RAIS Jakaya Kikwete ameshangazwa na hatua ya baadhi ya wanasheria na wanasiasa kumlaumu yeye kutokana na kuanza kwa mchakato wa kuundwa kwa Shirikisho la Afrika Mashariki ifikapo mwaka 2013.
Kikwete aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na kamati inayokusanya maoni kuhusu uanzishwaji wa shirikisho hilo, Ikulu jijini Dar es Salaam.
“Wazo la kwamba tuwaachie wananchi waamue kuhusu shirikisho, lilikuwa ni wazo la Tanzania, wenzetu waliona tunapoteza wakati, waliona viongozi wanaweza kuamua tu kuwapo kwa shirikisho. Nawashangaa sana wale wanaosema eti tumekosea kuwashirikisha wananchi,” taarifa iliyotolewa na Ikula jana ilimnukuu Rais Kikwete akisema.
Aliiambia kamati hiyo kuwa, baada ya tume iliyokuwa ikiongozwa na Mwanasheria wa Kenya, Amos Wako kuhusu shirikisho kuja na ‘road map’, “sisi Tanzania tulisema ngoja tuwashirikishe wananchi ili tupate uhakika kwamba wananchi wanaridhika kuwa na shirikisho au la.”
Aidha, katika kile kinachoonyesha kuwa kuna nchi wanachama wanalitaka shirikisho kwa udi na uvumba, Rais Kikwete aliwaeleza wajumbe wa kamati hiyo kuwa, kuna nchi moja (hakuitaja) ilifikia hatua ya kuandaa rasimu ya muundo wa shirikisho bila kuzishirikisha nchi nyingine, achilia mbali wananchi.
“Tulipogundua hili, Rais Mkapa alinituma mimi, wakati huo nikiwa Waziri wa Mambo ya Nje, kwenda Kenya na Uganda, tukawaeleza wenzetu jamani hapana, hivi sivyo tunavyotakiwa kwenda, tukawapa somo, hatimaye wenzetu wakatuelewa. Lakini wenzetu waliona kuwaachia wananchi waamue ni kama vile viongozi tunajivua madaraka,” alisema.
Akionyesha kuwa uamuzi wa kuwashirikisha wananchi hauna lengo la kuwa ghiliba, Kikwete alisisitiza kuwa, maoni yatakayotolewa na wananchi yataheshimiwa, kuzingatiwa na kupewa umuhimu unaostahili.
Akizungumzia kuhusu nafasi ya Zanzibar katika shirikisho, alisema hakuna maslahi ya nchi kama nchi, na kwamba jambo la msingi la kujadili ni namna ya kuisaidia Zanzibar kukuza sekta yake ya uzalishaji ili iwe na bidhaa za kuuza katika soko la Afrika Mashariki.
“Muundo wa sasa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki si sawa na ile iliyovunjika ambayo angalau kulikuwa na maslahi kama nchi, hii ya sasa inazungumzia zaidi soko. Tusipoteze muda kujadiliana nani atafaidika vipi na namna gani. Tujadili namna gani tutaisaidia Zanzibar iwe na viwanda, izalishe bidhaa,” alisema.
Alisema suala la msingi la kujadili ni kuwa Tanzania inaingiaje katika ushirikiano huo chini ya muundo wa muungano wake.
Kuhusu hofu ya wananchi wengi kupoteza ardhi na ajira, Kikwete alisema masuala hayo hayatakuwa katika shirikisho, bali yatadhibitiwa na nchi husika.
Rais Kikwete alitoa maelezo hayo licha ya majuzi kukataa kulizungumzia suala hilo, alipoulizwa na wahariri akisema kwa kuwa suala hilo bado lipo kwa wananchi, ni vema wakaachiwa watoe maoni yao kabla ya yeye kulisemea.
Ili kuhakikisha kuwa kamati inakusanya maoni kutoka kwa watu wengi, Rais Kikwete aliitaka kuhakikisha inakutana na watu wengi kadiri inavyowezekana.
“Ningependa pale mtakapofika kwenye makundi kama vile vyama vya siasa, hakikisheni kwamba mnawapata wanachama wengi wa vyama hivyo, badala ya kukutana na viongozi peke yao,” alisema na kubainisha kuwa, lengo liwe ni kupata mawazo mchanganyiko.
Akitoa ripoti ya kamati hiyo, mwenyekiti wake, Profesa Samuel Wangwe, alisema kazi imekwenda vizuri, ingawa kuna changamoto kubwa kutokana na uelewa mdogo wa wananchi kuhusu suala zima la Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Alisema uelewa mdogo, ambao umeonyeshwa hata na wasomi, umeifanya kamati hiyo kufanya kazi mbili kwa wakati mmoja; kuwaelimisha wananchi na kisha kukusanya maoni na kusababisha ionekane kana kwamba inafanya kazi ambayo si yake.
Utetezi huo wa rais unakuja wakati makundi ya wanasiasa na wanasheria yakionyesha waziwazi kutofautiana na mchakato huo, na kupinga kitendo cha Rais Kikwete kuruhusu hoja ya kuundwa kwa Shirikisho la Afrika Mashariki.
Wengine wamefikia hatua ya kuhoji uhalali wa kikatiba uliompa nguvu Rais Kikwete kuteua tume ya kukusanya maoni kuhusu suala ambalo hatimaye litasababisha kufa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.