Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Wabunge wa Uingereza walia na rada ya Tanzania
Wabunge wa Uingereza walia na rada ya Tanzania
By Habari Tanzania | Published  01/1/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
LONDON, Uingereza

BUNGE la Uingereza limeambiwa kuwa mkataba wa uuzaji wa rada wa nchi hiyo kwa Tanzania mwaka 2001, ulitawaliwa na kashfa.

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa zamani wa Maendeleo ya Kimataifa wa nchi hiyo, Clare Short, ambaye aliungana na wabunge wa Chama cha Conservative kumtuhumu Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair, kwa kuruhusu uuzaji wa rada hiyo uliogharimu jumla ya pauni 28milioni (karibu Sh50 bilioni) kupitia kampuni ya BAE Systems.

Kitengo cha Kupambana na Makosa ya Ulaghai (SFO), hivi sasa kinachunguza madai kuwa kampuni ya BAE iliwapa rushwa maofisa wa serikali ya Tanzania.

Short, ambaye hivi sasa ni mbunge wa kujitegemea, alisema Tanzania ingeweza kununua rada hiyo kwa bei ya chini zaidi.

"Ninaamini kuwa pande zote zilizohusika katika mkataba huo zinapaswa kuona aibu," alisema mwanamama huyo wakati wa mjadala wa suala hilo bungeni Jumanne usiku.

Short alisema mkataba huo haufai na ni hatari kwa maslahi ya Tanzania na kwamba ulipingwa na mawaziri waandamizi, akiwemo Waziri wa Fedha, Kansela Gordon Brown.

Alisema benki ya Barclays ilipanga njama kwa kushirikiana na serikali katika kuikopesha Tanzania fedha hizo, lakini ikaidanganya Benki ya Dunia kuhusiana na aina ya rada na kiasi cha mkopo.

Mbunge kutoka Chama cha Liberal Democrats, Lynne Featherstone, alisema Uingereza inapaswa kuwa safi ikiwa inataka kuendeleza ushawishi, heshima au uaminifu duniani.

Waziri kivuli wa Maendeleo ya Kimataifa, Andrew Mitchell, alisema BAE haikueleza ukweli kuhusiana na teknolojia na kwamba rada hiyo haikutosheleza kununuliwa kwa gharama kubwa.

Mitchell alisema kuwa mkataba huo ulikuwa na dalili za tahadhali kwamba bei yake ilipandishwa, rada hiyo haikufaa pamoja na ufadhili wake wenye utata.

"Licha ya kukosolewa na watu mbalimbali wenye uelewa wa mambo, watu wenye kuheshimika na wenye sifa za otoaji wa kibali ulikubaliwa kwa nguvu kupitia Baraza la Mawaziri lililokuwa limegawanywa na Waziri Mkuu," alisema.

Alimuhoji Blair kama wakati wanaikubalia BAE kuiuzia Tanzania rada hiyo, walikuwa wanaelewa kuwa kamisheni ilikuwa ni asilimia 30.

Akijibu hoja za wabunge hao, Waziri wa Maendeleo wa Kimataifa, Hilary Benn, alisema kweli ununuzi wa rada hiyo una harufu ya rushwa, lakini cha msingi ni kusubiri uchunguzi ukamilike.

Hivi karibuni, akihojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Rais Jakaya Kikwete, alisema suala la rada ni aibu ya Uingereza, kwani shirika lililohusika kuuza rada inayodaiwa kupaishwa bei ni mali ya serikali hiyo.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala) Bora, Philip Marmo, awali alilieleza gazeti hili kuwa serikali ilikuwa imeshtushwa na taarifa hizo, baadaye akasema wao hawawezi kulichunguza wanasubiri Uingereza ikamilishe uchunguzi wake.

Naye Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, alizibeza taarifa za uchunguzi wa tuhuma za rushwa unaofanywa na Uingereza kuhusiana na tuhuma kwamba Tanzania ilihongwa, ili inunue rada kuwa hayo ni maneno ya Wazungu.

Aliitaka Uingereza iisaidie Tanzania kutaja maafisa wa serikali waliohongwa na kulishawishi Bunge ili lipitishe fedha za kununulia rada hiyo.

Hivi karibuni, hazeti la The Guardian la Uingereza lilichapisha taarifa kuwa raia mmoja wa nchi hiyo anayeishi Tanzania, amekiri kupokea kwa siri kamisheni ya asilimia 30 ya thamani ya rada hiyo na fedha hizo kuingia katika akaunti yake nchini Uswis.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.