vimehifadhiwa katika chumba maalum.
 
Manumba alisema dawa hizo zina thamani ya sh. milioni 90 kwa bei ya mtaani na ziliibwa baada ya kuvunjwa kwa dari ya chumba ambacho zilikuwa zimehifadhiwa.
 
Akielezea tukio hilo, Kamishna Manumba alisema wizi huo uligundulika Juni 13 mwaka huu, saa 3 asubuhi na Mkuu wa Kitengo hicho, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Afwilile Mponi.
 
"Uchunguzi umebaini kwamba askari hao walifanya uhalifu huo, kwa kuvunja ofisi na kuiba, siku waliyokuwa wamepangwa zamu ya ulinzi kwenye ofisi hiyo.
 
"Kufuatia tukio hilo, pamoja na matokeo ya uchunguzi, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Saidi Mwema, amewafukuza kazi askari hao wawili leo (jana) na baadaye watafikishwa mahakamani kujibu mashitaka ya makosa waliyotenda kuhusiana na wizi wa vielelezo hivyo," alifafanua Kamishna Manumba.
 
Kamishna Manumba alisema hatua hiyo, imechukuliwa ikiwa ni juhudi zinazofanywa na IGP katika kupambana na vitendo viovu vinavyofanywa na askari wasiokuwa waaminifu, wanaolifedhehesha jeshi na serikali kwa ujumla.
 
Akifafanua Manumba alisema kukamatwa kwa askari hao, kunafuatia uchunguzi uliokwenda sambamba na upekuzi uliofanywa katika makazi yao.
 
Manumba alisema katika upekuzi huo, watuhumiwa walikutwa na fedha, vyombo vya thamani ikiwa ni pamoja na seti za muziki ambazo hazilingani na vipato vya askari hao.
 
Hata hivyo, alisema ni mapema mno kutaja kiwango cha fedha walichokutwa nacho askari hao.
 
Mbali na vyombo hivyo, mtuhumiwa Muganyizi pia alikutwa akiwa tayari amenunua nyumba katika kipindi hicho kifupi.
 
Kamishna Manumba alilielezea tukio hilo kuwa la aibu, kubwa na la kwanza kutokea katika historia ya kitengo hicho nyeti.
 
Askari hao walikuwa katika depo moja katika Chuo cha Polisi cha Kimataifa cha CCP, Moshi mkoani Kilimanjaro na kuhitimu Februari 25 mwaka 2005 kabla ya kupangiwa kazi katika kitengo hicho maarufu kama 'Anti Drug Unit' kilichopo barabara ya Kilwa.
 
Tukio hilo ambalo, limezidi kulipaka matope jeshi hilo, limepokelewa kwa masikitiko makubwa na baadhi ya askari wakiwemo wa vyeo vya juu.
 
Mmoja wa askari hao alisikika akisema kwamba limetokea wakati mbaya, hasa ikizingatiwa jeshi hilo liko katika hatua za kujisafisha kutokana na wimbi la kashfa linalokwenda sambamba na matukio ya ujambazi.

How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.