Na Mwandishi Wetu, Dodoma
SPIKA wa Bunge, Samueli Sitta amemsamehe Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe baada ya kumuamba msamaha katika shauri la kumdharau na kukataa maelekezo yake.
Vile vile Sitta alimtaka Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo, kumuomba radhi Mbunge wa Maswa, John Shibuda, kwa kutomtendea haki kwa kumtuhumu kuwa amesema uongo bungeni na Mbunge wa tarime, Chacha Wangwe kufuta kauli yake kuwa jimboni mwake yametokea mauaji ya kisiasa.
Akisoma maamuzi hayo bungeni jana, mara baada ya kupokea taarifa za kamati mbalimbali alizokuwa amezipa majukumu ya kushughulikia mashauri hayo, Sitta
alimtia hatiani Kabwe kwa kumdharau Spika kuwa hazijui kanuni za bunge kuhusiana na uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki ama alikuwa akizipindisha kwa makusudi.
Alisema kuwa Kabwe alitenda makosa ambayo alistahili kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni za Bunge, na alishindwa kutekeleza maelekezo ya Spika kumtaka amuombe radhi ndani ya siku tano, lakini kwa kuwa baadaye alionesha kujutia kosa lake aliamua kumsamehe.
Spika alisema baada ya kurudi kutoka Ujerumani Kabwe alifanya jitihada za dhahiri za kumtafuta ili kuomba radhi na kwamba kwa kuzingatia kuwa Mbunge huyo alikwenda kwake akiongozana na Mwenyekiti wa Kamati Maadili, Juma Nh'unga na kwamba lilikuwa kosa lake la kwanza aliamua kumsamehe.
Kuhusua Wangwe, Spika alisema kuwa mbali na Wangwe kuthibitisha ukweli wa kauli yake ya kuwepo kwa vitisho, majeraha na mauaji katika jimbo la Tarime wakati wa mchakato wa kampeni za uchaguzi mkuu, lakini alishindwa kuthibitisha kwamba vitendo hivyo vilifanyika kisiasa, hivyo alitakiwa kufuta kauli yake bungeni kabla ya kumalizika mkutano huu wa sita.
Katika shauri jingine la John Shibuda na John Cheyo zilizohusiana na mfuko wa elimu wa wakulima ulivyosaidia ujenzi wa Shule za Sekondari Mkoani Shinyanga, Spika alisema Cheyo alikuwa na haki ya kumtaka Shibuda athibitishe kuwa maneno aliyoyasema bungeni yalikuwa sahii, lakini alikosema kwa kumtuhumu kwenzake kwa kusema uongo.
Katika shauri hilo ambalo Shibuda alipongeza juhudi za ujenzi wa sekondari kupitia mfuko wa maendeleo ya kilimo, Shinyaga kwa kuongeza Sekondari 42 ,Cheyo hakukubaliana na hilo na kusema kuwa Shibuda alikuwa amezungumza uongo na kutakiwa athibitishe kauli yake.
Spika alisema kuwa Shibuda aliweza kuthibitisha bungeni hivyo Cheyo kutia hatiani kwa kutomtendea haki Shibuda na kuamuriwa amuombe radhi kwa kwa njia yoyote ya wazi.
wabunge wote waliohukumiwa walifiakiana na hukumu hizo na hakukuwa na yeyote aliyekata rufaa.
Shauri la nne linalohusu kesi ya Mbunge wa Mkuranga na Reginald Mengi haikutolea uamuzi na Spika alisema ataizungumzia baadaye.