Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Bajeti itaboresha maisha
Bajeti itaboresha maisha
By Habari Tanzania | Published  06/16/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:
Ushuru wa mafuta, mitungi ya gesi, karatasi wapungua
 
Sasa soda, bia, mvinyo, sigara na simu za mkononi juu
 
Wanaokwepa kodi, wasiowasilisha risiti kuadhibiwa zaidi
 
Na Simon Mkina, Dodoma
 
SERIKALI ya Rais Jakaya Kikwete jana ilidhihirisha nia yake ya kuboresha maisha ya kila mwananchi baada ya bajeti iliyosomwa jana bungeni kupunguza ama kuondoa ushuru kwa baadhi ya huduma na bidhaa muhimu.
 
Akisoma bajeti ya serikali kwa mwaka 2006/07, Waziri wa Fedha Zakia Meghji alisema serikali imepunguza kiwango cha ushuru wa mafuta ya taa kutoka sh. 122 kwa lita hadi sh. 52.
 
Sambamba na hatua hiyo, serikali katika bajeti yake hiyo imetenga sh. trilioni moja, milioni nne kwa ajili mishahara, ikilinganishwa na sh. bilioni 682 zilizotengwa katika bajeti ya mwaka 2005/06.
 
Waziri alisema kuwa lengo la kupunguza ushuru huo ni kutoa mwanya kwa wananchi wengi zaidi kutumia mafuta ya taa ikiwa ni nishati mbadala kwa mkaa, hivyo kulinda mazingira.
 
Waziri Meghji, hata hivyo, aliwaonya wafanyabiashara wa mafuta kutotumia mwanya huo wa kupunguzwa kwa kodi hiyo kuongeza ukwepaji kodi kwa kuchanganya mafuta ya taa na petroli. Alisema hatua kali za udhibiti zitaimarishwa zaidi.
 
Sambamba na hatua hiyo, serikali pia imefuta ushuru kwenye mitungi ya gesi ili kuhamasisha matumizi yake na hivyo kulinda mazingira.
 
Aidha, ushuru wa karatasi umepunguzwa kutoka asilimia 25 hadi 10, lengo likiwa ni kutoa fursa ya kupungua kwa bei ya machapisho mbalimbali yakiwemo magazeti na vitabu.
 
Waziri Meghji pia alielezea serikali kutoa msamaha wa ushuru kwa vifaa vinavyotumia mionzi ya jua kuzalisha umeme. Hatua hii itahamasisha wananchi kutumia nishati hii mbadala na kuhifadhi mazingira.
 
Katika kuongeza matumizi ya usafiri rahisi, serikali imefuta ushuru kwa viunganisho vya baiskeli huku ikipunguza ushuru kwa vifaa vya pikipiki. Awali, ushuru wa vifaa vya baiskeli ulikuwa asilimia 10 huku vile vya pikipiki vikiwa asilimia 25.
 
Sambamba na hatua hiyo, serikali pia imefuta ushuru kwenye malighafi zinazotumika kutengeneza vipuri vya magari (oil, air, fuel filters).
 
Hata hivyo, serikali imeongeza ushuru wa bidhaa zisizokuwa za petroli kwa asilimia saba, lengo likiwa kulinda thamani halisi ya mapato ya serikali kwenye vyanzo vyake.
 
Baadhi ya bidhaa hizo ni vinywaji baridi kutoka sh. 41.50 kwa lita hadi sh. 45 kwa lita. Vinywaji vikali navyo vimeongezewa ushuru kutoka sh. 1,216 kwa lita hadi sh. 1,302.
 
Ushuru wa bia inayotengenezwa kwa nafaka ambayo haijaoteshwa imepanda kutoka sh. 150 kwa lita hadi sh. 161 kwa lita.
 
Waziri Meghji alisema bia nyingine zote zimeongezwa ushuru kutoka sh. 256 kwa lita hadi sh. 274.
 
Mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 25, umeongezwa ushuru kutoka sh. 820 kwa lita hadi sh. 878 kwa lita.
 
Sambamba na ongezeko hilo la ushuru kwenye bidhaa za vinywaji, sigara nazo zimepandishiwa kiwango cha ushuru, ambapo sasa sigara zisizo na kichungi na zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa nchini kwa kiwango cha asilimia 75, imepanda kutoka sh. 4,170 hadi sh. 4,462 kwa kila sigara 1,000.
 
Waziri Meghji alisema sigara zenye kichungi na zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini ushuru wake umepanda kutoka sh. 9,840 hadi sh. 10,529 kwa kila sigara 1,000.
 
Pia, ushuru wa bidhaa kwenye huduma za mawasiliano ya simu za mkononi umeongezeka kutoka asilimia tano hadi saba ya mauzo ili kikaribiane na kiwango kinachotozwa kwa nchi jirani za Kenya na Uganda.
 
Katika kuhimiza ulindaji wa mazingira, serikali imeongeza ushuru wa bidhaa za mifuko ya plastiki inayoruhusiwa kutoka asilimia 15 hadi asilimia 120.
 
Pia, serikali kuanzia mwaka wa fedha wa 2006/07, imeongeza ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha asilimia 20 kwa magari madogo chakavu yenye umri wa miaka 10 au zaidi.
 
Katika kuwabana wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu, serikali imeongeza kiwango cha adhabu kwa kosa la kutotoa stakabadhi kutoka sh. 200, 000 hadi sh. 500,000. Wale watakaogundulika kushndwa kuwasilisha fomu za marejesho nao watakumbwa na adhabu ya kulipa kiwango kama hicho cha fedha.
 
Waziri Meghji alisoma hotuba hiyo kwa muda wa saa 1.07 kuanzia saa 10:00 jioni.

How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by Arnold)
    Rating
    Kusomwa kwa bajet ni jambo moja na utekelezaji ni jambo lingine hivyo ingekuwa vyema kusubiri utekelezaji

    Hongera mama Megji
     
  • Comment #2 (Posted by changono)
    Rating
    vyombo vya habari tanzania mmezidi kusifia kila kitu bila kufanya tathmini ya kitaalam, namna hiyo mnachangia kudumaza maendeleo.

    isitoshe mkisifia sana mtashindwa kukosoa kwa manufaa ya kuendeleza nchi.jifunzeni kwa wenzenu, siyo kila kitu lazima kisifiwe.kama na nyinyi ni kitengo cha gazeti la uhuru au radio tanzania ni vyema tukaelewa mapema.
     
  • Comment #3 (Posted by nkurufi)
    Rating
    Wasiwasi wangu ni namna ya udhibiti ushukaji na upandaji wa bei huko kwenye serikali maduka ports na vituo vya mafuta kwa baadhi ya huduma kwa mujibu wa hii bajeti kama utatekelezwa na kusimamiwa kihalali basi mambo yatakuwa supa hata hivyo mawasiliano kwa kuwa ni moja ya miundo mbinu kupanda kwa gharama ya simu za mikononi kutapelekea maisha ya watu wa chini kuwa magumu changamoto kwa vyombo vya habari na watanzania kwa ujumla wetu ni kufwatilia na kutoa taarifa kwa jamii na kuishauri serikali pale mapungufu ya utekelezweji wa bajeti hii mpya yanapotokea mbali na hayo hata hivyo hongera kwa serikali ya kikwete kwa bajeti hii ya ari .. mpya
     
Submit Comment


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.