Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Serikali yainyamazisha tena HakiElimu
Serikali yainyamazisha tena HakiElimu
By Habari Tanzania | Published  01/31/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:

Na Leon Bahati

OFISI ya Waziri Mkuu imepiga marufuku machapisho na matangazo yanayotolewa na Shirika lisilo la Kiserikali la HakiElimu kupitia vyombo vya habari na kutishia kulichukulia hatua kali za kisheria iwapo litakiuka amri hiyo.

Hatua hiyo imeelezwa na shirika hilo kuwa ni ya ukandamizaji inayolinyima haki ya kikatiba ya uhuru wa maoni na kujieleza.

Onyo la kutishia kuichukulia hatua kali za kisheria HakiElimu pamoja na Mkurugenzi wake Mtendaji, Rakesh Rajani, limo katika barua iliyoandikwa na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Vincent Mrisho, Desemba 5 mwaka jana.

"Tumekuandikia kukukumbusha kwa mara nyingine tena kwamba machapisho na matangazo yako ambayo yamekuwa yakitolewa kwenye redio, televisheni na vyombo vingine vya habari yalipigwa marufuku na serikali kwa kuwa kinyume na maslahi ya jamii," inaeleza sehemu ya barua hiyo ikionya kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa ukiukwaji wa amri hiyo.

Hii ni mara ya pili kwa serikali kutoa tamko la kupiga marufuku HakiElimu kufanya au kuchapisha tafiti kuhusu shule, kuandaa na kurusha filamu au matangazo katika redio na televisheni na kusambaza machapisho mashuleni.

Onyo la awali lilikuwa limetolewa na aliyekuwa Waziri wa Elimu na Utamaduni, katika serikali ya awamu ya tatu, Joseph Mungai, Septemba 8, 2005.

Akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa HakiElimu, Elieshi Lema, alisema kwamba wameshangazwa na barua hiyo ya ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuwa imekuja wakati wanafanya juhudi za kukutana ana kwa ana, ili kufanya maridhiano na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

Alisema kwamba HakiElimu imefanya mawasiliano ya barua pamoja na mawasiliano ya simu kwa zaidi ya mara 100 na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi tangu 2005 kuomba kufanya mazungumzo ya kumaliza tofauti zao, hivyo barua ya Ofisi ya Waziri Mkuu imekuwa kama msumari wa moto kwenye kidonda.

"Hatua hizi ni sawa na ukandamizaji. Zinaididimiza na kuinyima HakiElimu haki yake ya kikatiba ya uhuru wa maoni na kujieleza," alisema Lema na kufafanua:

"Siku zote tunaamini kuwa mjadala huru ukiongozwa na sheria na misingi ya demokrasia, utasaidia serikali na HakiElimu kufikia ufumbuzi na maelewano."

Alisema kuwa HakiElimu haijakata tamaa na wakati wote ipo tayari kukaa meza moja na serikali kwa kuwa lengo lao ni kutoa mchango wake wa kuisaidia serikali kuiboresha elimu nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Helen Kijo Bisimba ambaye piya ni mjumbe muanzilishi wa HakiElimu alisema kwamba maonyo hayo yanapingana na mpango mzima wa serikali ya Awamu ya Nne ya unaosisitiza suala la uwajibikaji.

"Kuna mkanganyiko kwa sababu wakati Rais (Jakaya) Kikwete alisisitiza hataki mtu ampake mafuta kwa mgongo wa chupa na badala yake akitaka akosolewe wakati wengine tunazibwa pumzi, hii inatoa ujumbe gani?" alihoji Bisimba.

Mjumbe mwingine, Mary Lusimbi, alisema kuwa kinachoonekana sasa ni kwamba serikali inaingilia uhuru wa mashirika yasiyo ya kiserikali.

Jenerali Ulimwengu ambaye pia ni mjumbe mwanzilishi wa HakiElimu, alisema kwamba mtiririko wa matukio ya kulifungia shirika hilo yanaweza kumfanya mtu kutafsiri kuwa serikali inaongozwa kwa mtindo wa kifashisti na kidikteta.

Ulimwengu alisema elimu ni suala nyeti katika nchi na kwamba wananchi wakipatiwa elimu bora ni jambo la muhimu katika maendeleo ya nchi, jambo ambalo HakiElimu inalipigania.

Alisema suala la kuboresha elimu hapa nchini limekuwa likizingatia zaidi ujenzi wa madarasa na madawati, lakini ukweli ni kwamba "maana ya shule ni kile kinachotendeka kati ya mwalimu na mwanafunzi."

Tangu kuibuka kwa mgogoro huo kati ya HakiElimu na serikali wadau na wananchi mbalimbali walionekana kuipinga serikali kwa uamuzi wake na kuiunga mkono taasisi hiyo, wakisema inachofanya ni kuonyesha ukweli katika masuala mbalimbali hasa yanayoihusu elimu.

Hivi karibuni, HakiElimu ilisitiza matangazo yake mawili yaliyokuwa yanapigania kucheleweshwa kwa mishahara ya walimu baada ya serikai kutangaza kuwalipa kila tarehe 23 kila mwezi.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.