Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Kufungiwa HakiElimu serikali yajipalia mkaa
Kufungiwa HakiElimu serikali yajipalia mkaa
By Habari Tanzania | Published  02/1/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:

Aloyce Geofrey na Leon Bahati

WASOMI na wasasiasa wamesema kwamba serikali imevunja haki za kidemokrasia kwa kuyafungia matangazo na machapisho yote ya Shirika lisilo la kiserikali la HakiElimu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam jana, baadhi ya wanasiasa na wasomi hao waliionya serikali kuwa inatumia ubabe na inakwenda kinyume na haki za kikatiba.

Walikuwa wanatoa maoni yao kufuatia Ofisi ya Waziri Mkuu kutishia kulichukulia hatua kali za kisheria HakiElimu, iwapo litaendelea kutoa machapisho na matangazo yahusuyo shughuli za elimu nchini, kwa madai kuwa kila shirika hilo linapochapisha neno, picha au filamu linakiuka sheria.

Mkuu wa Idara ya Elimu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Peter Chonjo, alisema ameshtushwa kusikia kwenye vyombo vya habari jana asubuhi kuwa HakiElimu imefungiwa tena na serikali.

“Mimi kwa mtazamo wangu matangazo ya HakiElimu yanaielimisha jamii na pia yanachochea utendaji kazi bora wa idara mbalimbali serikalini, hivyo kinachofanywa na taasisi hii ni kuwaasa viongozi wasiwe wababishaji,” alisema Profesa Chonjo.

Alisema anakumbuka wakati wa uongozi wa aliyekuwa Waziri wa Elimu na Utamaduni, Joseph Mungai, tatizo hilo lilikuwepo na ilionekana kuwa serikali kupitia wizara hiyo inalikandamiza shirika hilo ili lisiweze kueleza mabaya yanayotokea katika wizara hiyo.

“Ninachokiona hapa ni kwamba, hawa HakiElimu wanafanya kazi nzuri ya kuweka wazi mambo mabaya na madhaifu yaliyopo katika sekta ya elimu nchini,” alisema Profesa Chonjo.

Alieleza kuwa yeye anaamini kuwa lengo la HakiElimu sio baya, na akashauri kama serikali imeona kuna ubaya ndani yake, basi itakuwa ni busara kuwaita na kuwaonya kuhusu huo ubaya ama tangazo ambalo limeonekana kuwa ni baya na linagusa maslahi ya jamii.

Mhadhiri Msaidizi katika Kitivo cha Sheria wa UDSM, Baraka Kanyabuhinya, alisema neno ‘maslahi ya jamii’ ni neno ambalo mara nyingi limeleta utata katika tafsiri na matumizi yake na wakati mwingine limetumika vibaya.

Alisema yeye haoni ubaya wa matangazo, ama vitu vinavyofanywa na HakiElimu, kwa mfano hata katika uhuru wa habari, mwananchi ana haki ya kupata taarifa, hivyo kwa kuifungia kunakiuka haki ya mtu kusikilizwa ama kutoa maoni.

“Unaposema kuwa jambo fulani linagusa maslahi ya jamii ni vizuri usiishiie hapo, bali ueleze hayo maslahi ya jamii ni yapi hasa. Kwa mfano unapomuondoa mtu kwenye eneo lake kwa sababu unataka kujenga shule, hapo utaeleweka na kisheria huwa unamlipa fidia,” alifafanua Kanyabuhinya.

Mhadhiri mwingine, Dk Johannes Mutanyata wa Kitivo cha Elimu UDSM, alisema inafaa Haki Elimu waachwe huru wafanye kazi yao, na kama serikali imeona kuwa wamekosea, basi watoe maelezo ya kitaalam kuthibitisha hilo.

“Kama HakiElimu imetamka jambo kwa makosa basi ni wajibu wa serikali kulikanusha kitakwimu ili kuuthibitishia umma kuwa hilo ni kosa na sio kusema tu maslahi ya jamii,” alisema Mutahinywa.

Wakati wasomi wakitoa maoni hayo, baadhi ya wanasiasa wameiunga mkono taasisi hiyo na kupingana na uamuzi wa serikali wa kuiziba mdomo.

Naibu Katibu Mkuu (Bara) wa Chama cha Wananchi (CUF), Wilfred Lwakatare, alisema serikali imelishughulikia suala la HakiElimu kibabe na hiyo “inadhihirisha wazi kwamba serikali isivyopenda kukosolewa.”

“Serikali wakati wote inapenda kusifiwa sifiwa tu, lakini pale inapotokea taasisi za kijamii zikaishika pabaya kwa kufunua pale penye uvundo, kitakachotokea ni kukemewa vikali pamoja na kupewa vitisho,” alisema Lwakatare.

Alisema kama serikali ingekuwa inatekeleza wajibu wake kikamilifu kama inavyojieleza kwa wananchi kuwa inaendeshwa kwa uwazi, inawajali wananchi, inahimiza utawala bora, basi ingeipongeza harakati za HakiElimu na kuwapa moyo wa kuongeza bidii katika kufunua utendaji mbovu katika elimu.

Aliihadharisha HakiElimu kuwa isijihangaishe kutaka kuingia kwenye mazungumzo na serikali katika kutafuta maridhiano, kwa madai kwamba itafumbwa mdomo ili isiendelee kufunua uozo wa watendaji wake katika utekelezaji wa mipango ya elimu nchini.

“Ninachoishauri HakiElimu ni kwamba izibe masikio na badala yake iendelee kuchapa kazi zake kama kawaida kwa sababu zipo ndani ya Katiba ya nchi,” alisema Lwakatare.

Katibu Mwenezi wa Chama cha NCCR-Mageuzi Taifa, Joseph Selasini, alisema kwamba nchi yoyote yenye demokrasia haiwezi kukataa maoni ya watu hata kama ni machungu kama shubiri.

“Tamko la Umoja wa Mataifa juu ya haki za binadamu linatamka uhuru wa kutoa na kupokea habari. Tanzania imeridhia na kutia saini tamko hilo, lakini kinachoonekana wao ndio wanaolivunja,” alisema Selasini.

Aliitetea HakiElimu akisema kwamba machapisho na matangozo yake ambayo walikuwa wanayatoa kupitia redio na televisheni yalikuwa ya ukweli kwa sababu ni mambo ambayo yamekuwa yakijirudiarudia katika mfumo wa utendaji kwenye sekta ya elimu.

Alitoa mfano wa tangazo linalohusu mwalimu aliyekopa fedha ya nauli aende mjini kuchukua mshahara wake na alipofika akakuta bado haujaingia kwenye akaunti yake ya benki na kuanza kujishauri namna atakavyomweleza aliyemkopesha, kwamba halina ubishi kwani ni jambo linalowakuta walimu wengi.

Ukweli huo aliuelezea kuwa ndio uliomfanya Rais Jakaya Kikwete aingilie kati na kuamuru watendaji wahakikishe kuwa walimu wanapata mishahara yao tarehe 23 kila mwezi.

Kinachojitokeza katika sakata hili, Selasini alisema, ni mgogoro kati ya serikali na wananchi, hivyo akaishauri HakiElimu kwenda mahakamani ili kuitaka ifafanue juu ya ukandamizaji huo.

Desemba 5, mwaka jana, Ofisi ya Waziri Mkuu ililiandikia shirika hilo, ikilitishia kuwa italichukulia hatua kali za kisheria iwapo litaendelea kufanya au kuchapisha tafiti kuhusu shule, kuandaa na kuruhusu filamu ama matangazo katika redio na televisheni pamoja na kusambaza machapisho mashuleni kwa sababu yanakiuka sheria na maslahi ya jamii.

Hii ilikuwa ni mara ya pili kwa serikali kuikemea HakiElimu, kwani Septemba 8, 2005, iliyokuwa Wizara ya Elimu na Utamaduni katika serikali ya awamu ya tatu ambayo sasa inajulikana kama Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, ilikuwa imeipiga marufuku kutoa matangazo na machapisho yaliyodaiwa kuidharirisha sekta ya elimu.

HakiElimu ni shirika la hiari lenye usajili halali wa kisheria, linalolenga kufikia usawa, ubora haki na demokrasia katika elimu na jamii, kwa lengo la kuiwezesha jamii kupata habari, kubadili shule na mfumo wa uundaji wa sera, kuibua mijadala, tafiti, uchambuzi wa sera na kushirikiana na wadau kwa manufaa ya pamoja kwa kuzingatia haki za jamii.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by A.H.Kinabo)
    Rating
    Mambo mengi huwezi kuyaelewa kama uko nje ya mfumo.Wengi tungetaka kujua ukweli halisi kama inawezekana.
     
Submit Comment


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.