Na Claud Gwandu,Arusha
MWENYEKITI wa chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila amefungua kesi katika mahakama ya Afrika Mashariki akitaka wabunge kutoka Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki(EALA) wasiapishwe.
Katika kesi hiyo namba 2 ya mwaka 2007, Mtikila anapinga kuapishwa kwa wabunge hao akidai kuwa Tanzania ilikiuka vipengele cha 50 na 51 vya mkataba wa kuundwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufungua kesi hiyo, Mchungaji Mtikila, mwenye rekodi ya kushinda kesi za kikatiba, alisema kuwa Tanzania imekiuka vipengele hivyo kwa kuwa ina wabunge 11 katika bunge hilo badala ya tisa kama ilivyoanishwa katika mkataba huo.
Alisema kwa mujibu wa vipengele hivyo, Mbunge wa EALA anatakiwa kuwa katika bunge hilo kwa miaka mitano lakini wabunge wawili wa Tanzania walioingia bungeni hapo Machi 2005 hawajamaliza kipindi cha miaka mitano kinachoelezwa na mkataba wa EAC
Wabunge hao, Dk Norman Sigala na Hulda Kibacha hawakuchaguliwa kurudi bungeni hapo baada ya kufanyika kwa uchaguzi mwishoni mwa mwaka jana, jambo ambalo Mchungaji Mtikila anadai kuwa bado ni wabunge halali wa Bunge hilo.
Sigalla na Kibacha waliingia katika Bunge la Afrika Mashariki kukujaza nafasi za Dk Harison Mwakyembe na Beatrice Shelukindo ambao walijiuzulu kwa ajili ya kugombea katika majimbo kwa ajili ya Bunge la Tanzania. Dk Mwakyembe ni Mbunge wa Kyela wakati Shelukindo ni Mbunge wa Kilindi.
“Hayo ndiyo mambo ya CCM. Wanafanya mambo ya kushangaza sana kwani hata wenzetu wanatushangaa hawa wabunge wawili waliingiaje kwenye uchaguzi wakati muda wao haujaisha, nami nimeamua kufungua kesi hii ili kuadabisha ukiritimba wa CCM,” alisisitiza.
Alidai kuwa kutokana na makosa hayo Tanzania hivi sasa ina wabunge 11 katika bunge hilo badala ya 9 kama ilivyo kwa nchi nyingine wanachama wa EAC, Kenya na Uganda ambazo kila mmoja zina wabunge tisa.
Hata hivyo, Mchungaji Mtikila alisema kuwa kesi hiyo bado haijapangiwa Jaji wala tarehe ya kusikilizwa ingawa alifungua hati ya kutaka kesi hiyo isikilizwe kwa dharura.
Bunge hilo ambalo lilipaswa kuanza shughuli zake Novemba 30, mwaka jana bado wabunge wake hawajaapishwa baada ya wabunge wa Kenya kupingwa mahakamani hapo.
Kesi hiyo iliyofunguliwa mahakamani hapo na Profesa Anyang Nyong na wenzake pamoja na mambo mengine inapinga taratibu zilizotumiwa na Bunge la Kenya katika uchaguzi wa wabunge wa EALA na Mahakama hiyo ilitoa amri ya muda ya kusimamisha kuapishwa kwa wabunge wa Bunge hilo.
Alisema katika kesi hiyo ameomba mahakama iseme kuwa Tanzania ina Wabunge 11 katika mahakama hiyo na iamuru kubadilishwa kwa Mkataba wa EAC ili Kenya na Uganda nazo ziwe na wabunge 11 au Tanzania ifanye uchaguzi mwingine wa wabunge saba watakaoungana na wenzao wawili ili wawe tisa.
Wakati huo huo, Mchungaji Mtikila alisema kuwa chama chake kinajiandaa kwenda Mahakama Kuu ya Tanzania kupinga tume ya kukusanya maoni ya wananchi juu ya Shirikisho la Afrika Mashariki akidai kuwa ni uvunjaji wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mchungaji Mtikila amejijengea umaarufu wa kufungua kesi dhidi ya serikali na kuibwaga mara kwa mara, ikiwemo kesi ya kupinga takrima na kesi ya kutaka mgombea binafsi aruhusiwe nchini.