Na Kizitto Noya
SERIKALI imesikia kilio cha wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu nchini cha kutaka iondoe utaratibu wa kuwataka wachangie asilimia 40 ya gharama za masomo yao, ingawa imeeleza kuwa haina uwezo kwa sasa kutekeleza madai hayo.
Rais Jakaya Kikwete alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa suala hilo linahitaji muda wa kutosha kulishughulikia kwa kupitia bajeti nzima ya wizara husika na kuifanyia marekebisho ya msingi.
Kikwete ambaye alikuwa akizungumza na wanavyuo zaidi ya 10,000 kutoka vyuo vikuu mbalimbali jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Diamond Jubilee alisema kuwa utaratibu utakaoangaliwa katika muda huo ni pamoja na kuhakikisha kuwa hakuna mwanachuo atakayeachishwa masomo kwa kushindwa kuchangia asilimia 40.
Kauli ya Rais Kikwete imefuatia mapendekezo ya wanavyuo hao waliyoyatoa katika risala yao kwake kuwa serikali ingeangalia uwezekano wa kuwafadhili wanafunzi wa elimu ya juu kwa asilimia 100 ili kuboresha mazingira ya upatikanaji wa elimu hiyo nchini.
Katika risala hiyo iliyosomwa na Happiness Kaiza, wanavyuo hao waliiomba serikali ifanye utafiti wa kina kubaini wanafunzi wasiokuwa na uwezo wa kuchangia gharama hizo ili iwafadhili kwa asilimia 100.
"Hili linawezekana endapo kutawekwa jitihada za makusudi kuwafuatilia wanafunzi waliosoma kwa ufadhili wa serikali miaka ya nyuma wakaanza kurudisha mikopo hiyo ili iwasaidie wengine," ilisema sehemu ya risala hiyo.
Wanavyuo hao walisema, serikali inapaswa kuboresha utaratibu wa kuwafadhili wanafunzi kwa kuwaondolea asilimia 40 ya michango ya gharama za masomo yao kuwapunguzia mzigo unaowakabili.
Walisema mchango wa asilimia 40 unamfanya mwanafunzi kulipa kati ya shilingi 500,000 na tsh. 1 milioni, fedha ambayo ni vigumu kwa mwanafunzi kuipata kutokana na ukweli kwamba wengi wao wanatoka katika familia maskini.
Katika mkutano huo, wanafunzi hao pia walilalamikia utaratibu wa Bodi ya Mikopo (HESLB) kuwafadhili wanafunzi wa madaraja ya kwanza kwa wavulana na kwanza na pili kwa wasichana wakisema kuwa unawanyima haki wanafunzi wengi waliotakiwa kupata ufadhili huo.
Walisema mara nyingi wanafunzi wanaoweza kupata alama hizo ni wale waliosoma katika shule za kimataifa au seminari na wanafunzi wengi waliosoma katika shule za sekondari za serikali watakosa bahati hiyo kutokana shule hizo kukosa miundombinu ya kuwafanya wafaulu vizuri.
Rais Kikwete ambaye ni mara yake ya kwanza kukutana na wawakilishi wa wanafunzi hao alisema kuwa pamoja na jitahada za serikali kuboresha sekta ya elimu, mabadiliko hayo ya msingi katika elimu ya juu yanahitaji muda kuyafanyia kazi.
"Tupeni muda tuyafanyie kazi, sio muda mrefu tutawajulisha tulichokubaliana. Shabaha yetu ni kuwasaidia wale wote wasiokuwa na uwezo kulipa asilimia 40 wasikose masomo yao.
"Sasa, ili tuwatengenezee mazingira mazuri zaidi tunahitaji muda kwa sababu huwezi kuingiza bajeti mpya leo mwezi Februari, lakini msimamo wa serikali ni kuwawezesha wote wasiokuwa na uwezo kulipa fedha hiyo wasome," alisema Rais Kikwete.
Pia, Kikwete alisema serikali yake inatambua umuhimu wa elimu kwa namna ya pekee na imetenga Sh113.5 bilioni kwa ajili ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, fedha ambayo ni nyingi kuliko bajeti nzima ya Wizara ya Elimu na Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu.
Alisema suala la wanachuo kuchangia gharama za masomo kwa asilimia 40 lilikuja baada ya serikali kuona kuwa imelemewa na mambo mengi, hasa elimu ambayo kwa kipindi kifupi imefikia mafanikio makubwa.
"Kwa kipindi kifupi tumefanikio kufikia asilimia 96 ya mafanikio katika elimu ya msingi na asilimia 79 ya asilimu ya sekoandari, haya yote yalihitaji pesa na ndiyo maana tukawaomba wananchi wachangia huduma za afya, maji na elimu," alisema Rais Kikwete.
Katika mkutano huo, wanafunzi hao walikuwa wakionyesha taswira na nyuso zenye kusubiri Rais Kikwete atamke kuanza mara moja kwa uamuzi wa kuwaondolea kero ya kuchangia asilimia 40.
Wanafunzi hao, ambao walikuwa wakipiga kelele za hapa na pale, zikiwamo wa kuimba wimbo wa hamasa na kumbukumbu kwa Mwalimu Julius Nyerere, hata hivyo walikuwa wasikivu na kusubiri kauli ya Kikwete.