MKUU wa Wilaya ya Kahama, Kanali Kelvin Msemwa, amesema utaratibu mbovu uliowekwa na wakala walioteuliwa na halmashauri, ndio kikwazo cha mbolea ya ruzuku kuwafikia wakulima.
Akizungumza juzi katika kikao cha Baraza la Madiwani baada ya kubainika kuwa pembejeo hiyo muhimu haikuwafikia wakulima, Msemwa alisema ugawaji wa mbolea ya ruzuku kupitia mawakala unafanywa kibiashara zaidi.
“Nina shaka na utaratibu huo uliotumika wa kuchanganya huduma na biashara, ni lazima mkulima anyanyasike, ni muhimu tubuni utaratibu mbadala,” alishauri.
Awali, madiwani wakiongozwa na Mbunge wa Jimbo la Kahama (CCM), James Lembeli, walidai mbolea hiyo haikuwafikia walengwa kama ilivyopangwa.
Mbolea nyingi ya ruzuku inafikishwa vijijini na walanguzi ambao wanawauzia wakulima kwa sh 40,000 kwa mfuko mmoja badala ya sh 23,000.
Hata hivyo, pamoja na madai hayo, wataalamu wa kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Kahama, walikiambia kikao hicho kuwa, tayari wameishasambaza tani 100.5 katika kata ambazo zilithibitika zina wakulima wa tumbaku, ambao hukopeshwa pembejeo za kilimo na kampuni za tumbaku kupitia vyama vyao vya msingi.
Aidha, baada ya kubanwa na madiwani, Ofisa Kilimo na Mifugo, Isaya Ndaga, alikiri kuwa mawakala waliopewa kazi hiyo wamekuwa wakiuza mbolea hiyo nje ya utaratibu na kisha kutoa takwimu za uongo.