Na Kizitto Noya
UONGOZI wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), unadaiwa kuwa unaangalia uwezekano wa kukopesha wanafunzi wake asilimia 40 ya gharama zote za masomo wanazotakiwa kulipa kwa ajili ya masomo.
Hatua hiyo imekuja baada ya wanafunzi wa vyuo vikuu jijini Dar es Salaam, kuandamana kupinga agizo la Serikali linalowataka wachangie gharama za masomo kwa kiwango hicho.
Habari zilizopatikana chuoni hapo juzi zinadai UDSM kinaangalia uwezekano wa kuwakopesha wanafunzi wake kiasi hicho, ambacho watatakiwa kukirudisha kabla au baada ya kumaliza masomo.
Inadaiwa kuwa, uongozi wa chuo hicho, umekubali kuangalia uwezekano wa kutowadai wanafunzi wake gharama hizo, baada ya kupokea maombi kutoka kwa uongozi wa Serikali ya Wanafunzi Chuo Kikuu Dar es Salaam (DARUSO).
Rais wa DARUSO, Magesa Mwita, alisema suala la chuo kuwadhamini wanafunzi hao kwa asilimia 40 wanayotakiwa kuchangia, bado lipo kwenye mjadala na linahitaji baraka za Baraza la Chuo litakalokutana mwezi ujao.
Afisa Uhusiano Mkuu wa Chuo hicho, Julius Saule, alikataa kuzungumzia chochote kuhusiana na suala hilo kwa madai kuwa sio wakati muafaka.
Alisema madai ya wanachuo kutaka wasichangie gharama za masomo ni ya muda mrefu na tayari serikali imeshatoa uamuzi, hivyo sio busara chuo kuzungumza chochote sasa mpaka hapo itakapopatia ufumbuzi suala hilo.