Na Ramadhan Semtawa
WAKATI timu ya wachunguzi wakifuatilia meli ya Mv Mnazi Bay iliyopotea katika Bahari ya Hindi tangu Januari 23, mmoja wa mabaharia aliyeondokao Dar es Salaam na meli hiyo amejitokeza na kuelezea mlolongo wa safari kabla ya kupotea.
Maelezo yake yanaonyesha kuwapo kwa uwezekano mkubwa wa meli hiyo kuzama katika kina kirefu cha maji na kuua watu wote sita, wakazi wa Kigamboni.
Hata hivyo, timu ya wachunguzi wa tukio hilo iliyoondoka jana asubuhi na inayoundwa na afisa kutoka Mamlaka ya Bandari kitengo cha uokoaji, kutoka Chuo cha Ubaharia (DMI) na Polisi Majini na Sumatra ndiyo itaweka bayana kuhusu sakata hilo.
Baharia huyo, Idd Ally, alisema kabla ya meli hiyo kwenda Kilwa ilitokea Kigamboni Jeshi la Maji (Navy ) ambako ilifanyiwa matengenezo madogo na kupakia boti na jenereta kuelekea Kusini.
"Ilikaa Navy, mara ukapatikana mzigo wa kubeba majenereta kupeleka Songosongo ilipomaliza ikiwa Slipway (Msasani) ilibeba boti iliyofungwa nyuma," alisema.
Alifafanua kwamba walisafirisha mzigo huo hadi Songosongo na kuupakua kisha wakaanza kuelekea Kilwa kuchukua mafuta na maji.
"Tulipofika Kilwa tuliachana na tangu siku hiyo haijaonekana tena," alisema.
Kabla ya kuondoka Kilwa kwenda Songosongo kupeleka mzigo huo kulikuwa na watu nane, lakini yeye na mwingine walishuka na kubaki sita ambao baadaye mmoja wao, inasemekana mwili wake uliokotwa na wavuvi kwenye mwambao wa bahari ukiwa umeharibika.
Meneja Mawasiliano wa Sumatra, David Mziray, alisema jana kwa timu ya watalaam imekwenda Kilwa kufuatilia taarifa za meli hiyo.
Mziray alifafanua kwamba , timu hiyo itafanya uchunguzi huo kwa kuitafuta meli hiyo kwa kutumia vifaa kati ya Kilwa na Songosongo.
Kuhusu taarifa za kwamba meli hiyo imezama na tayari imeua, Mziray alijibu, "hayo yote tusubiri timu ya wataalam ichunguze itatoa ripoti."
Meli hiyo ndogo ya Mnazi Bay ni ya mizigo ina uwezo wa kubeba tani 10 hadi 20 na inamilikiwa na Kampuni ya MS Southern Logistics.
Leseni ya usalama ya Mnazi Bay ilitolewa na Sumatra Novemba mwaka jana na inatarajiwa kumalizika muda wake Novemba mwaka huu.