Na Mwandishi Wetu
SHIRIKA la Ndege la Emirates limetangaza nafasi za ajira kwa Watanzania na kuwashauri wale wanaohitaji ajira hizo wajitokeze na kuomba kazi hizo.
Limetangaza nafasi hizo katika kampeni iliyozinduliwa katika miji ya Dar es Salaam na Zanzibar, ikifuatia ile ya Novemba mwaka jana ambayo imeliwezesha shirika hilo kupata wahudumu wa ndege.
Katika kampeni hiyo mwishoni mwa wiki, watu zaidi ya 200 wanaosaka ajira katika shirika hilo walijitokeza na kampeni hiyo ilifanikishwa kwa ushirikiano na ubalozi mdogo wa Tanzania uliopo Dubai, Falme za Kiarabu.
Maofisa uajiri waliotoka makao makuu ya Emirates yaliyoko Dubai walitoa mada katika kampeni hiyo kuhusu mazingira ya kazi katika shirika hilo lenye wafanyakazi kutoka mataifa mbalimbali duniani na pia kuhusu maisha ya jiji la Dubai.
Shirika hilo linaajiri watumishi kutoka mataifa 100 duniani na hivi karibuni limetangaza ajira kwa wafanyakazi wapya ili kuendelea kuboresha huduma zake ambazo zimekuwa zikitolewa kwa zaidi miaka 20.
Meneja wa Emirates, tawi la Tanzania, Khalid Al Serkal alisema shirika lake tayari limeajiri wahudumu wa ndani kutoka Tanzania na kwamba limeridhika na utendaji wao wa kazi.
Hata hivyo, Watanzania wanakaopenda kupata ajira katika shirika hilo la Emirates na makampuni yake mengine, wameshauriwa kutuma maombi kupitia tovuti ya shirika hilo la www.emiratesgroupcareers.com