Waandishi Wetu, Dar na mikoani
RAIS Jakaya Kikwete na Jaji Mkuu, Barnabas Samatta wameyabeza matangazo dhidi ya rushwa yanayotolewa kwenye vyombo vya habari yaidhalilisha mahakama na kuonyesha kuwa mfumo mzima wa mahakama umejaa rushwa.
Wakati Kikwete aliyazungumzia Ikulu jijini Dar es Salaam alipokutana na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari jana, Samatta aliyasema hayo kwenye maadhimisho ya siku ya sheria jana na kufafanua kuwa yamebuniwa kwa lengo la kuwaridhisha wafadhili.
Samatta alisema matangazo hayo yanalenga kuwahakikishia wafadhili kuwa misaada yao inatumiwa ipasavyo, wakati ukweli ni kwamba hayasaidii kuondoa tatizo la rushwa mahakamani.
"Matangazo hayo yamekuwa yakitolewa kama burudisho yanaweza kuwakatisha tama watumishi hao wema hivyo kuwafanya wala rushwa wajione tayari ni washindi katika vita hiyo,” alisema Jaji Samatta katika hotuba yake aliyoitoa jijini Dar es Salaam jana kwenye maadhimisho ya siku ya sheria nchini.
Alisema vita dhidi ya rushwa hasa katika mahakama ikiendeshwa kimzahamzaha, matokeo yake yanaweza kuwa mabaya kwa nchi kwa badala ya kujenga itakuwa ni kubomoa.
Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, alisema kati ya maeneo yanayolalamikiwa na wananchi katika mahakama ni ucheleweshwaji wa kesi.
“Malalamiko hayo yana sura nyingi ikiwa ni pamoja na upungufu wa watumishi, vitendea kazi na majengo, ”alisema.
Kwa upande wake Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Josephat Mackanja, alisema vita dhidi ya rushwa itaimarika iwapo askari wa kitengo cha upelelezi wa jeshi la polisi na Taasisi ya Kuzuia Rushwa (Takuru), watapewa mafunzo ya hali ya juu kuhusiana na rushwa
" Kwa kuwa vita ya rushwa ni ngumu, kila mchukia dhuluma anatakiwa kushirikiana kama askari katika vita hiyo, " alisisitiza wakati akihutubia maadhimisho hayo yaliyofanyika jana mjini Mwanza.
Vilevile aliomba serikali kuangaliwa upya kwa maslahi madogo ya watumishi wa idara ya mahakama ambayo alidai hayakidhi.
Nacho Chama Chama cha Tanganyika Law Society mkoani Morogoro, kinatarajia kuwapatia mafunzo maalum kwa wakazi wa Mkoa huo jinsi ya kushughulikia kesi mahakamani.
Mwenyekiti wake, Cyriacus Binamungu, alisema mafunzo hayo yataanza kutolewa mwezi ujao katika Manispaa ya Morogoro, Wilaya ya Morogoro Vijijini, Mvomero, Kilosa, Kilombero na Ulanga.
Kutoka Dodoma, ilielezwa katika maadhimisho hayo kuwa kesi nane za rushwa zilifunguliwa katika Mahakama ya Mkoa ya Dodoma tangu mwaka 1998 hadi 2006.
Jaji Mfawidhi wa Mkoa wa Dodoma, Joseph Masanche alifafanua kuwa, mwaka 1999 kulikuwa na kesi tano zilizofunguliwa, kati ya hizo, mmoja wa washtakiwa aliachiwa huru na nne kufutwa wakati mwaka 2002 kulikuwa ka kesi tatu ambazo nazo zlifutwa.
Akizungumzia kuhusiana na rushwa ndani ya mahakama, alisema inavyoelekea ni rushwa ya kupokezana visenti vidodo vidogo
jambo ambayo ni kero.
Kutoka mkoani Pwani, watumishi wa serikali na wananchi wametakiwa kubadili tabia kwa kuacha kupokea na kutoa rushwa ili kufanikisha mapambano dhidi ya adui huyo.
Wito huo umetolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa wa Pwani, Amos Fungo wakati wa maadhimisho hayo ambayo hufanyika Februari 1, kila mwaka.
Fungo alisema kila mtumishi wa serikali pamoja na raia hana budi kujenga tabia ya kuchukia na kuona ni mbaya na ni dhambi kwa kutoa na kupokea.
Vilevile aliomba serikali iangalie upya viwango vya mishahara kwa watumishi wa idara ya mahakama ambayo alidai ni vidogo na haviwatoshelezi katika mahitaji yao ya kila siku.