Na Mwandishi Wetu Rais Jakaya Kikwete, jana alirudia tena kauli yake kuwa urais wake hauna ubia na kwamba kama ni ubia basi mbia wake ni Makamu wa Rais Dk Mohamed Shein ambaye kwa pamoja walichaguliwa na wapiga kura kuiongoza Tanzania.
Rais alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa swali katika mkutano wake na wakuu wa vyombo vya habari, uliofanyika jana Ikulu jijini Dar es Salaam kama alipotoa kauli hiyo alilenga kundi gani la watu. “Nilisema wakati fulani kauli hiyo…na siogopi kuirudia tena kuwa kama ni ubia basi ubia wa urais wangu ni na Dk Shein ambaye alikuwa mgombea mwenza na wengine wote tumewateua kutusaidia,” alisisitiza Rais Kikwete.
Rais Kikwete ametoa kauli hiyo huku kukiwa na minong’ono mitaani kuwa wana mtandao wana sehemu kubwa juu ya maamuzi ya ikulu yake kutokana na matukio mbalimbali ambayo baada ya kuenezwa na wana mtandao, huibuka kuwa ya kweli kama vile uteuzi wa viongozi mbalimbali katika ngazi tofouti.
Aidha hapo awali, vikundi vya wanamtandao ambavyo vilijitokeza kwa nguvu kipindi cha uchaguzi mkuu kwa ajili ya kumpigia debe mgombea wao (Kikwete) vilionekana katika vyumba vya habari na kuwa vyanzo muhimu vya ubashiri wa habari ambazo wakati mwingi zilikuwa sahihi.
Hata baada ya ushindi wa Kikwete na maandalizi ya kuundwa kwa baraza la mawaziri wakuu wa mikoa na wilaya, taarifa za awali kutoka kwa wana mtandao zilipenyezwa katika vyombo mbalimbali vya habari na kuwa sahihi kwa asilimia kubwa. Ni kutokana na mazingira hayo baadhi ya wahariri waliohudhuria mkutano huo wanahisi kuwa Rais Kikwete, ametumia nafasi hiyo kuiweka bayana nafasi ya yake ya urais, ili kuwapa tahadhari watu wanaotaka kutumia ukaribu wao kwake kuwa hawako karibu na mamlaka ya urais.