CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) jana kilifanya sherehe za kutimiza miaka 30 ya kuzaliwa kwake katika hali iliyoonyesha mabadiliko makubwa ya kimtazamo miongoni mwa wananchi.
Jijini Dar es Salaam, wanachama na wapenzi wachache wa chama hicho walijitokeza kinyume kabisa na matarajio ya awali.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Jitegemee ndio walioonekana kupamba zaidi sherehe hizo zilizofanyika jana katika viwanja vya Jangwani, na kuongozwa na Mwenyekiti wake wa Taifa, Rais Jakaya Kikwete.
Maadhimisho hayo ambayo kimsingi yalipaswa yafanyike leo, ambayo ndiyo tarehe hasa za kuzaliwa kwa chama hicho, yaliamuliwa kufanywa jana, lengo likiwa ni kuwawezesha wananchi wengi zaidi kujitokeza.
Hii inaweza kuwa ni ishara kwamba wakazi wa Dar es Salaam wamechoshwa na maandamano na shamrashamra, kwani pigo hilo la CCM linakuja siku chache tu baada ya vyama vya upinzani kukumbwa na mkasa kama huo wakati vilipoandaa maandamano yake wiki chache zilizopita.
Wapinzani hao waliokuwa wakishinikiza kuchukuliwa hatua kwa wale wote waliohusika katika kashfa ya ununuzi wa rada, walishtuka kukuta umati mdogo wa watu waliojitokeza kuiunga mkono ajenda yao.
Kwa upande wa CCM jana, maandamano hayo hafifu yaliyoanzia Ubungo na kumalizika katika viwanja vya Jangwani, yalihitimishwa kwa hotuba ya Rais Kikwete.
Katika hotuba yake, Rais Kikwete alibainisha kuwa changamoto kubwa inayolikabili taifa hivi sasa ni namna ya kuwaondoa Watanzania wengi katika hali duni ya maisha.
“Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2005-2010 ndiyo msingi wa kutufikisha katika maisha bora tuliyowaahidi Watanzania,” alisema.
Alisisitiza kuwa, changamoto iliyo mbele, ni kila mwanachama wa chama hicho tawala na kiongozi kuhakikisha kuwa ilani hiyo inatekelezwa.
Kutoka Moshi, Mwandishi Maalumu anaripoti kuwa, Mlezi wa CCM wa Mkoa wa Kilimanjaro, Waziri Mkuu, Edward Lowassa, jana aliwataka wanachama wa chama hicho kutowapa kura wana-CCM waliokisaliti chama hicho wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 30 ya kuzaliwa kwa CCM na kuwapa kadi wanachama wapya wakiwamo waliotokea upande wa upinzani katika eneo la Pasua Sokoni, mjini hapa jana, Lowassa aliwataka wanachama wa chama hicho kuwanyima kura wakati wa uchaguzi wa ndani wa chama hicho utakaofanyika baadaye mwaka huu.
“Wale wana-CCM waliotusaliti, wakiwamo baadhi ya viongozi, tusiwape kura watakapoomba uongozi katika uchaguzi wa chama chetu mwaka huu…mchana wako CCM, usiku wako Chadema…tuwanyime kura,” alisisitiza.
Uchaguzi wa uongozi ndani ya CCM kutoka ngazi ya shina hadi taifa, unafanyika mwaka huu na kuhitimishwa na uchaguzi ngazi ya taifa utakaofanyika Oktoba. Uchaguzi huo hufanyika kila baada ya miaka mitano.
Katika mkutano huo uliofuatia matembezi ya mshikamano ambayo aliyaongoza, Lowassa pia alikabidhi kadi kwa wanachama wapya zaidi ya 2,000 wakiwamo kutoka vyama vya upinzani vya Chadema, CUF na TLP ambao baadhi yao walikuwa viongozi.
Viongozi hao waliohama vyama vya upinzani walisema kuwa wameamua kujiunga na CCM si kwa kuhongwa wala kurubuniwa, ila kwa kuvutiwa na sera za CCM na utekelezaji wake.
“Hatukurubuniwa wala kuhongwa. Sisi tunaohama tunavutiwa na sera nzuri za CCM na utekelezaji wake chini ya Rais Jakaya Kikwete… wengi wengine watarudi,” alisema Consolata Lyimo, aliyekuwa Chadema.
Consolata, ambaye alikuwa akizungumza kwa niaba ya wenzake, alikuwa Katibu Kata wa Chadema na mgombea udiwani wa chama hicho.
Katika hotuba yake, Waziri Mkuu Lowassa, pia alihimiza elimu, hasa ujenzi wa shule za sekondari na uanzishaji wa vyama vya kuweka na kukopa kwa ajili ya kupata “mabilioni” yaliyopelekwa ya kuwawezesha wananchi.